Tuesday, July 22, 2014

KUHUSU BINTI ALIYETUMIKISHWA KWENYE MADANGURO CHINA, ALIEHOJIWA NA POLISI KWA MASAA 11

SHIRIKA la Polisi la Kimataifa (Interpol), Tawi la Tanzania, limemhoji kwa saa kumi na moja binti aliyerubuniwa na kupelekwa China ambako kwa miezi mitatu alikuwa akitumikishwa kwenye madanguro nchini humo. 
Siku chache zilizopita, Mwananchi liliandika mfululizo, makala kuhusu msichana Munira Mathias, (si jina lake halisi) aliyetumikishwa kwenye madanguro nchini China, baada ya kurubuniwa kwamba alikuwa akipelekwa kufanya kazi kwenye hoteli kubwa.

Munira alisema baada ya taarifa zake kuandikwa Interpol walimtaka afike ofisini kwao kwa mahojiano. Mara ya kwanza alihojiwa kwa saa saba na aliitwa tena mara ya pili na kuhojiwa kwa saa tatu na nusu.
“Walinihoji jinsi safari yangu ilivyokuwa na namna ambavyo wale wanawake waliotuchukua kutoka hapa (Tanzania) hadi China na walivyosuka mipango ya kunisafirisha,” alisema.
Alisema: “Walikuwa wanataka kuendelea kufahamu kwa kina jinsi nilivyosafirishwa na walionisafirisha, hata hivyo nimewapa ushirikiano wa kutosha.”
Mkuu wa Interpol Tawi la Tanzania, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Gustav Babile alikiri ofisi yake kumhoji Munira na kwamba lengo ni kufahamu kwa undani jinsi Watanzania wanavyotumikishwa kwenye madanguro hayo, pamoja na kujua jinsi biashara ya binadamu kati ya China na Tanzania inavyofanyika.
“Nia ilikuwa ni kujua namna wasichana wanavyotolewa hapa na kupelekwa huko, lakini kikubwa ni kufanya kazi yetu kukomesha biashara hiyo kimataifa,” alisema Babile.

Alisema siyo mara ya kwanza kwa Interpol kufanya jitihada za kukomesha biashara ya binadamu na kwamba hatua zimekuwa zikichukuliwa kila mara na siyo kwa Watanzania pekee, bali hata raia wa kigeni wanaokuja nchini.
“Tunafanya hii operesheni mara kwa mara. Kwa mfano, waliwahi kuletwa wanawake kutoka Nepal, walipofika hapa hati zao za kusafiria zikafichwa na wale wanaowatumikisha na wakaanza kufanya biashara ya ukahaba na baadaye kuwalipa wale waliowaleta,”alisema Babile.

Alisema kitengo hicho kimewahi kuwarudisha wanawake kutoka China waliofika hapa nchini kwa nia ya kufanya biashara ya ukahaba.
Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Lucy Ngonyani ambaye ndiye aliyemhoji Munira alisema wanaendelea kufanya uchunguzi wa kina kuhusu tukio la binti huyo kupelekwa China na matukio mengine yenye uhusiano au kufanana na hilo.
Atishiwa kifo
Wakati hayo yakiendelea, Munira amesema hatua yake ya kuweka wazi ukatili aliofanyiwa China umemfanya aishi kwa shaka baada ya kusikia kuwa wanawake wa Magomeni ambao anawataja kuhusika kumsafirisha wanamsaka ili kumdhuru.
“Nilipata taarifa kutoka kwa rafiki yangu mmoja (jina linahifadhiwa) ambaye tulikuwa naye China, aliniambia wale mabosi wetu wa China wamewapa taarifa wanawake wa Magomeni ili wakinipata popote waniue,” alisema Munira.

Alisema alianza kuona dalili hizo tangu alipotua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), akitoka China kwani walikuwapo baadhi ya wanawake ambao walishiriki katika mipango ya safari yake.
Alisema aligundua kuwa mawakala waliomsafirisha wanamtafuta walipomfuata rafiki yake aliyemsindikiza na kuuliza ni wapi anakoishi hivi sasa.
“Hali hiyo inanitia shaka sana na ndiyo maana naishi maisha ya kujificha hata vyombo vya usafiri wa umma situmii,” alisema.

Kutokana na tishio hilo, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba amesema kituo hicho kinaandaa taratibu za kumsaidia msichana huyo kisheria.
“Tumeshazungumza naye, kwa bahati mbaya leo (jana) aliitwa mahali lakini ilikuwa aje hapa na tufanye mipango ya kumsaidia kisheria,” alisema Dk Bisimba....
Alisema kituo hicho kinalaani biashara ya usafirishaji wa binadamu na kuwataka wasichana wote waliowahi kufanyiwa vitendo hivyo kuwa na ujasiri wa kusema ili sheria zichukuliwe dhidi ya wahusika.
“Tulipambana mpaka sheria ya kudhibiti usafirishaji wa binadamu ikatungwa, awali iliwekwa pamoja na ile Sheria ya Makosa ya Kujamiiana lakini hivi sasa ni sheria inayojitegemea,” alisema.

Taasisi nyingine iliyojitokeza kumsadia binti hiyo ni Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), ambacho kimeahidi kukutana naye ili kuona jinsi ya kumsaidia.
Munira alipelekwa China katika Jimbo la Guangzhou na kufanyishwa biashara ya ukahaba baada ya kurubuniwa kuwa anakwenda kufanya kazi katika hoteli kubwa.
Pamoja na manyanyaso mengine, aliwahi kubakwa na wanaume wanne wa Nigeria na kuambukizwa magonjwa ya zinaa pamoja na kushika ujauzito ambao hata hivyo, ulitoka baadaye.
Pamoja na adha hizo, alikuwa akiwajibika kuwalipa mabosi wake Dola 200 za Marekani (Sh330,000) kila siku, kutokana na fedha azizokuwa akipata kwa kufanya ukahaba 
Chanzo: Gazeti  la  Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI