Wednesday, August 26, 2015

CHADEMA YAWAKATIA RUFAA WALIOPITA 'KIULAINI'

Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimekata rufani katika majimbo matatu ya Bumbuli, Mlalo na Ludewa baada ya pingamizi zake kutupiliwa mbali.

Pingamizi hizo zilitupiliwa mbali na Wasimamizi wa Uchaguzi wa Majimbo hayo na hivyo kuwatangaza wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamepita bila kupingwa. Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwanasheria wa Chadema, Peter Kibatala, alisema tayari wamewasilisha rufani na wanasubiri uamuzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) na wanaamini haki itatendeka.

Alisema Jimbo la Ludewa, Msimamizi wa Uchaguzi, alidai kwamba katika fomu ya mgombea wa Chadema haikuwa na fomu namba 10, huku mgombea akisema aliwasilisha kila kitu kinachohitajika ikiwamo fomu hiyo.

Kibatala alisema baada ya kufuatilia, ofisi ya msimamizi ilibaini kwamba wao ndiyo walifanya uzembe katika kuihifadhi. Alisema sababu za kutupiliwa mbali pingamizi katika majimbo mengine, hazikuwa na msingi hususan Majimbo ya Bumbuli, Mlalo, Peramiho, Handeni Mjini na Chalinze na hivyo kulazimika kukata rufani.

Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu, alisema sababu za wasimamizi wa uchaguzi katika majimbo hayo kutupa pingamizi hizo, siyo za msingi na inaonekana wamepanga kuwabeba wagombea wa CCM wapite bila kupingwa.

Akizungumza na Nipashe, Mkurugenzi wa Uchaguzi Nec, Ramadhani Kailima, alisema hakuwapo ofisini wakati rufani hizo zinapelekwa, lakini alisema anaamini zitafanyiwa kazi.

“...lakini kama wamesema wameleta, yamepokelewa na yatafanyiwa kazi kwa mujibu wa sheria.

Nec ndiye muamuzi wa mwisho katika suala hilo na ikishatoa uamuzi hauwezi kupingwa popote ikiwamo mahakamani labda yawe ni jinai yanayohusisha matusi au rushwa,” alisema.

KUZINDUA KAMPENI JUMAMOSI
Na katika hatua nyingine, Mwalimu alisema Ukawa watazindua kampeni zake Agosti 29, mwaka huu katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam.

Akizungumzia sababu za awali kutaka kuutumia Uwanja wa Taifa katika uzinduzi huo, alisema ni za kiusalama, idadi kubwa ya wafuasi wao.

Hata hivyo, alisema wameshangazwa na serikali kuwanyima uwanja huo kwa kutumia kigezo ya mihemko mikubwa ya kisiasa na kwamba kitendo hicho ni muendelezo wa kuminya demokrasia nchini.
#CHADEMA Blog

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI