Saturday, November 21, 2015

NDUGAI AWAPASHA WABUNGE JUU YA NIDHAMU BUNGENI

WAKATI Rais John Magufuli akieleza kusikitishwa na vitendo vya kitoto vilivyofanywa bungeni na Kambi ya Upinzani jana, Spika wa Bunge, Job Ndugai amewataka wabunge wasimfanye awe Spika mbabe.
 Akizungumza baada ya Dk Magufuli kumaliza kutoa hotuba yake, Ndugai alisema amesikitishwa na tukio lililofanywa na wabunge wa upinzani na kuahidi kwamba halitajirudia siku za usoni.
   “Naomba niwapelekee ujumbe rafiki zangu waliotoka kwamba nyie ndiyo mnaweza kunifanya niwe Spika mpole, lakini pia mnaweza kunijenga nikawa Spika mbabe. Vitendo hivi naomba visijirudie, leo iwe mwisho,” alisema Spika Ndugai na kufafanua kwamba amevumilia leo kutokana na ugeni mzito uliohudhuria.
  Ugeni huo ni pamoja na marais wastaafu, Mzee Ali Hassan Mwinyi wa
 Awamu ya Pili, Benjamin Mkapa wa Awamu ya Tatu, Jakaya Kikwete wa Awamu ya Nne, Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, mawaziri wakuu wastaafu, maspika wastaafu, mabalozi na viongozi wengine.
 Awali katika hotuba yake, Dk Magufuli alisema kilichofanywa na wabunge hao si kitendo cha kiungwana na ni aibu na utoto kwa hadhi ya Bunge.
 Aliwaeleza wabunge kwamba wote ni kitu kimoja na kuwa lugha za vijembe, mipasho, ushabiki wa vyama visiwe na nafasi katika Bunge hilo na kuwataka wazungumze masuala yao na si kwa njia ya kuzomea au kutoka nje kwani mambo hayo yanaaibisha Bunge.
 Dk Magufuli aliyetumia muda wa saa 1:38 akianza kuhutubia saa tisa na dakika 52 alasiri hadi saa 11 na nusu jioni, alisema kazi iliyo mbele ya wabunge ni kubwa katika kuwatumikia Watanzania.
 Alimpongeza Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo) kwa kuonesha ukomavu wa kisiasa na kusema kuwa hivyo ndivyo inavyotakiwa mwanasiasa awe.
   Jana wabunge wa kambi ya upinzani  kutoka vyama vya CUF, Chadema na NCCR Mageuzi walitolewa nje na Spika Ndugai baada ya kukaidi amri yake ya kuwataka wakae muda mfupi baada ya Rais kuingia ukumbini.
 Wabunge hao walianza kwa kuimba huku wakipiga meza na kusema: “Maalim Seif… Maalim Seif...(Katibu Mkuu wa CUF na mgombea urais wa Zanzibar),” walitoa kauli hiyo baada ya kutolewa tangazo bungeni la kuwasili wageni mbalimbali ndani ya ukumbi huo.
   Tukio hilo la fedheha lilianza saa tisa na nusu wakati Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho alipokuwa anaingia ukumbi hapo, pia dakika tatu baadaye lilijirudia wakati anaingia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd.
  Lakini hali ilionekana kuzidi wakati alipoingia Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein saa tisa na dakika 40, wakipiga meza na kumtaja Maalim Seif na hata alipoingia Dk Magufuli saa tisa na dakika 45 waliendelea kuimba kwa staili hiyo hiyo.
 Kutokana na hali hiyo, Spika Ndugai alitamka mara tatu wabunge hao wakae chini na wawe watulivu, lakini walikaidi amri hiyo hivyo kuwataka watoke nje kwa hiari yao.
 Pengine kwa kuhofia askari wa aina tofauti waliokuwepo nje na ndani ya ukumbi, wabunge hao bila kushurutishwa walitoka nje ya ukumbi na baadaye walitolewa kabisa nje ya viwanja vya Bunge.
    Awali Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu alianza kwa kuomba Muongozo wa Spika muda mfupi baada ya Bunge kutengua kanuni ya kuwaingiza ukumbini viongozi ambao kikatiba hawatajwi kuingia katika eneo hilo.
   Lissu alisema  ibara ya 28 (2) ya Katiba ya Zanzibar inasema Rais wa Zanzibar ataachia wadhifa huo miaka mitano baada ya kuapishwa na kwamba Dk Shein aliapishwa Novemba 3, 2010 hivyo muda wake kikatiba ulimalizika Novemba 2 mwaka huu.
    Akijibu muongozo huo, Naibu Spika, Dk Tulia Ackson alisema Tundu Lissu alisoma ibara ya 28 (2), lakini ibara ya 28(1) inasema Rais wa Zanzibar ataendelea kushika wadhifa huo hadi Rais mpya atakapoapa na kueleza kuwa Dk Shein ni Rais halali wa Zanzibar kikatiba.

#Habarileo  

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI