Wednesday, May 21, 2014

KAGERA SUGAR: KUSAJILI KWA MFUMO WA MAJARIBIO HAKUNA MAANA, TUNATAKA KIFAA CHA KIGANDA

Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
WAKATI dirisha la usajili wa ligi kuu soka Tanzania bara likiwa njiani kufunguliwa, wakata miwa wa Kaitaba, `Wanankulukumbi` Kagera Sugar wamegoma kufanya usajili wao kwa mfumo wa majaribio .
Kocha msaidizi wa klabu hiyo, Murage Kabange amesema tayari wameshapata wachezaji 30 na tayari wameanza mazungumzo ya awali na baadhi ya wanandinga hao.
“Siku zote sisi hatufanyi usajili kwa kuwafanyia majaribio. Unajua ukumuita mtu afanye majaribio, daima anajipanga vizuri sana”.
“Kila mchezaji anajiandaa kwasababu anajua anafanya usaili. Unaweza kumchagua na kumwingiza katika timu, halafu tatizo likaanzia hapo”. Alisema Kabange.
“Usajili wetu unaanza mbali sana. Wakati ligi inaendelea tunaangalia wachezaji gani wanatufaa. Na mwishoni mwa msimu tunakuwa na majina mengi sana”.
“Kwasasa tuna majina 30, kuna wachezaji tumeshaanza mazungumzo nao, cha msingi tunasubiri dirisha la usajili lifunguliwe rasmi ili tukamilishe taratibu zote”.
Aidha, Kabange aliongeza kuwa dhamira yao ya kusaka mshambuliaji wa kati wa kimataifa iko palepale na tayari kocha mkuu, Jackson Mayanja ameshaanza mchakato.
“Bahati nzuri mwalimu wetu ni mwenyeji wa Uganda. Kama unavyojua Uganda kuna vipaji vingi, kwa hiyo hilo halina ugumu. Kuna uwezekano tukapata mshambuliaji Mganda”. Alisema Kabange.

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI