Saturday, July 4, 2015

JOKATE: MAPENZI YA STAA KWA STAA MBONA POA TU!


Jokate Mwegelo ‘Kidoti’.
*********
Saphyna Mlawa, Dar es Salaam
ANAJULIKANA kwa jina la Jokate Mwegelo ‘Kidoti’, alianza kupata umaarufu kupitia fani ya urembo lakini kwa sasa sauti yake kusikika kwenye Bongo Fleva na kazi zake za urembo ndizo zinamfanya asomeke kwenye vyombo vya habari.

 Mwanamuziki Ali Kiba.
Jokate ambaye alitumia alama iliyopo kwenye uso wake kujipa jina la utani la Kidoti, amezungumza na Championi Ijumaa katika mahojiano maalum:

Hivi nini maana ya jina la Jokate?
Ni muunganiko wa majina mawili, la kwanza ni Joachim ambalo ni jina la babu yangu na la pili ni Katalina ambalo ni jina la bibi yangu, hili jina nilipewa na mama yangu.
Wadada mmeanza kuamka kimuziki, upande wako kwa nini unafanya muziki na malengo yako ni nini?
(Anavuta pumziko kidogo kisha anajibu) Ninafanya muziki kwa sababu nina kipaji na ningependa watu waone ubunifu wangu kwenye hiki kipaji.
Unatumia njia gani kulinda urembo na mwonekano wako?
Aaah! (Anatabasamu, meno yake yaliyojipanga vizuri yanaonekana) Siri kubwa ya urembo wangu ni kwamba, mi nalala sana, naoga mara nyingi, nakula matunda mengi, nakunywa maji kwa wingi pamoja na kufanya mazoezi ya kutosha. 

Je, unategemea kuolewa lini? 
(Anacheka, mashavu yanatuna, si unajua kaanza kunenepa kwa mbaaali) Dah! Kwa kweli bado sijapanga, kifupi sitegemei kuolewa leo wala kesho na hiyo ndiyo mipango niliyojipangia, ila mambo yakikaa sawa nitakuja kuolewa, watoto wa mjini wanasema bado nipo nipo kwanza, ha! Ha! (anacheka tena sana)

Umepanga kuwa na watoto wangapi?
Kuzaa ni majaliwa ila kikubwa ningependa nizae watoto kuanzia watatu na kuendelea kwa sababu ninaamini uwezo wa kulea ninao kutokana na kujishughulisha kwangu, hivyo watoto wangu hawatalala njaa.

Unajua kupika? Kama ndiyo chakula gani unapenda kupika zaidi?
‘Yes, I can!’ Chakula ninachopendelea zaidi ni pilau kwa sababu hicho ndicho chakula kikubwa ninachopenda kukila.

Mapenzi ya watu maarufu yanaweza kuchangia kumkuza au kumpoteza msanii?
Sidhani kama mkiwa maarufu mkawa wapenzi mtakuwa mnapoteza ubora wenu katika kazi za usanii, ila kwa upande wangu naweza kusema inategemea ni jinsi gani mmeamua kuishi katika uhusiano na malengo yenu ni nini hasa, mkiwa na mipango mizuri mtaenda sawa. 

Wewe na Ali Kiba mna uhusiano gani?
Tuna uhusiano mzuri sana kwenye kazi kiasi kwamba anaweza kunishauri mahali ambapo ninakwenda ndivyo sivyo, mimi pia hufanya hivyo pindi anapohitaji ushauri, kwenye maisha binafsi mimi na Ali Kiba ni washikaji wakubwa tena sana na siyo kimapenzi kama watu wengi ambavyo wamekuwa wakizungumza vitu ambavyo havina ukweli wowote. 

Ulizaliwa wapi?
Nilizaliwa Washington DC nchini Marekani ambako wazazi wangu walikuwa wanafanya kazi miaka hiyo.

Tuelezee elimu yako kwa ufupi
Elimu yangu ya msingi nilisomea Olympio Primary School iliyopo Dar, O-level nilisoma katika Shule ya St Anthony, high school nilisoma Loyola High School na elimu ya chuo niliipata pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Neno lako kwa mashabiki wako...
Ninawapenda sana mashabiki wangu naomba waendelee kunisapoti katika kazi zangu na mimi ninawaahidi kutowaangusha, nitaendelea kutoa vitu vizuri na vinavyoteka hisia zao.
#GP

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI