KUMEKUWA na maswali yasiyo na majibu miongoni mwa jamii kwamba imekuaje vijana
wa kiume wamekuwa ni waongo sana hasa linapokuja swala la kuoa? Kwa kadiri siku
zinavyozidi kwenda ndivyo ambavyo idadi ya wanaume wanaoogopa kuoa inazidi
kuongezeka.
Utakuta
wapenzi wanaambiana kwamba wanapendana na kuahidiana kuwa wataoana, lakini
kitakachotokea baada ya hapo ni mwanaume kuanza kupiga chenga kwa visingizio
lukuki.
Kwa
nini hali hiyo hutokea? Ukweli ni kwamba hakuna jibu la moja kwa moja juu ya
tatizo hilo, lakini yapo mambo ambayo yanaweza kutupa angalau tafakuri.
Nitajaribu kudadavua baadhi ya sababu
zinazowafanya wanaume siku hizi kukwepa kuingia katika taasisi ya ndoa:
1 Ukosefu wa mtu wa kumchukulia kama mfano:
Hapa
nawazungumzia wale watoto wa kiume waliolelewa malezi ya upande mmoja yaani
walilelewa na mama peke yao. Sina maana ya kudharau au kutweza malezi ya mama,
la hasha, lakini ni vyema mkafahamu kwamba kuwa na baba asiye na malezi mazuri
si sawa na kutokuwa na baba.
Na ndio
maana nikasema ukosefu wa mtu wa kumchukulia kama mfano. Achilia mbali aina ya
malezi atakayoyapata kwa familia yawe mazuri au mabaya lakini lazima kutakuwa
na tabia za kiume zitakazoakisi malezi ya mtoto wa kiume katika familia husika.
Watoto
waliolelewa na mama peke yao kuna kitu huwa wanakosa, kwani wanakuwa hawana mtu
wa kumchukulia kama mfano kwa upande wa jinsia ya kiume na hapo ndipo hujikuta
wakijifunza wenyewe namna ya kuongea na kutenda kama wanaume kwa sababu katika
makuzi yao hawakupata fursa ya kuwa karibu na baba zao.
Kwa
kuwa siku hizi kuna kundi kubwa la kina mama ambao wamejikuta wakiachiwa mzigo
wa malezi ya watoto, baada ya aidha kuachwa na waume zao au kuzalishwa na
kutelekezwa (Single mothers), na hapo ndipo tunaposhuhudia mtoto wa kiume
anapokua kwa umri na kimo huku akiwa hana mtu wa kumuangalia kama mfano wa mume
anavyotakiwa kuwa katika familia zaidi ya kujifunza mambo hayo kupitia katika
TV, senema au miziki.
Wanaume
waliopitia malezi ya aina hii huchelewa sana kuoa kwani huyaangalia maisha ya
ndoa kwa namna ya kujaribu na ndipo hapo wengi huishia kuishi kinyumba na
wanawake kwa ajili ya kutaka kujifunza namna ya maisha ya ndoa yanavyotakiwa
kuwa na ndio sababu huchukua muda mrefu kufanya maamuzi. Na mara nyingi huishia
kubadilisha wanawake kutokana na kutokuwa na uhakika wa kile wanachokitafuta.
2 Mgogoro wa kiuchumi:
Kuna
kundi kubwa la vijana siku hizi hawana ajira au hawana uhakika na kipato.
Ukweli ni kwamba hakuna mwanaume atakayependa kujiingiza kwenye ndoa wakati
hana kazi au hana uhakika na kipato chake.
Na hiyo
ni kutokana na wanawake wengi siku hizi kuonekana kujali zaidi wanaume wenye
uhakika na kipato. Hii misemo ya wanawake ya kebehi dhidi ya wanaume wasio na
ajira au kipato, kama vile "mwanaume suruale" ina mchango mkubwa sana
katika kuwafanya wanaume kukwepa kuoa iwapo hawana ajira au hawana uhakika na
kipato chao.
3 Wanawake wengi kuwa na kiwango cha elimu
ya juu:
Siku
hizi wanawake wengi wameibuka katika kutafuta elimu ya juu kwa juhudi kubwa.
Idadi ya wanawake wanaojiunga na vyuo vikuu ni wengi tofauti na ilivyokuwa
zamani.
Na hiyo
ni kutokana na wazazi wengi kubadili mtazamo wao juu ya mtoto wa kike. Zamani
mtoto wa kike alichukuliwa kama kitega uchumi.
Kwa
maeneo ya vijijini na katika familia masikini, watoto wa kike walikuwa
wanatazamwa kama, 'biashara ya kesho' ambapo watauzwa kwa njia ya mahari. Kwa
hiyo thamani yao ilikuwa ni kuolewa, ni ile ya kibidhaa na sio kibinadamu.
Lakini
tofauti na zamani siku hizi hata kule vijijini kumekuwa na mwamko mkubwa sana
wa kumsomesha mtoto wa kike hadi elimu ya juu. Kutokana na mwamko huo wanawake
wengi wamejikuta wakiona elimu kama kimbilio pekee la kuepukana na mfumo dume.
Mwanamke
gani atakubali kunyanyaswa na mwanaume akiwa na elimu yake na labda pia akiwa na
kazi yake yenye mshahara na marupurupu ya kutosha, naamini watakuwa ni wachache
sana ambao hawajiamini au waliathiriwa na malezi.
Kwa
upande wa wanaume nao, wamejikuta wakiwaogopa wanawake hawa wenye elimu ya juu
kwa hofu ya kuzidiwa kipato na labda kukosa sauti kama mwanaume na hiyo
inatokana na ego tu.
4 Wanaume huwaona wanawake kama tishio
wanapokuwa na mafanikio makubwa kifedha:
Inaweza
kutokea mwanaume anaweza kuwa na uhusiano na mwanamke ambaye labda tu nisema ni
mbangaizaji. Wakati huo anaweza kuahidi kufunga ndoa na mwanamke huyo, lakini
iwapo itatokea mwanamke huyo akapata mafanikio kibiashara na kuinuka kifedha.
Kama
mwanamke asipokuwa makini anaweza kusababisha mwanaume huyo akaingia mitini.
Sababu kubwa hapo inaweza kuwa ni hofu ya kuogopa kuongozwa na mwanamke.
Kumbuka kwamba mfumo dume bado umetawala vichwani mwa wanaume wengi kutokana na
malezi.
Mwanaume
asiyejiamini ni vigumu sana kwake kuoa mwanamke aliyemzidi kipato. Kwa sababu
akifanyiwa jambo dogo tu, inakuwa kama ametoneshwa. Atahisi kutaka kutawaliwa
na mwanamke huyo. Jambo ambalo wanawake wanatakiwa kulifahamu ni kwamba kila
mwanaume anataka kutambuliwa na kuheshimiwa kama shujaa kabla ya kumfuata
msichana.
Iwapo
utakuwa umesimama iwe ni kifedha au kielimu pale unapotafuta kupata mwenza,
inabidi ujishushe sana la sivyo utadoda.
5 Wanaume wengi siku hizi wana hofu ya majukumu,
hasa ya kulea watoto:
Kutokana
na malezi yao au kile wanachokijua kuhusu watoto, baadhi ya vijana huamini
kwamba, kulea watoto ni jambo gumu sana. Lakini wengine wanaamini kwamba, hata
mke anapaswa kulelewa kama ilivyo kwa mtoto. Hivyo wanaamua kutafuta kwanza
uwezo ambao haupatikani kiurahisi.
Kuna
wengine, ambao wamefundishwa au kuelekezwa na mila na desturi zao kwamba, kabla
hawajaoa, ni lazima wawe na nyumba kwanza, tena kwao. Kwa hiyo, hawa hadi waje
wapate uwezo wa fedha wanakuwa wameshachelewa.
6.Kuna baadhi ya wanaume, maisha bila ya
ndoa wanayaona kuwa ndiyo bora kuliko yale ya ndoa:
Kuna
baadhi ya wanawake hujirahisisha sana kwa wanaume. Siku hizi ni jambo la
kawaida sana kukuta mwanaume anaishi na mwanamke bila ndoa, wenyewe wanaita
Trial Marriage.
Na hapo
ndipo unapokuta wanaume hawaoni tena umuhimu wa kuoa. Sasa kama mwanamke
anaweza tu kuishi na mwanaume bila ya ndoa na mwanaume huyo akapata huduma zote
kutoka kwa mwanamke huyo, unadhani ni kitu gani kitamvuta kufunga ndoa. Jambo
lingine ni ile dhana kwamba maana ya ndoa ni tendo la ndoa.
Siku
hizi wanaume wengi wamejikuta wakiwa hawahitaji tena kuoa kwa sababu tendo hilo
linapatikana kiurahisi tofauti na zamani. Siku hizi inawezekana kabisa
kumtongoza binti leo na kupata tendo siku hiyo hiyo…..
hapa
siwazungumzii makahaba. Nawazungumzia mabinti zetu ambao wengine ukiwaona ni
watu wa kuheshimiwa ukiwaangalia kwa nje lakini kwa ndani hawana lolote, vijana
wa siku hizi wenyewe huwaita maharage ya Mbeya.
Kuna
sababu nyingi zinazotajwa kusababisha wanaume siku hizi kujivuta sana katika
kufanya maamuzi ya kutafuta mwenza. Lakini hizo chache nilizozitaja zina
mchango mkubwa.
0 comments:
Post a Comment