Tuesday, April 8, 2014

RAIS KIKWETE APONGEZWA


Bw. Stanley Bergman akiteta jambo na Balozi Manongi wanaonekana pia wageni waalikwa waliojitokeza kwa wingi kwenye hafla hiyo.
Rais na Mwanzilishi wa MCW, Bw. Eddie Bergman akielezea historia ya Taasisi hiyo ambayo aliianzisha ( 1999) akatumia fursa hiyo kutoa shukrani zake kwa wadau , wafadhili na marafiki mbalimbali ambao wameendelea kuiwezesha Taasisi hiyo na hatimaye kupitia kwayo kusaidia jamii katika maeneo mbalimbali na uwezeshaji wa vijana.
Bw. Stanley Bergman, Mwenyekiti na CEO, Henry Schein Inc akizungumza wakati wa hafla ya miaka kumi ya uchangiaji wa Taasisi ya Miracle Corners of the World ( MCW) ambayo pia imetimiza miaka kumi na tano ya kuanzishwa kwake, katika mazungumzo yake alitoa shukrani na pongezi kwa Mhe. Rais Jakaya Kikwete kwa namna ambayo amekuwa akishirikiana na Taasisi hiyo ambayo inaendesha shughuli hususani uboreshaji na uimarishaji wa huduma ya afya ya kinywa.
Mhe. Balozi Tuvako Manongi Muwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, akisema machache wakati wa hafla hiyo.
Sehemu ya wageni waalikwa, aliyekaa mstari wa mbele ni Bw. Ali Velshi ambaye alikuwa ndiye mshereheshaji wa hafla hiyo. Bw. Velshi ni mtangazaji maarufu wa vipindi vya Biashara katika Televisheni ya CNN hivi sasa amehamia Al Jazeera Amerika
Balozi Manongi akiwa na Mwanamziki Maarufu Kanda Bongo Man, kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kanda Bongo Man alikuwa mmoja wa wageni waalikwa na kama alivyo Balozi Manongi naye pia ni Mwenyekiti wa Heshma wa MCW.
Na Mwandishi Maalum
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, ameelezwa kuwa ni kiongozi ambaye amekuwa akitoa ushirikiano mkubwa kwa Taasisi zisizokuwa za kiserikali na hivyo kuchagiza kasi ya taasisi hizo kuwekeza katika miradi ya kijamii nchini Tanzania.
Kauli hiyo imetolewa na Bw. Stanley Bergman, Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa Henry Schein Inc, wakati wa hafla ya miaka kumi ya uchangiaji wa shughuli za Taasisi ya Miracle Corners of the World ( MCW) hafla iliyokwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 15 tangu kuanziswa kwa Taasisi hiyo yenye makazi yake Jijini New York, nchini Marekani.
Hafla hiyo ilifanyika usiku wa Jumatatu na kuhudhuriwa na wageni wa kada mbalimbali yakiwamo makampuni makubwa kama vile NASDAQ OMX, CITI na the UPS Foundation ambayo yamekuwa yakichangia shughuli za Taasisi hiyo. 
Miongoni mwa wageni waalikwa alikuwa ni Muwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi.
MCW ilianzishwa mwaka 1999 na Bw. Eddie Bergman ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka kumi na mitano, inajihusisha miradi ya kijamii ikiwamo ya huduma za afya, na uwezeshaji wa vijana na kukuza ushirikiano na Taasisi nyingine.
Taasisi hii ilianza shughuli zake kwa kuanzisha kituo cha vijana jijini Arusha na baadaye ikasambaza huduma zake katika mikoa ya Iringa, Dar es Salaam, Ruvuma na Zanzibar.
“ MCW inajivunia ushirikiano na uhusiano wa karibu na Rais wa Tanzania Mhe. Rais Jakaya Kikwete, ambaye muwakilishi wake Balozi Manongi yupo pamoja nasi usiku huu. Ni ushirikiano na msaada wake wa hali na mali ndio unaoifanya MCW iendele kutoa huduma zake nchini Tanzania. Napenda kutumia fursa hii kumshukuru sana Rais Kikwete”. Akasema.
Katika miaka yake 15 ya shughuli zake hususani uwezeshwaji wa vijana kutambua vipaji vyao vya uongozi na kubwa zaidi uimarishaji na uboreshaji wa huduma ya afya hususani afya ya kinywa. MCW imekuwa ikishirikiana kwa karibu sana na Chuo Kikuu cha Tiba na Sayasi (MUHAS) katika kuimarisha na kuboresha Kitivo cha Meno kwa maana ya vifaa , mafunzo na miundo mbinu.
Ni katika hafla hiyo, ambapo Rais na Mwanzilishi wa MCW, Bw. Eddie Bergman wakati akielezea mafanikio ya Taasisi hiyo alieleza kwamba kontena lililokuwa na vifaa vyenye thamani ya dola za kimarekani 500.000 lilikuwa limewasili jijini Dar es Salaam ambapo kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Bohari Kuu ya Madawa, ( MSD) kontena hilo limeshatolewa bandarini na kukabidhiwa Chuo Kuu cha MUHAS.
Dkt. Marion Bergman ambaye ni Mkurugenzi wa miradi ya Afya katika MCW alishuhudia kuwasili kwa kontena hilo na makabidhiano.
Wakati wa hafla hiyo ya jumatatu jumla ya dola za kimarekani 950,000 zilichangwa kwa madhumuni ya kufanikisha shughuli za Taasisi hiyo ambayo sasa inazihusisha pia Zambia, Rwanda na Sierra Leone.
Akizungumza katika hafla hiyo, Balozi Manongi, alieleza kwamba Tanzania imekuwa mmoja wa wanufaikaji wakubwa wa MCW na kwamba Tanzania itaendelea kuenzi shughuli zake ambazo zimelenga katika kuinua na kuimarisha huduma za afya katika maeneo ya pembezoni mwa Tanzania.
Baadhi ya washiriki waliopewa fursa ya kuzungumza na ambao wamekuwa wakifanya kazi kwa karibu na MCW walieleza kwamba kwa kuja kwao Tanzania na kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na wadau mbalimbali wakiwamo vijana na wataalamu wa afya, si tu kwamba wao wametoa, lakini uzoefu walioupata katika maeneo waliyokwenda umewabadili kifikra na kimtazamo na kwamba wapo tayari wakati wowote kurejea tena Tanzania.

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI