Thursday, October 16, 2014

JINSI LORI LA MAFUTA LILIVYOSABABISHA VIFO VYA VYA WATU WATATU NA KUTEKETEZA BAA NA NYUMBA YA KULALA WAGENI DAR ES SALAAM


MATARAJIO ya neema ya kujipatia mafuta ya 'dezo’ kutoka katika lori lililoanguka eneo la Mbagala Rangi Tatu jijini Dar es Salaam, juzi usiku yaligeuka majuto na kuibua vilio na simanzi, baada ya kulipuka na kusababisha maafa, ikiwa ni pamoja na vifo vya watu watatu, huku wengine saba wakijeruhiwa vibaya.

Aidha, moto huo uliteketeza kabisa baa moja, nyumba ya kulala wageni yenye vyumba 32 na maduka manne ya vyakula.

Hayo yalithibitishwa jana na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Wankyo Nyijesa aliyemtaja aliyefariki dunia papo hapo kuwa ni Masoud Masoud huku wengine waliokufa baada ya kufikishwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) wakishindiwa kutambuliwa mara moja.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki aliyetembelea majeruhi katika Hospitali ya Muhimbili na baadaye eneo la tukio, alisema mtu mmoja alifariki papo hapo na watu wawili kati ya 15 waliokimbizwa hospitalini hapo walifariki wakiwa wanapatiwa matibabu.

“Kati ya waliokimbizwa Muhimbili wawili wamepoteza maisha na wengine takribani saba hali zao ni mbaya, hivyo kuna hatari ya kupoteza maisha ya watu wengine zaidi. Watu wanne waliolazwa katika hospitali ya Temeke hali zao ni nzuri kidogo,” alisema Sadiki.

Akizungumzia tukio hilo, mmoja wa mashuhuda aliyejitambulisha kwa jina la Laurent Kasigwa alisema tukio hilo lilitokea majira ya saa tano usiku na kuwa baada ya lori hilo kuanguka wananchi walikimbilia kuchota mafuta.

Alisema kutokana na umeme kukatika katika eneo hilo, mmoja wa watu hao aliwasha mshumaa ili aweze kuchota mafuta hayo kwa urahisi, lakini hali ilikuwa kinyume kwani lori hilo lililipuka na kuwaka moto.

Mbali na vifo na majeruhi, moto huo pia umeteketeza maduka manne, baa moja na nyumba ya kulala wageni inayoitwa United States Guest House yenye vyumba 32 ambavyo vyote vimeungua.

Kutokana na tukio hilo, Mkuu wa Mkoa amewataka Watanzania kuacha tabia ya kukimbilia eneo la ajali pale inapotokea malori ya mafuta yameanguka, kwani ni hatari kwa usalama wa watu na mali zao.

“Hata kama ni suala la ugumu wa maisha vitendo hivyo ni hatari, unakwenda kuchota lita moja ya mafuta itakusaidia nini na wakati unahatarisha maisha yako?” alihoji Mkuu wa Mkoa.

Katika kupambana na majanga, Sadiki alisema tayari serikali imeshaamua kuweka mtandao wa vikosi vya uokoaji badala ya kutegemea kuwa sehemu moja tu.

“Tulishafikia uamuzi wa kuwa na mtandao wa kuwa na vikosi vya uokozi katika maeneo ya kadhaa, ikiwa ni tofauti na sasa iko sehemu moja, suala hili linachosubiri ni utekelezaji kwani kuna mambo ya wafanyakazi na mahali,” alisema.
Chanzo: HABARILEO

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI