Tuesday, March 11, 2014

WALIOKWAMISHA UJENZI WA MIUNDOMBINU MLOGANZILA SASA WARUHUSU UJENZI KUENDELEA

Wengine kutoka  kushoto ni Katibu Tawala wa mkoa wa Dar es salaam Bi.Therezia Mmbando,Mkurugenzi Mkuu wa DAWASA Bw. Archard Mutalemwa na Meneja wa Tanroad mkoa wa Dar es salaam Bw. Ndyamukana Julius.
Picha na 4Mkazi wa eneo la Mloganzila Bw. Fredy Justine Masondole (Katikati) akiwapeleka katika eneo la nyumba yake lenye mgogoro viongozi wa mkoa wa Dar es salaam wakiongozwa na Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Saidi Meki Sadiki (upande wa nyuma katikati), mkuu wa wilaya ya Kinondoni Jordan Lugmbana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es salaam Bi. Theresia Mmbando.
Picha na 5Mafudi wakiendelea na ujenzi wa awali wa ofisi za muda katika eneo itakapojengwa Hospitali na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili(MUHAS) lililo kwenye mpaka wa wilaya ya Kisarawe na mkoa wa Pwani leo
……………………………………………………………………………………………… 

BAADHI ya wakazi wa eneo la Mloganzila waliokuwa wamezuia maeneo yao kutumiwa kupitisha miundombinu ya maji, barabara na umeme kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili(MUHAS) wamekubali kuyatoa maeneo yao ili kuruhusu kuendelea kwa ujenzi wa miundombinu hiyo.
 
Wakazi hao waliozuia ujenzi huo kwa madai ya kutolipwa fidia na baadhi yao kwenda mahakamani wamefikia uamuzi  huo leo mara baada ya mazungumzo baina yao na mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Mh. Saidi Meki Sadiki aliyetembelea eneo la mradi huo.
 
 Akiwa katika eneo la ujenzi wa mradi huo unaojengwa na Kampuni ya Colon Global Corporation kutoka Korea, Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mh. Saidi Meki Sadiki amesema kuwa mradi huo kwa muda umeshindwa kuendelea kutokana na kukosekana kwa maji,umeme na miundombinu ya barabara.
 
Amesema mkandarasi alikwisha onyeshwa eneo hilo la ujenzi toka Februari 23 na kuongeza tayari makabidhiano ya eneo hilo lililo mpakani mwa wilaya ya Kisarawe na mkoa wa Pwani yamekwishafanyika.
 
“Ujenzi wa hospitali hii kubwa na chuo Kikuu cha Afya na Tiba ni moja ya ahadi ya Rais Jakaya Kikwete, Mh. Rais aliahidi na kama  mnavyoona ujenzi huu umeanza lakini umekwamishwa na baadhi ya wananchi wachache na kama serikali tumeona si vema tuendelee kuchelewesha ujenzi wake” Amesema.
 
Amesema mkoa kwa kushirikiana na Shirika la Ugavi wa Umeme nchini (TANESCO), Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es salaam (DAWASCO) na Wakala wa Barabara Nchini (TANROAD) umekaa kwa pamoja ili kupata ufumbuzi wa mgogoro huo ili kuruhusu kuanza kwa ujenzi wa mradi huo haraka iwezekanavyo.
 
“Tumekua na mazungumzo na wenzetu hawa na leo tulikua na kikao cha pamoja ili tupate ufumbuzi wa suala hili na tayari wakazi hawa wawili ambao nyumba zao ziko kwenye eneo yatakapopita mabomba ya maji, nguzo za Umeme na Barabara tumezungumza nao na tayari wamekubali na kesho ujenzi unaendelea” Amesisitiza.
Ameongeza kuwa wamiliki wa maeneo hayo wamekubali busara itumike kwa wao kuruhusu mradi huo uendelee na kufafanua kuwa tathmini ya nyumba na maeneo yao inaendelea kufanyika ili waweze kulipwa stahiki zao.
 
“Tumeamua busara itumike ili kuokoa muda unaozidi kupotea na kuchelewesha ujenzi wa mradi huu mkubwa wenye manufaa kwa wananchi,licha ya kwamba baadhi yao wamekwishapeleka madai yao mahakamani”
Kuhusu sehemu ya eneo la mradi huo linalomilikiwa na JWTZ, Mh. Sadiki amesema kuwa atakwenda kuzungumza na Mamlaka husika ili kupata ufumbuzi wa jambo hilo na kutoa wito kwa wananchi ambao tayari wamekwisha pokea fidia zao kupisha ujenzi wa mradi huo.
 
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO Mhandisi Felchian Mramba akiwa katika eneo la tukio ameeleza shirika lake limeshindwa kufikisha umeme katika eneo husika kutokana na zuio lililowekwa na wananchi hao na kuongeza kuwa muafaka uliofikiwa leo ni faraja kwao kuwezesha kazi hiyo kuendelea.
“Sisi baada ya maelewano haya ni kazi kuendelea na kesho kazi ya kupitisha nguzo na nyaya inaendelea” amesisitiza.
 
 Mkurugenzi Mkuu wa DAWASA Bw. Archard Mutalemwa amefafanua kuwa tayari wao kama wahusika wakuu wa usambazaji wa miundombinu ya maji wameshalaza miundobinu hiyo kwa 50%, kujenga mnara wa tenki kubwa la maji, kununua vifaa na kuongeza kuwa wamejipanga kukamilisha kazi hiyo kwa muda uliopangwa.
 
Naye Meneja wa TANROAD mkoa wa Dar es salaam Bw. Ndyamukana Julius ameeleza kuwa ujenzi wa barabara za eneo hilo utakamilika mwezi Agosti mwaka huu.
“Sisi tumejipanga vizuri kukamilisha ujenzi huu kwa kushirikiana na wenzetu ili kufikia tarehe 22 Agosti  mwaka huu tukamilishe kazi” Amesema.


Picha na Habari na Aron Msigwa – MAELEZO.

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI