Sunday, June 22, 2014

SERIKALI YAKWAA KISIKI HIFADHI YA SERENGETI

MAHAKAMA ya Afrika Mashariki (EACJ), imeizuia Serikali ya Tanzania kujenga barabara ya lami kupitia Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, ikieleza kuwa ujenzi huo utaathiri mazingira, maisha ya wanyamawwpori na baoanuai ya hifadhi hiyo.
Katika hukumu iliyotolewa jijini Arusha jana, jopo la majaji watatu wa mahakama hiyo wakiongozwa na Jaji Kiongozi Jean Bosco Butasi, liliiamuru Tanzania kutotekeleza mradi wowote wa ujenzi au ukarabati wa barabara hiyo utakaokuwa na madhara kwa mazingira na baoanuai ya hifadhi ya Serengeti.
"Zuio la kudumu linatolewa dhidi ya mdaiwa (Tanzania) kutekeleza mipango ya awali au pendekezo la ujenzi au ukarabati wa barabara kwa kiwango cha lami kupitia Hifadhi ya Serengeti itakayosababisha madhara kimazingira na baoanuai ya hifadhi hiyo," inasema sehemu ya hukumu hiyo.
Kila upande umeamriwa kubeba gharama zake katika shauri hilo lililoshuhudia mgawanyiko kati ya taasisi na mashirika yasiyo ya kiserikali, kwa yale ya Tanzania kuunga mkono ujenzi huo kwa madai kuwa una faida kwa maisha na jamii inayoishi maeneo itakayopita barabara hiyo
Kwa mujibu wa mpango wa Serikali, barabara hiyo ingepitia Mto wa Mbu-Engaruka-Loliondo- Kleins Gate-Serengeti-Mugumu-Nata na kuungana na ile ya Tarime-Musoma-Mwanza, hivyo kupunguza adha ya usafiri kwa wananchi wa maeneo haya ambao baadhi hulazimika kupitia Nairobi nchini Kenya.
Hukumu hiyo ilitolewa baada ya Taasisi ya Africa Network For Animal Welfare (ANAW), ya jijini Nairobi, Kenya kufungua kesi dhidi ya Serikali ya Tanzania kupinga ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa Kilomita 239, ikidai itaathiri mazingira, uhai wa wanyama na baionuai wa Hifadhi ya Serengeti kwa kuongeza shughuli za kibinadamu.
Akisoma hukumu hiyo kwa niaba ya majaji wenzake, Jaji Isaac Lenaola alisema Serikali ya Tanzania ina haki ya kutunga sera na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa ajili ya umma, lakini sharti izingatie upembuzi yakinifu kuepuka athari za kimazingira na baoanuai.
Jaji wa tatu katika jopo hilo ni Jaji John Mkwawa kutoka Tanzania ambaye anakamilisha mkataba wake mwishoni mwa mwezi huu. Nafasi yake tayari imejazwa na Jaji Fakih Jundu ambaye hadi uteuzi wake Aprili 30, mwaka huu, alikuwa Jaji Kiongozi.
Hukumu hiyo inasema kuwa licha ya haki ya nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kupanga na kutekeleza miradi na majukumu ya msingi kwa maendeleo ya wananchi, mipango hiyo lazima izingatie hoja ya kidunia ya ulinzi na uhifadhi wa mazingira, maendeleo endelevu, sheria na sera za kimataifa kuhusu mazingira na maliasili.
Mahakama imekubaliana na hoja za walalamikaji waliokuwa wakiwakilishwa kwenye shauri hilo na wakili Saitabao Ole Kanchory kuwa ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa Kilomita 239, ungeathiri mazingira na baionuai ya Hifadhi ya Serengeti nchini Tanzania na Maasai Mara nchini Kenya kwa kuwa kungeongeza shughuli za kibinadamu.
Hukumu hiyo inasema kuwa licha ya ukweli kwamba Serikali ya Tanzania ilipanga kuacha barabara yenye urefu wa Kilomita 53 inayopita ndani ya hifadhi katika kiwango cha changarawe, bado magari mengi yangepita kwenye barabara hiyo iwapo itajengwa kwa kiwango cha lami.
Ujenzi wa barabara hiyo ungetekelezwa ungekiuka ibara za 5(3), 8(1), 111(2) na 114 (1) ya mkataba wa EAC, zinazozungumzia wajibu wa kila nchi mwanachama kupanga na kutekeleza sera na miradi yote iliyo chini ya mamlaka na wajibu wao kwa kuzingatia ulinzi na uhifadhi wa mazingira kwa faida na masilahi ya jumuiya nzima.

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI