Friday, April 18, 2014

PAZIA LA LIGI KUU BARA LAFUNGWA, AZAM FC KUKABIDHIWA KOMBE LAO CHAMAZI KESHO

MICHUANO ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inafikia tamati kesho (Aprili 19 mwaka huu) kwa timu zote 14 kuwa viwanjani, huku mabingwa wapya Azam wakikabidhiwa kombe lao Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam katika mechi yao dhidi ya JKT Ruvu.

Mechi zote saba zitachezwa kuanzia saa 10 kamili jioni ambapo Yanga na Simba zitakuwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa mechi ambayo viingilio vyake ni sh. 7,000 kwa viti vya bluu na kijani, sh. 10,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 20,000 kwa VIP C na B wakati VIP A itakuwa sh. 30,000.

Tayari tiketi zimeanza kuuzwa leo (Aprili 18 mwaka huu) katika vituo saba vya; Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Kariakoo (Kidongo Chekundu), Buguruni Shell, mgahawa wa Steers uliopo Mtaa wa Ohio na Samora, Ubungo OilCom, Dar Live Mbagala na Uwanja wa Taifa.

Mechi nyingine zitakuwa kati ya Tanzania Prisons na Ashanti United (Uwanja wa Jamhuri, Morogoro), Rhino Rangers na Ruvu Shooting (Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora), Mbeya City na Mgambo Shooting (Uwanja wa Sokoine, Mbeya), Oljoro JKT na Mtibwa Sugar (Uwanja wa Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha) na Coastal Union na Kagera Sugar (Uwanja wa Mkwakwani, Tanga).

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI