Sunday, March 9, 2014

INASIKITISHA; MAPACHA WAWILI KATI YA WANNE WALIOZALIWA MBEYA WAFARIKI DUNIA

Mama akiwa na watoto wake wanne, kabla wawili
NDUGU, JAMAA NA MARAFIKI  WAKIWA KABURINI MUDA MFUPI KABLA YA MAZISHI 
KATIKA hali ya kusikitisha Watoto wawili kati ya Wanne 
ambao ni mapacha waliozaliwa kwa pamoja na mwanamke Aida 
Nakawala Mkazi wa Kijiji cha Chiwanda Wilaya ya Momba
Mkoani Mbeya wamefariki dunia kwa ugonjwa wa Nimonia.

Watoto hao wamefariki kwa mida tofauti ambapo Mtoto wa 
Kwanza alifariki Nyumbani kwao baada ya kuugua ghafla ndipo 
hali za wengine zilipoanza kutia shaka na kulazimu Waandishi 
wa Habari wa Mtandao wa Mbeya Yetu, Gazeti la Jambo Leo na 
Redio ya Bomba Fm waliohudhuria mazishi ya Mtoto huyo kulazimika 
kuwakimbiza katika Hospitali ya Wazazi Meta kwa matibabu zaidi.

Hata hivyo baada ya kupokelewa kwa watoto hao Watatu mtoto mmoja
aliaga dunia baada ya kuchelewa kupata matibabu kutokana na kubanwa 
na kifua na kusababisha kushindwa kupumua vizuri.

Hali za watoto wawili waliobaki wanaendelea vizuri na matibabu na 
kwa mujibu wa Daktari anayewatibu amesema taratibu za Hospitali 
hiyo ni kupokea watoto waliochini ya Miezi miwili lakini hao wamezidi 
umri huo hivyo badala ya kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mbeya 
wataendelea kuwepo Meta hadi hapo hali zao zitakapoimarika.

Baadhi ya wananchi na wauguzi katika Hospitali ya Wazazi Meta 
wamesema sababu ya watoto hao kuugua ni kutokana na  kukosekana 
kwa uangalifu wa karibu katika malezi ya watoto hao ukilinganisha 
na maisha ya vijijini kukosa watu wenye uelewa wa afya za watoto.

Wengine wameitupia lawama moja kwa moja Serikali kwa 
kushindwa kuchukua hatua za haraka tangu watoto walipozaliwa ili 
kujiridhisha na mazingira wanayopaswa watoto hao kuishi kwa 
kuwapatia msaada wa karibu na ushauri wa kitaalamu.

Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Mbeya, 
Thobias Mwalwego, alikiri kuwepo kwa urasimu katika Idara yao kwa 
madai kuwa tangu watoto hao walipokuwa wamezaliwa walipata taarifa 
na kuchukua hatua kwa afisa mmoja kufika kijijini na kuchukua picha zao.

Alisema urasimu unakuja kutokana na Ofisi ya Wilaya na Mkoa 
kukosa fungu la dharula ambapo barua za maombi zote hupelekwa 
makao makuu kwa Kamishna wa Ustawi wa Jamii ambapo 
Ofisi yake huchukua muda mrefu kurudisha majibu kutokana na 
waombaji kuwa wengi.

Alisema kila ofisi katika Ngazi ya Mkoa ingekuwa na fungu la 
Dharula kama ilivyo katika Ofisi zingine hali ambayo ingeweza 
kusaidia kuepusha vifo vya watoto hao kutokana na kupatiwa msaada 
wa ushauri na makazi rafiki kwa malezi ya mapacha wanaozidi wawili.

Aidha alishauri kila Halmashauri Nchini kutenga bajeti za kusaidia 
majanga kama hayo na vitu vya dharula wakati Serikali 
inajipanga kutekeleza kutokana na taratibu zake kuchukua muda 
mrefu ili kuweza kukabiliana na hali yoyote na muda muafaka.

Kwa Hisani ya Mbeya yetu blog.

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI