Thursday, April 10, 2014

SERIKALI YAENDELEA KUHIMIZA MATUMIZI YA MASHINE ZA EFDS NCHINI

Waziri Mkuu Pinda akisisiti jambo
Na Eleuteri Mangi -MAELEZO
UJIO wa mashine za kielekroniki za kutolea risiti za kodi (EFDs) nchini ni ukombozi wa ukusanyaji wa mapato ya nchi ambayo yalikuwa yakipotea na kulinyima taifa mapato kwa maendeleo yake, tofauti na mfumo wa zamani wa kukusanya mapato kwa risiti za vitabu vya mauzo.
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iliwahakikishia Wafanyabiashara na Watanzania kwa ujumla kuwa utaratibu wa kutumia Mashine za EFD ulianzishwa kwa lengo la kumrahisishia mfanyabiashara utunzaji wa kumbukumbu za biashara za kila siku pamoja na kuondoa usumbufu wakati wa ukadiriaji wa kodi. Kwa mantiki hiyo ni wajibu wa Serikali na taasisi inayosimamia mapato ambayo ni TRA kutoa elimu kwa wateja ambao ni wafanyabiashara wakubwa na wadogo juu ya mfumo mpya wa ukusanyaji kodi.
Dhamira ya TRA katika Mpango mkakati wake wa Nne wa kukusanya mapato nchini ni “Kurahisisha ulipaji wa kodi na kuyafanya maisha yawe bora”. Kwa dhamira hiyo, TRA imekuwa ikiendesha kampeni za kuwahamasisha walipa kodi na jamii kwa ujumla umuhimu wa kutoa na kudai risiti sahihi za mashine za kielekroniki za kutolea risiti za kodi (EFDs).
Kabla ya kuanza utekelezaji wa mfumo huu, elimu ilitolewa kwa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kupitia vyombo mbalimbali vya habari pamoja na semina ambazo zilitolewa kwa makundi mbalimbali ya wafanyabiashara.
Ni dhahiri kuwa elimu hiyo bado inaendelea kutolewa kwa njia mbalimbali ambapo kuhusu ununuzi wa mashine hizo kwa awamu ya pili, muda wa maandalizi ulisogezwa hadi Desemba 31, 2013 na taarifa ilitolewa na bado zinaendelea kutolewa kupitia vyombo vya habari.
Aidha, Serikali kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali wa Sekta Binafsi inaendelea kutoa elimu kuhusu matumizi endelevu na faida za Mashine za EFD kwa wafanyabiashara na wanunuzi wa bidhaa na huduma mbalimbali za kijamii.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mizengo Pinda alipokuwa akihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Desemba 21, 2013 wakati wa kuhitimisha mkutano wa 14 wa Bunge hilo, alisema kuwa Serikali ililiarifu Bunge kuhusu mikakati mbalimbali itakayotekelezwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa lengo la kuimarisha ukusanyaji wa Mapato ya Ndani.
Moja ya hatua hizo muhimu ni kuendelea kuimarisha matumizi ya Mashine za Kielektroniki za kutoa Risiti za EFDs. Mashine hizi zimeunganishwa kwa Mtandao wa Kompyuta moja kwa moja na Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa lengo la kuwezesha Serikali kupata mapato stahiki bila udanganyifu.
Aidha, Mashine hizi zinasimamiwa kupitia Mtandao wa Kielektroniki ambapo hupeleka taarifa moja kwa moja kwenye hifadhi kuu ya kumbukumbu TRA kila siku. Kwa kuzingatia kuwa Wabunge ni wadau muhimu, Waziri Mkuu Pinda alitoa wito kwao na Viongozi wa ngazi zote kushirikiana na Serikali kuwaelimisha Wananchi na Wafanyabiashara kuhusu manufaa ya Mfumo huo wa Mashine za Kielektroniki ili kwa pamoja washirikiane kujenga uchumi wa nchi na kuleta maendeleo endelevu kwa kulipa kodi stahiki.
Siku za hivi karibuni kumekuwa na upotoshwaji na uvumi kuwa matumizi ya mashine za EFDs yamesitihwa, Serikali tayari Aprili 9 mwaka huu ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari jijini Dare s salaam kuwa uvumi huo hauna ukweli wowote.
Kwa dhihirisha kuwa mashine za EFDs bado utaratibu wake unaendelea, Februari 26, mwaka huu Waziri Mkuu Pinda alikaa na TRA, Wizara ya Fedha, Wizara ya Viwanda na Biasha pamoja na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na kutoa maelekezo ya Serikali kwa ajili ya utekelezaji.
Maelekezo hayo yaliyotolewa ni pamoja na kutolewa orodha ya wafanyabiashara walioainishwa na kupewa barua iwe wazi kwa kubandikwa ofisi zote za TRA za mikoa na wilaya.
Aidha TRA itoe tamko kupitia vyombo vya habari na kutangaza namba za simu zitakazotumika kutoa taarifa kwa vitendo vya rushwa na unyanyasaji wakati zoezi linaendelea.
Jambo hilo la utekelezaji wa maagizo ya Waziri Mkuu Pinda limetekelezwa na TRA kama ilivyoelekezwa ambapo mpaka sasa tayari orodha ya wafanyabiashara zimekabidhiwa kwa wakuu wa mikoa na wilaya zote nchini.
Kuhusu taarifa za vitendo vya rushwa na unyanyasaji, utaratibu huo umekamilika ambapo namba za simu 0689 122515 itatumika kwa kupiga simu endapo mteja atakutana na moja ya vitendo vilivyoainishwa na 0689 122516 imetolewa mahususi kwa kutuma ujumbe mfupi.
Nia ya Serikali kwa kushirikiana na TRA ni kuendelea kuhamasisha na kuimarisha matumizi na udhibiti wa Mashine za Elektroniki za kutoa stakabadhi za kodi (EFDs) na kutoa elimu kwa walipakodi na wafanyabiashara kuhusu matumizi ya mashine hizi.
Walengwa katika mfumo huu wa kutumia mashine za kodi za kielektroniki ulianza kutekelezwa kwa awamu ambapo awamu ya kwanza ilianza mwaka 2010 ni wafanyabiashara waliosajiliwa kwenye kodi ya ongezeko la thamani, yaani VAT.
Awamu ya pili ilianza kutekelezwa mwaka 2013 kwa kuzingatia Sheria ya kusimamia Kanuni ya Kodi ya Mapato ya mwaka 2012 (Income Tax Electronic Fiscal Devices Regulations) ambayo inawahusu wafanyabiashara ambao hawajasajiliwa kwenye VAT ambao mauzo ghafi kwa mwaka ni shilingi milioni 14 na zaidi kwa mwaka.
Wafanyabiashara wasio rasmi aina ya Mama Ntilie na wale wanaotembeza bidhaa barabarani hawahusiki katika mpango wa kutumia mashine za EFD kwa sababu hawana sehemu maalum ya kufanyia biashara.
Serikali imewataka wafanyabiashara hawa waendelee na shughuli zao na wala hawatabughudhiwa. Walioko kwenye mpango huu ni wale wenye biashara wenye mauzo ya milioni 14 na zaidi.
Katika kunyambulisha, wafanyabiashara wanaotambuliwa katika mfumo huu wa ukusanyaji kodi, mfumo na sheria ziliainisha kuwa ni wenye biashara zifuatazo; wenye maduka ya vipuri, mawakili na maduka ya jumla (Sub wholesale shops).
Wengine ni wafanyabiashara wakubwa wa Mbao, migahawa mikubwa, maduka ya simu na vipuri vyake, baa na vinywaji baridi, studio za picha, watoa huduma ya chakula (Catering Services), wauzaji wa pikipiki, wauza magari, maduka makubwa ya nguo na biashara zinginezo.
Kwa Nchi nzima mfumo umewalenga wafanyabiashara 200,000 tu kwa awamu ya pili kati ya wafanyabiashara zaidi ya 1,500,000 ambao wamesajiliwa kulipa kodi.
Uzuri wa mashine hizi zimemlenga mtumiaji moja kwa moja, wanunuzi na serikali ikizingatiwa mfanyabiashara ana faida anapotumia kwa kazi zake za kibiashara.
Kitu chochote kinapoanzishwa huwa na faida na changamoto zake, miongoni mwa faida za Mashine za Kodi za Kielekitroniki ni kutoa risiti na ankara za kodi.
Kwa kuwa sheria inamtaka kila mfanyabiashara anayeuza au kutoa huduma ya Tsh. 5,000 na zaidi atoe risiti, mfanyabiashara huyu mwanzoni alilazimika kuchapisha vitabu vya risiti mara zote, kwa kutumia mashine hizi anaondokana na uchapishaji wa vitabu ambavyo ni vingi na utunzaji wa nakala zake unaleta usumbufu.
Mashine hizi zina uwezo mkubwa wa kutunza kumbukumbu za mauzo, manunuzi na mali ya biashara (Stock) bila kufutika kwa muda usiopungua miaka mitano na hivyo kuondokana na usumbufu wa kuchapisha vitabu vya risiti kwa kipindi hicho.
Zaidi ya hapo mashine hizi zintumia lugha ya Kingereza na Kiswahili ambazo zinamrahisishia mtumiaji kuchagua lugha anayoitaka.
Vile vile mtumiaji ana uwezo wa kutoa taarifa za mauzo kwa siku, wiki, mwezi na mwaka, kwa kipindi kisichopungua miaka mitano muda ambao mtumiaji hatahangaika ni namna gani atatunza kumbukumbu za biashara yake kwa uhakika bila kuhofia kuharibika kwa njia mbalimbali ikiwemo kuungua moto au kulowana kwa maji.
Mfanyabiashara pia ana faida inayomuwezesha kupokea maelekezo moja kwa moja kutoka kwenye mfumo wa Mamlaka ya Mapato (TRA Server) kuruhusu kuziongezea uwezo wa hizi mashine wakati wowote bila kuathiri ufanyaji kazi wake.
Faida nyingine kwa mtumiaji ni kutuma na kupokea ujumbe (SMS) kutoka kwenye mfumo wa Mamlaka ya Mapato. Hii huwezesha TRA kumtaarifu mtumiaji taarifa yoyote ya kodi inayomuhusu bila kuonana ana kwa ana njia ambayo imeondoa usumbufu kwa wateja kwa kupanga foleni ofisi za TRA kusubiri huduma.
Kwa kuwa tupo kwenye ulimwengu wa sayansi na teknolojia mashine hiyo hiyo inaweza kutumika kutuma na kupokea fedha “mobile money” na kwa hiyo kumruhusu mtumiaji kuitumia kuongeza kipato zaidi au kulipa kodi na huduma zingine kama vile umeme, maji na huduma nyinginezo bila kupoteza muda kwenda kwenye ofisi husika.
Kwa kuzingatia umuhimu wa kutunza kumbukumbu kwa wafanyabiashara nchini, TRA pamoja na watengenezaji na wasambazaji wa mashine za kielektroniki walijadiliana na kuafikiana kwamba bei za mashine ziuzwe kuanzia Sh. 600,000/= na ukomo uwe Sh. 778, 377 kwa kulinganisha na mauzo dola za Kimarekani ambazo bei ya chini ya mashine za EFD nchini ni dola za Kimarekani 375 na bei ya juu ni Dola za Kimarekani 487.
Bei za mashine hizi hapa nchini zipo chini ukilinganisha na bei ya mashine katika nchi zinazotumia mfumo unaofanana na wa Tanzania.
Nchi hizo ni pamoja na Italia, zinauzwa kwa bei ya chini kwa Dola za Kimarekani 870 na bei ya juu ni Dola 1,000, Rwanda, bei ya chini kwa dola za Kimarekani 800 bei ya juu ni dola za Kimarekani 830, Ethiopia, bei ya chini kwa Dola za Kimarekani 446 na bei ya juu ni Dola za Kimarekani 1,026.
Nchi nyingine ni Serbia, bei ya chini ni Dola za Kimarekani 360 na bei ya juu ni dola za kimarekani 1,750 na Bulgaria bei ya chini ni Dola za Kimarekani 230 na bei ya juu ni Dola za Kimarekani 400.
Ili kumrahisishia mfanyabiashara nchini anunue mashine hizi, TRA imeongea na wasambazaji ambao wamekubali kuuza mashine hizi kwa kupokea malipo kwa awamu iwapo wafanyabiashara watajiunga katika vikundi vitakavyopewa dhamana ya kuhakikisha wauzaji wanapata malipo yao.
Kuhusu gharama za matengenezo kuwa kubwa, watengenezaji wametoa “warranty” ya miaka mitatu kwa mashine inayoharibika pasipo makusudi.
Hivyo pale mashine inapoharibika mfanyabiashara anatakiwa kuwasiliana na mtengenezaji kwa ajili ya matengenezo. Wasambazaji wanawajibika kufunga mashine, na kutoa elimu bora ya matumizi ya mashine hizo. 
Ni vyema wafanyabiashara wakaelewa kuwa sheria inamtaka kila msambazaji pamoja na kuuza mashine anawajibika kuzifanyia matengenezo mashine hizo. Hii itasaidia kudhibiti taarifa ambazo zimo ndani ya mashine.
Ikumbukwe kuwa gharama zote za ununuzi wa mashine hizi zinarudishwa kwa wafanyabiashara pale watakapowasilisha mahesabu yao ya kodi. Hivyo kuifanya Serikali kulipia gharama za mashine kwa kupitia kodi ambayo itasamehewa pindi mfanyabiashara atakapowasilisha mahesabu.
Kwa wajenga nchi wote ni vema tuitikie wito wa kujenga tabia ya kiungwana ya kila mwananchi kudai risiti kila anaponunua bidhaa au kupata huduma.
Kwa kufanya hivyo, kama asipopewa risiti kodi hiyo inaingia mfukoni mwa mfanyabiashara maana haitowasilishwa TRA na hivyo kuikosesha serikali mapato ambayo yangesaidia miradi ya maendeleo ya taifa na kuboresha huduma za jamii kwa wananchi.
Kwa kuwa mawasiliano ni njia pekee ya kupata taarifa, TRA kwa kutambua hilo imeanzisha mawasiliano ya simu yasiyo na malipo katika kituo cha huduma kwa wateja wake.
Simu hizo ni 0786 800 000 kwa watumiaji wa Airtel, 0713 800 333 kwa watumiaji wa Tigo, 0800110016 kwa watumiaji wa Vodacom na TTC ikiongozwa na kauli mbiu “Pamoja tunajenga taifa letu”.
Ili kuhakikisha kumbukumbu zipo sahihi karatasi zinatumika zinazojulikana kama “Thermal Paper” ni za kisasa na hazifutiki kwa urahisi na zina Alama za Siri ndani yake kwa ajili ya kuongeza usalama.
Kwa kuzingatia ubora wa karatasi, zina uwezo wa kutoa wastani wa risiti kati ya risiti 200 hadi 1,000 kulingana na urefu wa “Paper Roll”! au bunda ambazo zinafaa kwa matumizi ya kila siku.
Kwa kuzingatia umuhimu wa ukusanyaji wa mapato nchini, Manaibu Waziri wa Fedha Adam Malima na Mwigulu Nchemba kupitia ziara walizofanya walisema kuwa Serikali itaendelea kuwasisitiza wafanyabiashara kununua na kuzitumia mshine za EFD kwa maendeleo yao endelevu na ya taifa.
Manaibu Waziri hao kwa nyakati tofauti walipoongea na wafanyabiashara wa mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza, Njombe, Ruvuma na Mbeya walisema kuwa mashine ya EFD zinawarahisishia wafanyabiashara kulipa kodi na kufanya biashara yenye tija na bora nchini.
Kwa upande wao wafanyabiashara hao wamesema hawapingi kutumia mashine hizo za EFD lakini wakanung’unikia changamoto ya bei za mashine hizo na wakidai zinawaumiza kwa kuwa ni kubwa zisizolingana na mitaji yao.
Changamoto ambayo Kamishna wa Kodi za Ndani wa TRA Patrick Kasera alibainisha kuwa hiyo ni hofu waliyopandikizwa wafanyabiashara ambayo sio sahihi.
Mchakato wa ununuzi wa mashine za EFD ulifanyika kwa uwazi kupitia tenda ya kimataifa na kila mtu alikuwa na uhuru kushiriki. Kati ya walioomba walipatikana wasambazaji 11 na sio mmoja au wachache kama inavyopotoshwa.
Mchakato wa kuwapata wazabuni ulifuata Sheria ya Manunuzi ya Umma ya Mwaka 2004 inayotumika, na uligawanyika katika sehemu mbili kama ifuatavyo;
Sehemu ya kwanza ilikuwa kuwapata watengenezaji wa Mashine; Tenda ya wazi ya Kimataifa (International bidding) ilitangazwa kupitia magazeti ya Daily News ya Agosti 10, 2012 na The East African ya Agosti 11-17, 2012. Watengenezaji waliokidhi vigezo vilivyoainishwa ndio waliopata tenda.
Sehemu ya pili ilikuwa kuwapata wasambazaji; Tenda ya wazi vile vile ilitangazwa kwenye gazeti la Daily News la Agosti 10, 2012 kwa wasambazaji wenye vigezo vinavyojumuisha; wajibu wa kufungua ofisi kila mkoa, mtaji usiopungua Shilingi za Kitanzania milioni 500, uzoefu wa kusambaza na kufanyia matengenezo mashine za kielektroniki kwa zaidi ya miaka miwili. Wasambazaji waliokidhi vigezo vilivyoainishwa ndio waliopata tenda. Ukweli ni kwamba bei za mashine hizo nchini ni ndogo ikilinganishwa na nchi nyingine duniani.
Ili kuendelea kuwaelimisha wafanyabiashara nchi nzima, Serikali kupitia Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na TRA inatarajia kuendelea na ziara ya kutembelea vituo vikuu vya ukusanyaji mapato vilivyopo mipakani ikiwemo kanda ya kaskazini katika mikoa ya Arusha, Tanga na Kimanjaro kupitia mipaka ya Namanga, Horohoro na Holili.
Zoezi hili la kutembelea maeneo mbalimbali nchini ni endelevu ambapo lengo lake ni kuhakikisha elimu inayotolewa inawafikia watanzania wote katika maeneo yao mahalia na watambue wajibu wao kwa nchi katika kukusanya mapato.
Ni matumaini mema kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazotumia mashine za EFD katika kukusanya mapato yake ya ndani kwa maendeleo endelevu ya uchumi wake.
Miongoni mwa nchi ambazo zinatumia mahine za EFD duniani ni pamoja na Malawi, Rwanda, Ethiopia, Serbia, Italia na Bulgaria.
Watanzania wote tuunge mkono juhudi za Serikali katika kukusanya mapato kwa kuzingatia kauli mbiu ambayo ndio dira, “Unapouza toa risiti, unaponunua dai risiti” na “Pamoja tunajenga taifa letu” iwe ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku yanayozingatia kujali maendeleo endelevu na ustawi wa watu wote nchini.

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI