Wednesday, August 26, 2015

KUBENEA AZUNGUMZIA ALIVYOKAMATA SHAHADA BANDIA 100 ZA KUPIGIA KURA *VIDEO*

MGOMBEA Ubunge wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Jimbo la Ubungo, Saed Kubenea, amedai kuwa zaidi ya kadi milioni mbili za kupigia kura zinatengenezwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kwa ajili kuongeza kura za ziada za kukiwezesha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kushinda katika uchaguzi Oktoba 25, mwaka huu.


Kubenea alidai tayari amepata kadi 100 ambazo alidai amepatiwa baadhi ya maafisa wa Tume ambao walimuahidi kumpatia kadi nyingine zaidi. 



“NEC wameweka mkakati wa kukisaidia CCM kupata ushidi katika kufanikisha hilo wametengeneza kadi ambazo hazijajazwa taarifa zozote ambazo wanatarajia kuzitumia kwa kuingiza taarifa za watu ambao hawastahili ili wapige kura,”
“Tunashukuru kuna wasamaria wema ndani ya NEC ambao hawakubaliani na hujuma hizo, wameamua kutuambia na wametuahidi kutupa kadi nyingine zaidi, na huyo aliyenipa hizi 100 aliniambia hata nikitaka kadi hizo 100,000 atanipa.”



Kubenea alisema tayari amekabidhi kadi hizo kwa mwanasheria na kwamba kabla ya kuzikabidhi, aliapishwa kwanza.



“Naomba NEC iache kufanya kazi za CCM, kama itaendelea kufanya hivi itaipeleka nchi kwenye machafuko, tunaomba ifanye kazi kwa uadilifu na ninamuomba Mwenyekiti wa Tume hiyo asiipeleke nchi pabaya, hatutaki kuona watu ambao hawakuandikishwa wanaingizwa kwenye daftari,” 



Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji, Damian Lubuva, alisema hawezi kuzungumzia chochote kwa kuwa hajaziona kadi hizo.



“Kama CHADEMA wamesema kadi hizo ni za kwetu ni vema wangezileta kwetu ili tuone kama kweli ni zetu, kwa kuwa wamezungumza hayo kwenye mkutano na waandishi wa habari na mimi sijaziona kadi hizo siwezi kuzungumza chochote mpaka nidhibitishe”
“Hata nikizungumza hapa itaonekana tunabishana Tume na CHADEMA, wao kama kweli wanazo watuletee tuthibitishe.”

Naye mgombea ubunge wa Kawe, Halima Mdee, aliitaka Tume hiyo kuhakikisha inahakiki taarifa za wananchi katika vituo vya kupigia kura walivyojiandikishia na si katika kata.



Alisema taarifa ambazo amepata ni kwamba baadhi ya ofisi za wakurugenzi wameambiwa na NEC kwamba wananchi wao watahakiki taarifa zao katika ofisi za kata na si katika vituo walivyojiandikishia kama inavyotakiwa kutokana na uchache wa vitabu.



Jaji Lubuva alisema changamoto za uhakiki wa wapiga kura ni suala ambalo linashughulikiwa kwa kushirikiana na wakurugenzi na kwamba watahakikisha kila aliyejiandikisha anahakikiwa.



#CHADEMA Blog

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI