JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA TAIFA YA UKAGUZI
OFISI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali inapenda kuujulisha Umma kuwa Ukaguzi Maalum wa akaunti ya Tegeta Escrow ambao unafahamika kama Ukaguzi wa IPTL unaendelea na unaongozwa na Hadidu za Rejea (ToR) zilizotolewa na kisha kuridhiwa na Ofisi ya Bunge na Wizara ya Nishati na Madini.
Ukaguzi wa akaunti ya Tegeta Escrow uliombwa na Katibu wa Bunge na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini. Ukaguzi huu unalenga kufanya uchunguzi wa kina ambao utatoa taarifa kamili yenye kuonesha hali halisi kuhusu miamala (transactions) kwenye akaunti maalum ya Tegeta Escrow kisha kutoa taarifa kuhusiana na ukaguzi huo.
Kwa kuwa Hadidu za Rejea pekee haziwezi kuonesha ukubwa wa kazi bali utekelezaji wa kazi yenyewe ndio unaoweza kutoa taswira halisi, ni vyema umma wa watanzania ukatambua kuwa Ukaguzi huu haujaweza kukamilika kwa kipindi kilichokadiriwa awali hivyo ukaguzi unaendelea kwa kuzingatia Hadidu za Rejea na kifungu cha 29 cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma Na. 11 ya mwaka 2008.
Aidha, ongezeko la muda wa kukamilisha ukaguzi huu limetokana na uhitaji wa kukusanya maelezo yanayoendana na vielelezo vinavyojitosheleza ili kumsaidia mkaguzi kufikia malengo ya ukaguzi huo.
Ukusanyaji wa taarifa hizo unategemea wahusika kutoka Taasisi za Serikali, Mashirika ya Umma na taasisi na Watu binafsi waliopo nchini na nje ya nchi ambao ni wadau katika suala hili.
Hata hivyo licha ya changamoto zilizoainishwa hapo juu, ukaguzi wa IPTL unaendelea na muelekeo ni mzuri kwa sababu ni maeneo machache tu yaliyobakia ambapo yatakapo kamilika tutawasilisha ripoti kwa taasisi zilizouomba ukaguzi huu kwa mujibu wa Sheria.
Aidha, tunaendelea kupata ushirikiano mzuri kutoka kwa wadau wa ukaguzi huo. Ifahamike kuwa ukaguzi bado unaendelea hivyo itakuwa ni kinyume na utaratibu kwa Ofisi hii kuzungumzia kwa kina taarifa ya ukaguzi wa IPTL kwa sasa.
Ofisi hii itaendelea kutekeleza majukumu yake yote kwa kuzingatia misingi ya uwazi na uwajibikaji usiokiuka taratibu za kisheria katika kukusanya na kutumia rasilimali za umma.
Imetolewa,
Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano
Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi.
0 comments:
Post a Comment