Saturday, November 1, 2014

RAIS WA BURKINA FASO APINDULIWA MADARAKANI, NI BAADA YA MAANDAMANO YA KUPINGA KUJIONGEZEA MADARAKA

JESHI la Ulinzi la Burkina Faso, limechukua madaraka na kutangaza kuvunja Serikali na Bunge la nchi hiyo, baada ya kuibuka kwa maandamano ya muda mrefu ya kupinga utawala wa miaka 27 ya Rais Blaise Compaore. 
Mbali na kuchukua madaraka, taarifa ya Mkuu wa Jeshi hilo, Nabere Traore, iliyosomwa na mmoja wa maofisa wa jeshi hilo juzi na kutakiwa kutolewa jana, imeeleza kuwa jeshi hilo litaunda chombo kitakachoongoza nchi hiyo ambacho kitatakiwa kurejesha utawala wa kidemokrasia ndani ya miezi 12. 
Jana asubuhi mmoja wa maofisa wa jeshi hilo, Kanali Boureima Farta, alitangazia umati wa waandamanaji kuwa Rais Compaore, amepinduliwa na kuibua kelele za shangwe miongoni mwa waandamanaji hao. 
"Kuanzia leo, Compaore hatakuwepo madarakani,” alisema Kanali Farta akiwa amesimama juu ya mabega ya wanajeshi wenzake mbele ya Makao Makuu ya Jeshi hilo, ambayo yalikuwa yamezingirwa na waandamanaji waliokuwa wakikadiriwa kuzidi elfu kumi. 

Compaore, ambaye amekuwa madarakani kwa zaidi ya miaka 27, Alhamisi wiki hii alikataa shinikizo la kujiuzulu lililokuwa likitolewa na waandamanaji hao, waliokuwa wakipinga jaribio lake la kurekebisha Katiba, ili kujiongezea muda wa kukaa madarakani. 
Alisema hakuwa na nia ya kugombea tena madaraka hayo, lakini ataendelea kuwa madarakani mwaka wote wa 2015 kusimamia kuanzishwa kwa utawala mpya. 
Hata hivyo, Shirika la Habari la Kimataifa la Reuters, lilieleza kuwa Kituo cha Redio cha Omega katika nyakati tofauti kilitangaza kwamba Compaore alitoa tamko la kujiuzulu na kusema kuwa nafasi ya Mkuu wa Nchi ilikuwa wazi. 

Kabla ya kupinduliwa kwa Serikali ya Compaore jana mchana, asubuhi wananchi waliendelea kuandamana, pamoja na kuwepo kwa tamko la Rais huyo kwamba hatawania nafasi hiyo kwa mara nyingine. Mbali na kutamka kutowania nafasi hiyo kwa mara nyingine, Compaore pia aliahidi kukutana na vyama vya upinzani na asasi za kiraia, ili kuanzisha utawala wa muda kabla ya Uchaguzi Mkuu. 
Vyama vya upinzani nchini humo, vimekuwa vikidai kuwa karibu watu 30 wameuawa huku wengine 100 wakijeruhiwa katika maandamano makubwa yaliyofanyika Alhamisi. 
Mashuhuda wa maandamano hayo, wamedai kuwa baadhi ya watu walitumia nafasi hiyo kupora maduka ambapo baadhi walionekana wakiwa wamebeba viroba vya sukari na mchele. Redio ya Taifa na Televisheni ya Taifa ya nchi hiyo, vilisitisha matangazo yake na hata mawasiliano ya Intaneti, yaliingiliwa na vyombo vya usalama. 
Katika hatua nyingine habari kutoka Lusaka, Zambia, zimeeleza kuwa mwili wa Rais wa nchi hiyo, Michael Sata, aliyefariki mjini London Uingereza baada ya kuugua kwa muda mrefu, utasafirishwa kurudi nchini kwake leo. 
Katibu wa Baraza la Mawaziri la nchi hiyo, Roland Msiska, alitamka juzi kuwa Sata atazikwa Lusaka, Novemba 11 mwaka huu. 

Aidha, jana Jeshi la Polisi nchini humo lilitangaza kumkamata mmoja wa viongozi wa juu wa zamani wa nchi hiyo, Guston Sichilima, ambaye amewahi kushika nafasi za Naibu Waziri wakati wa utawala wa Rupia Banda, kwa kufanya sherehe huku akirusha risasi angani wakati Taifa likiomboleza kifo cha Rais 

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI