Wednesday, October 15, 2014

ASKOFU KIJANJALI ASHIRIKI UZINDUZI WA KITUO CHA WALEMAVU KARAGWE WENYE THAMANI ZAIDI YA SHILINGI BILIONI 1.5

Na Hilali Alexander Ruhundwa wa Ulimwengu wa Habari, Kagera.
************
KANISA la Anglikana Dayosisi ya Kagera kupitia kitengo chake cha kuhudumia watu wenye ulemavu KCBRP wakishirikiana na wadau wengine wamezindua mradi wa ujenzi wa Kituo cha utengamavu, mikutano na mafunzo katika kata ya Ndama wilayani Karagwe; kituo kinachotarajiwa kuwasaidia watu wenye ulemavu mkoani Kagera.
Katibu mtendaji wa KCBRP Bwana Agrey Mashanda akiongea na mwandishi wa mtandao huu wa Ulimwengu wa Habari amesema kituo hicho kitasaidia kurekebisha hali ya afya ya walengwa pamoja na kuwapa mafunzo mbalimbali kwa ukaribu zaidi ikilinganishwa na awali ambapo wamekuwa wakifuata huduma katika hospitali za nje ya mkoa na pengine nje ya nchi.
Mashanda amesema mradi huo unatarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi bilioni moja na nusu zinazotarajiwa kuchangwa na shirika hilo kwa ushirikiano na halmashauri ya wilaya ya Karagwe pamoja na shirika lijulikanalo kama LILIAN FOUNDATION kutoka nchini UHOLANZI.
Katika sherehe hizo uzinduzi wa mradi huo umetekelezwa na Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Kagera kupitia kwa askofu wake Aron Kijanjali, mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Karagwe Wales Mashanda pamoja na mwakilishi kutoka Uholanzi aliyechangia Euro laki mbili wakishuhudiwa na mwakilishi wa mkuu wa mkoa wa Kagera Bwana Fikira Kisimba aliyekuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo.
Pande zote zinazohusika na utekelezaji wa mradi huo zimeahidi kuhakikisha zinatimiza wajibu kwa mujibu wa makubaliano ili kufanikisha utekelezaji wa mradi huo kwa muda uliopangwa.
Askofu Kijanjali aliambatana na wachungaji mbalimbali toka wilayani Ngara ambapo amewapongeza KCBRP kwa kufanikisha azma hiyo ya kusaidia makundi maalum hasa ya watu wenye ulemavu.
Uzinduzi huo uliambatana na burudani toka kikundi cha utamaduni cha Rugu pamoja na kwaya ya Anglikana Kayanga, Karagwe.

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI