Friday, August 8, 2014

MKUTANO WA WANACHAMA COASTAL UNION JUMAPILI

Mwakilishi wa wanachama wa Coastal Union, Salim Al Mazrui akisisitiza jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari jana.
MKUTANO mkuu wa dharura wa wanachama kujadili kuhusu aliyekuwa Mwenyekiti wa Coastal Union, Hemed Aurora kujiuzulu unatarajiwa kufanyika Jumapili wiki hii kwenye ukumbi wa Makao makuu ya Klabu ya Coastal Union barabara ya 11 jijini Tanga.
Mkutano huo unatarajiwa kuanza saa nne asubuhi utakaohusisha wanachama hai ambao wamelipia kadi zao na hawadaiwi madeni yoyote.
Akizungumza na waandishi wa habari,Mwakilishi wa Wanachama wa Coastal Union, Salim Al-Mazrui alisema maandalizi ya kuelekea mkutano huo yamekamilika kwa asilimia kubwa na utakuwa na agenda mbili muhimu zitakazojadiliwa.
Al Mazrui alisema agenda ya kwanza itakuwa ni kujadili uvumi uliojitokeza wa kujadili kujiuzulu kwa aliyekuwa mwenyekiti wa Klabu ya Coastal Union, Hemed Hilal Aurora.
Alisema agenda ya pili itakuwa ni kujadili utendaji wa Makamu Mwenyekiti wa Coastal Union, Steven Mguto ndani ya klabu hiyo hasa kuelekea msimu mpya wa Ligi kuu Tanzania bara na kutoa maamuzi.
Mwakilishi huyo aliwataka wanachama wa Coastal Union waliokuwa hai kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi kwenye mkutano huo wenye lango pia la kuangalia namna ya kuipa hamasa timu hiyo kufanya vizuri katika msimu ujao wa ligi kuu.
Kwa upande wake,Katibu Mkuu wa Coastal Union,Kassim El Siagi alithibitisha kupokea taarifa ya mkutano huo na hivyo utafanyika siku ya Jumapili kutokana na wanachama hao kufuata taratibu zote.

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI