Tuesday, August 12, 2014

MAPACHA WALIOZALIWA WAKIWA WAMEUNGANA MKOANI GEITA WAFARIKI DUNIA

WATOTO wawili mapacha waliozaliwa wakiwa wameungana tumbo na kifua, wamefariki muda mchache baada ya kuzaliwa katika kituo cha afya Katoro wilaya ya Geita mkoani Geita. 
Akizungumza, mama wa watoto hao, Neema Luswetura (23), alisema alijifunga Agosti 6, muda mchache baada ya kufikishwa katika kituo hicho cha afya.
Muuguzi  wa zamu katika kituo hicho, Joyce Michael akizungumza na mwandishi wa habari hizi, alisema walimpokea mwanamke huyo saa 7 usiku akilalamika uchungu, na hivyo kupelekwa wodi ya wazazi na asubuhi alijifungua watoto wenye uzito wa kilo 5.1 wakiwa  wameshikana na kufariki.
Alisema wakati wa zoezi la kumzalisha, alilazimika kuomba  msaada toka kwa mganga wa zamu, Dk. Daniel Izengo ili kunusuru uhai wa mama huyo lakini watoto wake hawakuweza kupona. 
Dk. Izengo alithibitisha kuwepo kwa tukio hilo na juhudi za kunusuru uhai wa watoto hao zilishindikana, akieleza kitalaam tukio hilo linajulikana (coujoined twins).
Kutokana na hali hiyo, Dk. Izengo ameishauru jamii hususani wajawazito kuzingatia ushauri wanaopewa  na madaktari.

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI