ILIYOKUWA Tume ya Mabadiliko ya Katiba, chini ya Jaji Joseph Warioba, imetoa ufafanuzi katika baadhi ya maeneo ya Rasimu ya Katiba yaliyokosolewa na Rais Jakaya Kikwete katika hotuba yake ya uzinduzi wa Bunge Maalumu la Katiba wiki iliyopita.
Taarifa ya Tume hiyo kwa umma wa Watanzania, iliyosambazwa jana kwenye vyombo vya habari, ilisema hatua hiyo ya kutoa ufafanuzi katika baadhi ya maeneo imetokana na kile kinachoelezwa na Tume hiyo kuwa shauku kubwa ya wananchi kutaka ufafanuzi wa mambo mbalimbali kuhusu Rasimu ya Katiba baada ya hotuba ya Rais Kikwete. (J.G)
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ufafanuzi huo umetokana na kikao cha tathmini kilichofanywa na wajumbe wa iliyokuwa Tume hiyo ya Warioba, kilichofanyika Jumatatu wiki hii ya Machi 24, mwaka huu jijini Dar es Salaam, baada Tume kuhitimisha kazi yake hiyo.
Maeneo ambayo Tume hiyo imeyafanyia ufafanuzi ni pamoja na Usanifu wa Katiba; Malengo muhimu na mwelekeo wa shughuli za Serikali na sera za kitaifa (Dira); Nchi mbili, Serikali mbili; Mamlaka ya Rais; Orodha ya mambo ya Muungano; Katiba na Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mamlaka ya Mahakama ya Rufani na takwimu kuhusu maoni ya wananchi juu ya muundo wa Muungano.Ufafanuzi kamili ni kama ifuatavyo:-
UTANGULIZI
Tume ya Mabadiliko ya Katiba katika kutekeleza majukumu iliyopewa imetoa taarifa ya Tume yenye viambatisho vingi na vyenye maelezo ya kina kuhusu mchakato wa kuratibu, kukusanya, kuchambua maoni ya wananchi na kuandaa ripoti.
Baada ya kukamilisha kazi hiyo, Tume iliwasilisha Rasimu ya Katiba katika Bunge Maalumu la Katiba Machi 18, mwaka huu. Pamoja na Rasimu hiyo, Tume iliwasilisha Randama ya Rasimu ya Katiba na Bango kitita la Randama ya Rasimu ya Katiba ambayo ilitoa maelezo ya kila Ibara ya Rasimu ikitoa maudhui, madhumuni na lengo pamoja na sababu za mapendekezo ya kila Ibara.
Tangu kuwasilishwa kwa Rasimu na vyaraka zilizoambatana nayo katika Bunge Maalumu la Katiba, kumejitokeza tafsiri tofauti kuhusu baadhi ya mapendekezo yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba na baadhi ya taarifa zilizoambatana na Ripoti ya Tume. Katika maeneo ambayo kumekuwepo na tafsiri tofauti tofauti, ufafanuzi wa kina umetolewa kwenye Randama na bango kitita ya Randama ya Rasimu ya Katiba.
Kutokana na hali hiyo, Tume ya Mabadiliko ya Katiba, katika kikao chake cha tathmini ya kuhitimisha kazi kilichofanyika Machi 24, mwaka huu, jijini Dar es Salaam, imeamua kutoa maelezo ya ziada ya ufafanuzi kama ifutavyo:-
NCHI MBILI SERIKALI MBILI
Tangu Mwaka 1984 hatua ambazo zimechukuliwa na serikali zote mbili za Muungano na Zanzibar zimeifanya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka kuwa Nchi Moja yenye Serikali mbili na kuwa Nchi mbili zenye Serikali mbili. Kwa maana nyingine Masharti yaliyomo katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano yanaelekeza kwamba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Nchi moja yenye Serikali mbili- Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kufuatia Mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984, Zanzibar imetamka ni Nchi tofauti na ilivyokuwa imetamka kwamba ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano kabla ya Mabadiliko hayo.
Wakati Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa ni Nchi moja, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilikuwa na Mamlaka ya Kutunga Sheria juu ya Mambo ya Muungano kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yote, sasa uwezo huo umewekewa mipaka na Katiba ya Zanzibar Katika Ibara ya 132 ambayo inaelekeza kwamba Sheria iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kabla ya kuanza kutumika Zanzibar ipelekwe kwenye Baraza la Wawakilishi na kupata ridhaa ya kutumika Zanzibar .Zipo Sheria zilizotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zilipokosa ridhaa ya Baraza la Wawakilishi zilirejeshwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kufanyiwa marekebisho ili kukidhi maelekezo ya Baraza la Wawakilishi, kwa mfano, Sheria ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (Commission for Human Rights and Good Governance Act) na Sheria ya Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu (Deep Sea Fishing Authority Act)
MAMLAKA YA RAIS
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 imempa Rais wa Jamhuri ya Muungano mamlaka ya kuigawa Jamhuri ya Muungano katika maeneo ya kiutawala katika Mikoa na Wilaya. Hata hivyo, Marekebisho ya 10 ya Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984 yanampa Rais wa Zanzibar Mamlaka kama hayo ya kuigawa Zanzibar bila kufanya marekebisho stahiki ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Mwaka 1977. Kwa mantiki hiyo mamlaka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano yamepungua na kubaki kwa Tanzania Bara tu.
MAMLAKA YA MAHAKAMA YA RUFANI
Katiba ya Muungano ya 1977 imetoa mamlaka ya kusikiliza rufaa nchi nzima. Lakini Zanzibar imezuia Mahakama hiyo kusikiliza rufaa kutoka Mahakama za Kadhi, kutafsiri Katiba ya Zanzibar na rufaa kuhusu mashauri ya haki za binadamu.
Kwa kifupi:
Waasisi walituachia mambo 21 (ukiacha usajili wa vyama) kwenye orodha ya Muungano. Katika kipindi cha miaka ishirini iliyopita yamepunguzwa. Mambo yote yaliwekwa kwa utaratibu uliowekwa na Katiba lakini yameondolewa kinyume na Katiba. Sehemu zote mbili ziliamua kuachia baadhi ya mambo yake kuwa chini ya Serikali ya Muungano, sasa sehemu moja inaondoa mambo yake. Kwa hiyo serikali ya Muungano itakuwa inashughulikia zaidi mambo ya upande mmoja.
Waasisi walituachia Bunge lenye madaraka nchi nzima. Sasa ni lazima lipate idhini ya Baraza la Wawakilishi.
Waasisi waliacha Rais akiwa na madaraka kamili. Madaraka hayo yamepunguzwa bila kufuata utaratibu wa Katiba.
Waasisi walituachia Mahakama ya rufani yenye madaraka kamili. Madaraka haya yamepunguzwa.
Waasisi waliunganisha nchi mbili ikawa moja. Sasa tunazo nchi mbili.
Hii ndiyo inafanya wananchi wa Tanzania Bara waamini Zanzibar ni huru katika mambo yao. Wanaona ina mamlaka kamili kushughulikia mambo yake na imechukua rasilimali zake. Serikali ya Muungano imebaki na mamlaka na rasilimali za Tanzania Bara. Wabunge wa Zanzibar wanashiriki kuamua mambo ya Tanzania Bara lakini wabunge wa Tanzania Bara hawana nafasi ya kushiriki katika kuamua mambo ya Zanzibar.
Tume iliona ni vigumu kwa Zanzibar kurudi kwa hiyari kwenye hali ya awali, yaani kurudisha mambo yote yaliyotolewa kwenye orodha ya Muungano, kurudisha madaraka ya Rais na kufuta kipingere cha nchi mbili kwenye Katiba yake. Tume iliona kwamba pamoja na mambo haya kufanywa kinyume na Katiba ya Muungano hali ibaki hivyo hivyo. Lakini kwa kufanya hivyo basi malalamiko ya Tanzania Bara nayo yasipuuzwe. Hivyo Tume nayo ikapendekeza Serikali ya Tanganyika iundwe.
HITIMISHO
Tume inapenda kuwashukuru wananchi wote kwa shauku kubwa ya kutaka ufafanuzi wa mambo mbalimbali kuhusu Rasimu ya Katiba.
0 comments:
Post a Comment