Friday, July 18, 2014

AJALI: LORI LAPARAMIA KLABU YA POMBE NA KUUA WATANO PAPO HAPO!

VILIO na simanzi vimetalawa katika kitongoji cha Isimila old stone age cha  kijiji cha Ugwachanya wilaya ya Iringa Vijijini mkoani Iringa baada ya watu watatu kufa papo hapo na wengine watatu kujeruhiwa kwa kugongwa na lori kwenye kilabu cha pombe za kienyeji.
 Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo juzi jioni baada ya lori hilo kuacha barabara kuu ya Iringa-Mbeya na kugonga kilabu hicho.
 Mungi alisema kuwa ajali hiyo ilitokea majira ya saa 3:30 usiku wakati   lori hilo aina ya M benz likiwa na tela likiendeshwa na Juma Omari (40), Mkazi wa Makorongoni Manispaa ya iringa.
Aliwataja waliokufa katika ajali hiyo kuwa ni Leodard Mkendela (35), Neema Mkendela, Kamisia Mkendela,  Ester Mwoloma na Oscar Nzosamia (25), wakazi wa Ugwachanya.
Waliojeruhiwa katika ajali hiyo ni  Musa Kadege (25), Kasimu Mambo (44) na Juma Omari, wakazi wa Kijiweni na kwamba wamelazwa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Iringa kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
 
“Ajali hii ni ya kusikitisha ni mbaya sana na kusononesha tena imeua watatu wa familia moja na wawili ambao ni mke na mume, ”alisema Mungi.
 Alisema  eneo ilipotokea  ajali hiyo lipo baada ya kupanda mlima ambao dereva alitakiwa kuendesha kwa mwendo wa polepole.
Alisema baada ya ajali hiyo kutokea, dereva huyo alijaribu kukimbia lakini kutokana na kujeruhiwa vibaya,  alijisalimisha kwenye makazi ya watu.
Alisema bado wanaendelea kufanya uchunguzi ili kubaini chanzo cha ajali hiyo na kwamba dereva huyo atafikishwa mahakamani baada ya kukamilika.
 Kwa upande wake Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Iringa, Dk.  Alfred Mwakalebela amethibitisha kupokea kwa maiti ya watu hao na majeruhi hao.
Alisema mmoja wa majeruhi hao hali yake ni mbaya na amelazwa chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum (ICU).
Baadhi ya mashuhuda wa ajali hiyo wamesema kuwa marehemu hao walikuwa wamekaa kilabuni hapo wakinywa pombe.
“ Nilikuwa nyumbani ghafla nikasikia kelele katika  eneo hilo, nikasogea karibu na kuona gari limesimama likiwa limevunjika sehemu za mbele ya kilabu na watu hao wamefariki dunia, ”alidai mmoja wa mashuhuda hao.
-Freebongo

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI