Sunday, November 8, 2015

CUF WAKATAA UCHAGUZI KURUDIWA

Baraza kuu la uongozi la chama cha wananchi (CUF) katika kikao chake cha dharura limetoa tamko na kusema chama hicho hakipo tayari kurudia uchaguzi mwengine na
badala yake umeitaka Tume ya uchaguzi kukamilisha kazi ya kuhesabu kura.

Akisoma tamko hilo mbele ya waandishi wa habari hapo Vuga mjini hapa, Mwenyekiti wa kamati ya muda ya uongozi ya chama cha wananchi (CUF) Twaha Taslima alisema chama
chake kinaamini kwamba zoezi hilo limekwenda vizuri kwa hivyo hakuna sababu ya kufutwa kwa uchaguzi mkuu wa Oktoba 25.

Alisema Tume ya uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) itenguwe uamuzi wake wa Mwenyekiti Jecha Salim Jecha wa kufuta matokeo ya uchaguzi mkuu kwa sababu taasisi hiyo haina mamlaka na uwezo wa kufanya hivyo kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar na sheria ya uchaguzi
nam.11 ya 1984.

'Baraza kuu la uongozi la chama cha (CUF) ambacho ndiyo chombo cha juu cha maamuzi katika kikao chake kimetoa tamko na kusema hakipo tayari kurudia uchaguzi mwengine utakaoitishwa na Tume ya uchaguzi ya Zanzibar ZEC'alisema Taslima.

Alifahamisha kwamba Baraza linaitaka Tume ya Uchaguzi kuendelea na mchakato wa kuhesabu na kufanya majumuisho ya hatua zilizobakia za kuhakiki matokeo ya uchaguzi ya majimbo 14 ya Pemba.

Aidha kimesema uchaguzi wa marudio hautakuwa huru na haki isipokuwa utatawaliwa  na
mizengwe na vitisho vingi kwa wananchi ikiwemo wafuasi wa chama cha CUF.

'Athari za kurudia uchaguzi mkuu mwengine zipo nyingi kwanza uchaguzi huo hautakuwa
huru na haki lakini zaidi utajenga mazingira ya hofu na wasiwasi mkubwa kwa wapiga
kura wakiwemo  wafuasi wa CUF'alisema.

Mapema Waziri wa Katiba na Sheria wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Abubakar
Khamis Bakary ametangaza rasmin kuachia wadhifa wake huo huku akikabidhi dhamana na
majukumu yake Wizarani.

Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari alisema muda wa ukomo wa mawaziri kuwepo afisini kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao umefikia wiki iliyopita Novemba 3 kwa hivyo yeye haoni sababu ya kuendelea kushikilia wadhifa huo.

' Tayari nimekabidhi Afisi kwa watendaji husika ikiwemo vitendea kazi pamoja na gari kwa hivyo kuanzia sasa mimi sio waziri tena wa Katiba na sheria wa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar'alisema.

Katibu mkuu wa chama cha wananchi CUF maalim Seif Sharif Hamad ameanza ziara ya kutoa maelezo kuhusu tamko lililotolewa na baraza kuu la uongozi la chama cha CUF kwa watendaji mbali mbali wa ngazi za chama Zanzibar.

Tume ya uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imefuta matokeo ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 na kusema utarudiwa na kupangwa katika terehe itakayotangazwa baadaye.

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI