Thursday, September 4, 2014

DAYASPORA WASHANGAA UHAMIAJI KUWAPA URAIA WAGENI, NA KUWANYIMA WATANZANIA


Na Gaudensia Mngumi, Nipashe
BAADHI ya Watanzania walioko Marekani (Dayaspora) ‘wameliponda’ Bunge Maalumu la Katiba, kukumbatia mapendekezo ya Idara ya Uhamiaji na kutupilia mbali pendekezo la kuruhusu Watanzania kuwa na uraia pacha.

Wanadayaspora hao wakizungumza katika kipindi cha Habari za Ulimwengu kilichorushwa na Sauti ya Amerika (Voa) Jumatatu wiki hii jioni, walisema wameshangazwa na Uhamiaji, ambacho ni chombo cha serikali kukataa mapendekezo hayo kwa kisingizio cha kuvuruga usalama wa taifa na kuhatarisha uzalendo.

Waliwashangaa wajumbe hao kupokea mapendekezo ya maofisa hao kukataa uraia pacha wakati hutoa pasi za kusafiria za Tanzania kwa raia wa India na Somali, ambao wanamiliki pasi za kusafiria zaidi ya moja.

Katika mahojiano hayo, waliwashangaa watendaji hao kutekeleza sheria za mataifa mengine za kuruhusu uraia pacha kwa raia wao, huku wakiwanyima Watanzania haki ya kumiliki uraia wa nchi zaidi ya moja na kuhoji uzalendo wa wageni hao uko wapi kwa taifa lipi?

Walipinga madai kuwa uraia pacha utahatarisha usalama wa taifa na kuondoa uzalendo na kuhoji hivi ni kweli Watanzania walioko nyumbani ni wazalendo kuliko wale wa dayaspora?
“Sisi tupo ughaibuni kwa kupenda lakini pia tunaipenda nchi yetu na tunasaidia maendeleo kuliko hao wenye pesa walioko nchini,”alisema Jessica Mushara, mwana dayaspora aliyeshiriki mahojiano hayo.

‘Waliwaponda’ maofisa hao kwa kuwasilisha mapendekezo yaliyowatupa mbali wanadayaspora, ambao wamejikuta wanadharauliwa na nchi yao wenyewe licha ya kwamba, walitambuliwa awali na kutakiwa kuwasilisha maoni yao kwa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Kitendo cha maofisa hao kukataa mapendekezo yao, ambayo awali walishawishiwa na viongozi, akiwamo Rais Jakaya Kikwete kuwa wajitokeze kutetea suala la uraia pacha, kimewashangaza na kuhoji iwapo ni kweli hoja za kuwa na uraia pacha haina mashiko
Chanzo: Nipashe

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI