Friday, August 8, 2014

WANAOHISIWA KUWA NI MAJAMBAZI WAPORA FEDHA NA KUUA NDUGU WAWILI

NDUGU wawili wameuawa na majambazi waliovamia baa eneo la Mwananyamala kwa Mama Zacharia, jijini Dar es Salaam na kupora mkoba uliokuwa na fedha zaidi ya Sh milioni mbili.
Tukio hilo ni la juzi usiku na waliouawa ni Jeremiah Tarimo (37), mkazi wa Kimara na Nestor Tarimo (49) maarufu kwa jina la ‘Mangi Shasha’, mkazi wa Mwananyamala Kisiwani.
Hali ya taharuki ilizuka eneo hilo baada ya wakazi wake kusikia milio ya risasi na kusababisha maduka na nyumba kufungwa kwa hofu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura alithibitisha tukio hilo jana na kusema lilitokea saa 1.45 usiku katika baa ya Mahamo.
Alisema majambazi hao baada ya kufanya mauaji walitokomea na pikipiki ambayo hakuitaja namba zake za usajili kwa sababu za kichunguzi.
Ndugu wa marehemu ambaye alikuwa na mkoba ulioporwa, Mwajuma Jeza, mkazi wa Mbezi Louis, alisema alikuwa amekaa kwenye baa hiyo na ndugu zake wakati wa tukio hilo.
"Mwanamke huyo alikuwa na mkoba ambao ulikuwa na fedha karibu Sh milioni mbili, simu ya mkononi, kadi za benki na funguo. Aliingia kijana katika baa hiyo akaenda kupora mkoba huo, kukawa na purukushani ndipo wenzie wawili waliinuka kumsaidia," alisema Wambura.
Wambura alisema walitokea vijana wengine wawili ambao walivyatua risasi tatu ikampiga Jeremiah ubavu wa kulia na kumpiga tumboni Nestor.
Alisema wale majambazi walitokomea kwa katumia pikipiki na ndugu hao wawili walifariki wakati wakipatiwa matibabu hospitali ya Mwananyamala.

0 comments:

Post a Comment