Thursday, July 17, 2014

TIDO MHANDO AAGA MWANANCHI COMMUNICATIONS LTD

Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Limited (MCL), Tido Mhando akizungumza na wafanyakazi wa MCL, jijini Dar es Salaam.
Picha na Venance Nestory 
MKURUGENZI Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Tido Mhando amewaaga wafanyakazi wa kampuni hiyo baada ya kumaliza mkataba wake wa miaka miwili na nusu.
Mkataba wa Tido katika kampuni ya Mwananchi utafika kikomo mwishoni mwa mwezi huu.
Taarifa ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa Nation Media Group (NMG), Linus Gitahi kwa wafanyakazi wote wa Afrika Mashariki ambako kampuni hiyo inamiliki vyombo vya habari, inasema Mhando anaondoka MCL huku akiacha mafanikio makubwa katika nyanja zote na kwamba atakumbukwa kwa mchango wake.
MCL ni kampuni tanzu ya NMG inayochapicha magazeti ya Mwananchi, Mwananchi Jumamosi, Mwananchi Jumapili, The Citizen, The Citizen on Saturday, Sunday Citizen na Mwanaspoti.
Kabla ya kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa MCL mwaka 2012, Mhando alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kati ya mwaka 2006 na 2010. 
Awali alikuwa Mkuu wa Idara ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la BBC (1999-2006).
Mhando aliiwezesha MCL kukua kwa kasi kubwa katika mapato na katika mpango wa uchapishaji wa magazeti ya MCL Kanda ya Ziwa ambako wakazi wa mikoa hiyo sasa wamekuwa wakisoma magazeti asubuhi tofauti na zamani.
Wafanyakazi wa MCL walimpongeza kwa kuboresha masilahi yao kwa kipindi cha uongozi wake na kuandaa misingi bora ya uongozi, ikiwamo kumwandaa mrithi wake.
Akiwaaga wafanyakazi jana asubuhi, Mhando aliwashukuru kwa ushirikiano wao pia alisema amejifunza mambo mengi mapya, ikizingatiwa kuwa kwa miaka mingi alikuwa kwenye sekta ya habari ya utangazaji tofauti na uchapishaji. 
“Safari hii ilinipa uzoefu mpya na wenye changamoto nyingi lakini kupitia ushirikiano wenu wa dhati tulifanikiwa kuiweka kampuni katika hali nzuri,” alisema Mhando.
Gitahi alisema nafasi ya Mhando itachukuliwa na aliyekuwa Ofisa Mwendeshaji Mkuu wa MCL (COO), Francis Nanai.
Nanai alijiunga MCL , Agosti mwaka jana akitokea Kampuni ya Saruji ya Mbeya Cement (Lafarge Tanzania) ya mkoani Mbeya akiwa Mkurugenzi wa Biashara.

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI