TANZANIA, Taifa Stars imeshinda mechi ya pili mfululizo nyumbani chini ya kocha mpya, Mholanzi Mart Nooij baada ya kuilaza 1-0 Malawi katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Israel Nkongo aliyesaidiwa na Hamisi Chang’walu na Jesse Erasmo wote wa Tanzania, Taifa Stars ilikwenda mapumziko ikiwa tayari inaongoza kwa bao hilo.
Bao hilo lilifungwa na kiungo mkongwe, Amri Ramadhani Kiemba wa Simba SC dakika ya 35 kwa shuti kali baada ya kupokea krosi pasi nzuri ya mchezaji wa AS Cannes ya Ufaransa, Shomary Kapombe kutoka wingi ya kulia.
Mfungaji wa bao la Stars Amri Kiemba baada ya kufunga
Awali, Kapombe aliyekuwa anacheza kama kiungo wa ulinzi jana, alilazimika kumpokonya mpira mchezaji hatari wa Malawi, Gabadinho Mhango na kugongeana vizuri na kiungo wa Azam FC, Kevin Friday kabla ya kutia krosi hiyo.
Timu zilishambuliana kwa zamu kipindi cha kwanza na Malawi inayofundishwa na beki wake wa zamani Young Chimodzi ikiongozwa na mkali wake wa mabao Gabadinho ilikosa bahati tu ya kufunga, lakini ilicheza vizuri.
Kipindi cha pili, Nooij alibadilisha karibu timu nzima iliyoanza na kuingiza wachezaji ambao wanajulikana kama chaguo la kwanza, ambao hata hivyo hawakubadilisha matokeo zaidi ya sura ya timu uwanjani.
Winga wa Taifa Stars, Simon Msuva akimtoka beki wa Malawi, Young Chimodzi Jr. katika mchezo wa leo Uwanja wa Taifa.
Kipa Deo Munishi ‘Dida’ wa Yanga SC, alifanya kazi ya ziada dakika ya 86 baada ya kupangua shuti kali la ndani ya boksi la Rodrick Gonani.
Mchezo huu ulikuwa maalum kwa kila timu kujiandaa na mchezo wa marudiano wa hatua ya kwanza ya mchujo kuwania kupangwa kwenye makundi ya kugombea tiketi ya Fainali za Mataifa ya Afrika mwakani Morocco.
Tanzania baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Zimbabwe na Malawi ikitoka kuifunga 2-0 Chad, zote zitakuwa ugenini wikiendi hii kujaribu kutafuta nafasi ya kusonga mbele.
Kikosi cha Tanzania leo kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Himid Mao, Edward Charles, Said Mourad, Joram Mgezeke/Kevin Yondan dk72, Shomary Kapombe, Simon Msuva/Ramadhani Singano ‘Messi’ dk46, Erasto Nyoni/Frank Domayo dk76, Kevin Friday/Said Juma dk73, Amri Kiemba/Mwinyi Kazimoto dk73 na Khamis Mcha ‘Vialli’.
Malawi; Richard Chipuwa, Moses Chabuvula/Francis Mulimbika dk79, Limbikani Mzava/Bashiri Maunde dk57, John Lanjesi, Foster Namwera, Philip Masiye, Young Chimodzi Jr.,Gabadinho Mhango, Chimango Kaira, Joseph Kamwendo/Frank Banda dk67, Atusaghe Nyondo/Robin Ngalande dk30.
0 comments:
Post a Comment