Bondia nyota nchini wa ngumi za kulipwa nchini, Francis Cheka atapigana na bondia wa Uingereza, Martin Murray katika pambano maalum lisilo la ubingwa la uzito wa Super Middle.
Pambano hilo limepangwa kufanyika mjini Manchester Septemba 19 na maandalizi yake yamekwisha kamilika.
Meneja mpya wa bondai huyo, Juma Ndambile alisema kuwa Cheka ataondoka hapa nchini Septemba 15 kwenda Uingereza kwa ajili ya pambano hilo la raundi 10.
Ndambile ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Advance Security alisema kuwa ameamua kuingia mkataba wa mwaka mmoja na Cheka ili kuresha heshima yake katika mchezo huo na pambano la Uingereza ni la mtoano kwa ajili ya kuwania ubingwa wa Dunia.
Alisema kuwa Cheka anatakiwa kushinda pambano hilo ili kusaini mkataba mnono wa zaidi ya dola za Kimarekani 25,000 (Sh milioni 50) ili kupigana katika pambano linalofuata la ubingwa. Alisema kuwa endapo atashinda pambano hilo, atasaini mkataba mwengine za zaidi ya dola 25,000 ili kupigana pambano la tatu.
“Lengo ni kumfanya bondia bora ili hata akiachana na masumbwi ya kulipwa, awe na maisha mazuri, chini yangu pia nitamfundisha jinsi ya kuwekeza katika biashara na kujipatia kipato, nilisikitishwa sana matatizo aliyopata,” alisema Ndambile.
Alisema kuwa Cheka amekuwa na heshima kubwa hapa nchini na ghafla heshima hiyo kupotea kutokana na mambo ya ‘kidunia’ na yeye ameakua kumkwamua kabisa.
Cheka alisema kuwa amefurahi sana kupata meneja mpya ambaye tayari amemtafutia pambano nje ya nchi na sasa imebakia kwake ni kufanya kazi tu. “Ndambile amenilipia kambi ya zaidi ya Sh milioni 2 hapa jijini, nakaa mimi na kocha wangu, naahidi kufanya vyema kwenye pambano hilo,” alisema Cheka.
0 comments:
Post a Comment