Wednesday, April 22, 2015

SIMBA YA EMMANUEL OKWI YAIFUMUA MGAMBO JKT 4-0 LIGI KUU TANZANIA BARA UWANJA WA TAIFA DAR ES SALAAM


https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEij9KHVrPPq5tgUV-Jw9hoI9vuUguEbOTJnMzx_p9O5tV0ptcZgFJMcSS93gJqTKr5xNrLVA7iJdsTwxJ1gLXk2Ohp6TY9cYLbFvFo-cCIwpV2yaxSHVeY9K2XqtroMr3lRr_NUf90CZ8w/s1600/s4.jpg 
TIMU ya Wekundu wa Msimbazi Simba SC, leo imefuta machungu ya kupoteza mchezo uliopita jijini Mbeya dhidi ya Mbeya City baada ya kuwashushia mvua ya magoli wanajeshi wa Mgambo JKT kutoka jijini Tanga kwa kuwachakaza magoli 4-0 katika mchezo ulipigwa uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Simba wakiwa katika kiwango cha hali ya juu kabisa hii leo walianza kuliona lango la mgambo JKT mapema kabisa mnamo dakika ya 8 kupitia kwa mshambulizi wao machachari kutoka nchini Uganda Emmanuel Okwi baada ya krosi nzuri kabisa ya Ramadhan Kessy aliyegongeana pasi kwa uzuri na Ramadhan Singano 'Messi'.

Wakiendelea kupekeleka mashambulizi langoni mwa mgambo kama Mvua, Simba walifanikiwa kuandika bao la pili mnamo dakika ya 15 kupitia kwa winga wake msumbufu Ramadhan Singano 'Messi' kutokana na mpira wa adhabu aliouchonga kwa umaridadi wa hali ya juu na kuingia moja kwa moja wavuni huku akimuacha mlinda mlango wa Mgambo JKT Godson Mmasa akiwa hana la kufanya.

Mgambo walijitahidi kufanya shambulizi langoni mwa Simba mnamo dakika ya 26, lakini shuti la mshambuliaji wa Mgambo Malimi Busungu liliokolewa maridadi kabisa na mlinda mlango wa Simba Ivo Mapunda.

Simba waliendelea kulisakama lango la Mgambo JKT na hatimaye katika dakika ya 41 Okwi kwa mara nyingine tena aliweza kuifungia Simba bao la 3 baada ya mabeki Mgambo kujichanganya na yeye kumtoka mmoja wao kabla ya kuachia shuti kali na kutinga kimiani.

Mgambo walijaribu tena kutafuta goli langoni mwa Simba lakini ukosefu wa umakini kwa Salim Azizi Gilla uliwakosesha bao baada ya kufika langoni na kupaisha mpira juu.

Mvua ya ya magoli iliendelea kumiminika langoni mwa Mgambo baada ya Emmanuel Okwi kuifungia Simba bao la nne huku kwa upande wake likiwa ni bao la tatu la mchezo (hat-trck) mara baada ya kuwachambua mabeki wa Mgambo na kufunga goli kirahisi kabisa.

Mgambo walijitahidi kutafuta walau goli la kufutia machozi wakati walipopeleka shambulizi la kushtukiza langoni mwa Simba lakini hata hivyo Ivo Mapunda aliokoa na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Ilikuwa almanusura Simba waandike bao la tano baada ya Okwi kuwachambua kwa uzuri mabeki wa Mgambo na kumpasia mpira Jonas Mkude lakini shuti lake lilimlenga mlinda mlango wa Mgambo na kuudaka mpira huo.

Mapaka mwamuzi wa mchezo anapuliza kipyenga cha mwisho Simba waliibuka na ushindi mnono wa mabo 4-0 dhidi ya Mgambo kutoka jijini Tanga huku nyota wa mchezo wa leo Emmanuel Okwi akijiondokea na mpira wake baada ya kukwamisha kimiani mabao matatu (hat-trick).

Ikumbukwe tu hiki ni kigo cha pili kizito ambacho Simba imekitoa kwa Mgambo JKT ikiwa mwaka jana wakiifunga magoli 6-0 katika dimba la Taifa huku Amissi Tambwe ambaye kwa sasa yupo Yanga akipiga hattrick pia.

Tangu ipande daraja timu ya Mgambo JKT imekutana na Simba mara 6 na kushinda mara mbili, huku wao wakipoteza mara tatu na kutoka sare mara moja.

Sio Simba wala Mgambo ambaye amewahi kupata ushindi nyumbani kwa mpinzani wake isipokuwa Mgambo iliwahi kupata sare mbele ya Simba katika dimba la Taifa jijini Dar es Salaam.

Katika mchezo baina ya Polisi Moro SC na Coastal Union umemaliza kwa kushindwa kutambiana.

kutokana na matokea hayo Coastal Unioni imejiongezea pointi moja na kufikisha 28 huku Polisi Moro ikifikisha pointi 25 baada ya kugawana pointi moja moja kufuatia sare tasa ya 0-0 katika uwanja wa jamhuri Morogoro.

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI