KOCHA Mkuu wa Azam FC, Joseph Marius Omog anaridhishwa na maendeleo ya mshambuliaji John Raphael Bocco ambaye aliuanzia wadini msimu huu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania kwa matibabu ya goti.
Mcameroon huyo amesema anaridhishwa na namna mfungaji huyo bora wa zamani wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara anavyoimarika taratibu na anaamini msimu ujao atakuwa vizuri zaidi.
“Wakati nafika hapa Bocco alikuwa majeruhi, lakini sasa amepona na uwakilishi wake umekuwa mzuri katika timu, ni jambo zuri kuwa na mchezaji kama yeye wakati kama huu unataka kushinda mechi,”alisema Omog.
Bocco alifunga bao la kwanza katika ushindi wa mabao 2-0 kwenye mchezo mgumu dhidi ya Mgambo JKT Uwanja wa Mkwakwani, Tanga Jumatano, wakati bao la pili alifunga Mganda, Brian Umony.
Ushindi huo uliifanya Azam FC iendelee kuwa kileleni mwa Ligi Kuu kwa pointi zake 50 ilizovuna katika mechi 22, ikifuatiwa na mabingwa watetezi, Yanga SC wenye pointi 46, lakini wana mchezo mmoja mkononi.
Yanga SC imebakiza mechi tano kuelekea tamati ya Ligi Kuu na Azam FC ina mechi nne, wakati mchuano wa kuwania ubingwa unaonekana kuwa mkali baina ya timu hizo mbili na mechi za Jumapili zinatarajiwa kutoa picha zaidi ya mbio zao.
Azam FC ikiwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kumenyana na Simba SC, wapinzani wao katika mbio za ubingwa, Yanga SC watahamia Mkwakwani, Tanga kuwakabili Mgambo JKT.
Chanzo: Tovuti ya Azam FC
0 comments:
Post a Comment