Monday, March 17, 2014

ASIYEKUBALI KUSHINDA SI MSHINDANI KALENGA, IRINGA

Akina mama mkoani Iringa katika Jimbo la Kalenga wakishangilia baada ya Godfrey Mgimwa kuibuka mshindi wa ubunge jimboni hapo.
Godfrey Mgimwa akinyanyuliwa na mmoja wa viongozi wa CCM mkoani Iringa katika Jimbo la Kalenga baada ya kuibuka mshindi katika uchaguzi ulifanyika Machi 16 mwaka huu akirithi kiti cha ubunge kilichoaachwa wazi na baba yake baada ya kufariki dunia.
LICHA ya uchaguzi wa jimbo la Kalenga kumalizika na Godfrey Mgimwa (CCM) kuibuka kidedea bado umeacha kovu lisilotibika haraka miongoni mwa walioumizwa kipindi cha kampeni za uchaguzi huo.

Katika kampeni hizo CHADEMA na CCM vilikuwa vikituhumiana kwa kuwatumia vijana katika matukio ya kiuhalifu kama vile kuwakamata viongozi wa vyama hivyo na kuwapiga na hata kuwateka viongozi hao.

CCM waliwatuhumu wafuasi wa CHADEMA kupiga na kumuumiza kiongozi wa CCM na dereva wa Naibu Waziri wa Uchumi Mwigulu Nchemba wakati CHADEMA wakiwatuhumu wafuasi wa CCM kwa kumpiga mchungaji wa kanisa la Orthodox, na kumpiga mbunge wa viti maalum wa CHADEMA Rose kwa madai alikuwa anatoa rushwa kwa wapiga kura.

Kasoro zote zilizojitokeza kipindi cha kampeni hadi uchaguzi serikali na vyama vya siasa havina budi kutafuta suluhu ya kutatua kasoro hizo ikiwemo kuwafundisha vijana wao namna ya kufanya kampeni za Amani kwa kutoa sera za kuwashawishi wananchi wamkubali mgombea badala ya kushindana kwa virungu na mapanga.
Matukio haya yote kama yatafumbiwa macho hakika yataliingiza  taifa katika machafuko ya kisiasa yasiyo na tija yoyote kwa taifa hili.

Kukomaa kwa Demokrasia si kushindana kwa kupigana bali ni kushindana kwa sera na pindi mtu anaposhindwa katika uchaguzi baada ya wananchi kuamua kumpa kura mtu mwingine, aliyeshindwa basi anakubaliana na matokeo na kumpongeza aliyepita.

Sasa baada ya wanakalenga kumchugua Godfrey Mgimwa kuwa mbunge wao, mbunge huyo hana budi kuondoa tofauti zao zote na wanachama wa vyama vya upinzania na kuwatumikia wananchi wake kwa kuhakikisha ahadi zilizo ahidi katika kipindi hiki kifupi cha uchaguzi anazitekeleza kwa muda mwafaka ilikujiwekea mazingira ya kukubalika na wananchi waKalenga.

Wanakalenga hawakuhitaji na wala hawakumchagua kwa ngonjera za ahadi bali wamempa fursa hiyo ya kuwatumikia wananchi hao baada ya kumwona ametambua matatizo wanayokabiliwa nayo ambayo mbunge huyo atayatatua katika kipindi hiki kifupi cha mwaka mmoja.

Hata hivyo si dhambi kwa mbunge mteule Mgimwa akatimiza baadhi ya malengo ambayo yaliaachwa na marehemu Williamu Mgimwa badala ya kuongeza ahadi nyingi zisizotekelezeka kwa wanakalenmga kwa lengo tu aonekana ana ahadi na malengo mazuri kwa wananchi wa Kalenga.

Aidha, katika kampeni wanafunzi ama watoto walichukuliwa kama mfano wa kuonesha namna gani serikali ya chama tawala inavyoshindwa kuwasaidia wananchi hata wanafunzi katika kuhakikisha wanapata mahitaji muhimu ya jamii.

Ni wazi sasa aliyepita atahakikisha pia wanafunzi waliooneshwa kama mfano wa wanafunzi wanaotoka katika familia masikini wanasaidie na wanapata elimu sawa na watoto wa vigogo badala ya kuwaacha watoto katika mazingira yale yale ambayo hayaoneshi utofauti wo wote wa chama hicho kugundua kuwa watoto hao wanatoka katika familia masikini.

Hata hivyo kuna haja ya kuangalia upya sheria ya vyama vya siasa ili ifanyiwe mabadiliko kutokana na sheria hiyo kutokuwa na kikomo cha idadi ya vyama vya siasa vinavyotakiwa kusajiliwa nchini.

Kutokana na sheria hiyo kukosa meno ya imesababisha utitiri wa vyama vingi vya siasa ambavyo vinaonekana kuanzishwa kwa malengo ya kupata ruzuku ambayo inaingia mifukoni mwa watu wachache.

Ruzuku zinazotolewa kwa vyama vya siasa ni fedha za wananchi ambazo zingeweza kuwasaidia wananchi katika mambo mengine ya msingi kwa jamii.

Uwingi wa vyama vingi nchini Tanzania haumanishi kukomaa kwa Demokrasia kwa kuwa nchi zilizoendelea kama marekani ina vyama viwili tu na bado ni nchi iliyokomaa kidemokrasia.
Wapiga kura katika Jimbo la Kalenga Mkoani Iringa wakiwa tayari kwa kupiga kura kumchagua mgombea wapendaye baada ya kampeni za kujinadi wagombea hao kuwashawishi wananchi hao na kuamua kwa hiari yao nani wampe kura zao. 
Picha kwa hisani ya Michuzi blog

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI