Tuesday, May 20, 2014

WAANDISHI WA SHERIA KUNOLEWA

 
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Angellah Jasmine Kairuki (kushoto) akimsikiliza Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Maendeleo (UNDP) Bw. Philippe Poinsot alipomtembelea Naibu Waziri ofisini kwake, Mtaa wa Mkwepu, jijini Dar es Salaam leo (Jumatatu, Mei 19, 2014). Kulia ni Naibu wake anayeshughulikia Programu Bi. Mandisa Mashologu
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Angellah Jasmine Kairuki akiagana na Naibu Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Maendeleo (UNDP) Bi. Mandisa Mashologu (kulia) alipomtembelea Naibu Waziri ofisini kwake, Mtaa wa Mkwepu, jijini Dar es Salaam leo (Jumatatu, Mei 19, 2014). Katikati ni Mkurugenzi Mkazi wa UNDP Bw. Philippe Poinsot. (Picha na Wizara ya katiba na Sheria)
SERIKALI kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Maendeleo (UNDP) inatarajia kutoa mafunzo kwa Waandishi wa Sheria kwa lengo la kuwaongezea uwezo wa kuandaa miswada katika lugha ya kiswahili – lugha ambayo inatumiwa na watanzania wengi.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Angellah Jasmine Kairuki amemwambia Mkurugenzi Mkazi wa UNDP Bw. Philippe Poinsot kuwa kwa sasa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inatekeleza mkakati wa kuandaa miswada yote inayosilishwa Bungeni katika lugha mbili, Kiingereza na Kiswahili ili kuwawezesha wananchi wengi kuisoma.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Naibu Waziri Kairuki, katika kutekeleza kazi hiyo, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Uandishi wa Sheria inakabiliwa na changamoto kadhaa zikiwemo uhaba wa watumishi na uwezo na hivyo kuhitaji msaada wa mafunzo.
“Kwa sasa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ina kazi ya kuandaa miswada katika lugha mbili ikiwemo Kiswahili ambayo ndiyo lugha ya taifa ambayo wananchi wengi wanaifahamu,” alisema Bi. Kairuki katika mkutano wake na Bw. Poinsot leo (Jumatatu, Mei 19, 2014) jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo ulifanyika katika ofisi ya Naibu Waziri Kairuki jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. George Masaju, Mkurugenzi wa Mashtaka Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi, Naibu Mwakilishi Mkazi wa UNDP Bi. Mandisa Mashologu na maafisa wengine waandamizi wa serikali.
Akizungumza katika mkutano huo, Bw. Masaju alisema kwa sasa Ofisi yake ina Waandishi wa Sheria 18 tu na kuwa idadi hiyo ni ndogo ikilinganishwa na majukumu ya Idara ya Uandishi wa Sheria.
“Serikali imeanzisha utaratibu huu wa kuandaa miswada katika lugha mbili lakini tuna changamoto ya uhaba wa watumishi na hata hao waliopo, walifundishwa kuandaa miswada katika lugha ya kiingereza na hivyo kuhitaji mafunzo,” alisema Bw. Masaju.
Akiongea katika mkutano huo, Bw. Poinsot alisema Shirika lake limepokea maombi ya Serikali na kuwa litayafanyia kazi kwa kushirikiana na Serikali ili hatimaye miradi hiyo itekelezwe.
“Kwetu sisi UNDP, sekta ya sheria ni muhimu sana hususan katika miradi inayolenga kuwasaidia masikini na kujenga uwezo … ndiyo maana tupo tayari kuisadia,” alisema kiongozi huyo wa UNDP hapa nchini.
Kwa mujibu wa Bw. Poinsot, Shirika lake limepanga kuisaidia Serikali kupitia mradi wake unaolenga kuimarisha usimamizi wa utoaji haki (Strengthening Administartion of Justice Project). Miradi ya awali inatarajiwa kuanza kutekelezewa hivi karibuni kabla ya kuanza kutekelezwa kwa awamu ya pili ya Mpango Maalum wa Shirika hilo (UNDAP II) unaotarajia kuanza kutekelezwa mwezi Januari 2015.
Maeneo mengine ambayo Serikali na UNDP zinatarajia kushirikiana ni katika utoaji wa huduma za msaada wa kisheria; kuimarisha uwezo wa waendesha mashtaka na watumishi wa mahakama; na kuboresha mifumo ya uendeshaji ili kupunguza mlundikano wa kesi mahakamani.
Mwisho.
Omega S. Ngole,
Head - Government Communication Unit,
Ministry of Constitutional and Legal Affairs,
PO Box 70069,
Dar es Salaam,
Tel: +255 (0) 22 2137823,
Fax: +255 (0) 22 2137831,
Mobile: +255 (0) 757 500800,
Website: www.sheria.go.tz
Facebook:www.facebook.com/people/Omega-Ngole
Twitter: https://twitter.com/OmegaNgole

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI