Tuesday, September 8, 2015

MASHA ADAI MASHTAKA DHIDI YAKE NI BATILI

ALIYEWAHI kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha (45) amewasilisha mahakamani pingamizi juu ya kesi inayomkabili ya kutumia lugha ya matusi kwa maofisa wa Jeshi la Polisi, akisema mashitaka aliyofunguliwa ni batili.
 
Kupitia kwa wakili wake, Peter Kitabala, Masha aliwasilisha pingamizi hilo akiwa na hoja tatu za kisheria katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.
 
Kesi hiyo ilikuwa umekuja kwa kutajwa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Waliarwande Lema ambapo Wakili wa Serikali, Sakina Sinda, aliomba iahirishwe kwa kuwa upelelezi haujakamilika.
 
Ndipo Wakili Kibatala akasema wamewasilisha pingamizi, kupinga uhalali wa mashitaka dhidi ya Masha na kwamba Septemba Mosi, mwaka huu walipeleka nakala ya pingamizi hilo kwa upande wa Jamhuri, hivyo walitarajia jana wangesikiliza.
 
Kutokana na hoja hiyo, Sakina aliiomba mahakama iwape muda ili wapitie pingamizi hilo na kuwasilisha majibu kwa sababu bado hawajaliona.
 
Katika pingamizi hilo, Masha anadai kwamba hati ya mashitaka ni batili, haina hadhi ya kisheria kwa kuwa maofisa wa polisi siyo miongoni mwa watu wanaohusishwa na kifungu cha 89 (1) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.
 
Anazidi kudai kwamba hati hiyo ni batili kwa kuwa imeshindwa kueleza ni kwa jinsi gani lugha ya matusi anayodaiwa kuitoa inaweza kusababisha uvunjifu wa amani. Aidha pingamizi linasema hati hiyo ni batili kwa kuwa maneno yanayodaiwa siyo ya udhalilishaji na ya matusi, hivyo hayawezi kutumika kama sheria inavyoeleza.
 
Hakimu Lema aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba mosi mwaka huu, itakapokuja kwa haua nyingine.
 
Katika shitaka hilo, Masha anadaiwa kwamba Agosti 24, mwaka huu katika kituo cha Polisi cha Oysterbay, alitoa lugha ya matusi kwa Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Juma Mashaka na wenzake akiwaambia ni “wajinga, washenzi, waonevu, hamna shukrani, huruma wala dini,” maneno ambayo polisi katika mashitaka yao wanadai yangesababisha uvunjifu wa amani.

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI