UTUNZAJI wa mazingira ni jukumu la kila mtu kwa pale anapoishi na maeneo yote yanayomzunguka kwa kuhahakisha kuwa maeneo yanabaki katika uasilia wake.
Suala la uharibifu wa mazingira linazidi kuenea kila sehemu na kuathiri misitu,vyanzo vya maji na maeneo mbalimbali ya asili yaliyopo katika makazi.
Uharibifu huu wa mazingira unadaiwa kuwa umechangia kupotea kwa asili katika Kijiji cha Kwedikabu Kata ya Kwamsisi wilayani Handeni mkoani Tanga kwani Mto wa ajabu umeanza kukauka.
Kwa wakazi wa kijiji hiki mto huu ulikuwa muhimu kwani ulikuwa ukitoa maji baridi na pia pamoja na ukame wa eneo hilo, ulifurika mwaka mzima.
“Hili eneo lilikuwa halikauki maji ila leo hii yamekauka, tatizo ni hawa Wamang’ati wanaingiza ng’ombe na kusababisha mizimu kukasirika na kukausha maji yao. Hapa haparuhusiwi kufanya shughuli yoyote zaidi ya kuchota maji tu,”anasema mmoja wa wakazi wa kijiji hicho aliyejitambulisha kwa jina moja Mgaza.
Hamisi Luhezi (55) anaelezea historia ya Mto Mgulwi na kusema kuwa tangu anazaliwa aliukuta na kamwe hakuwahi kuuona ukikauka.
Anasema kila baada ya miaka mitatu wazee walikwenda eneo hilo na kuchinja ng’ombe ambapo nyama yake huliwa hukohuko na hakuna mtu atakayeruhusiwa kwenda nayo nyumbani.
Luhezi anasema ndani ya msitu huo kuna nyoka mkubwa ambaye ndiye anaelinda msitu na vyanzo nya maji ila wanahisi kwasasa atakuwa ametoweka ama kufa kutokana na mazingira ya mto na msitu huo kuharibiwa na shughuli za kibinadamu.
“Hapa mtoni kuna nyoka mkubwa anaeitwa Mzimuwachesa, walikuwa wawili na kazi yao ni kulinda maji lakini hawa Wamang’ati tayari wamemuua mmoja hali ambayo ilileta kutoelewana miongoni mwa wanakijiji, lakini tayari hatua stahiki zimechukuliwa kwa wazee kutafuta ng’ombe na kwenda kumchinjia mtoni kwa minajili ya kutoa sadaka ya kuomba msamaha kwa kosa hilo,”anasema Luhezi.
Akielezea masharti ya mto huo, Luhezi anasema ni lazima kila anaekwenda mtoni apige hodi mara tatu ndio aingie na kwamba hakuna atakaeitikia ila ni lazima kufanya hivyo.
Anasema kuwa kuwa majira ya mchana huwa kuna mwali (Malikia) huwa anakuja kuoga hivyo ni muhimu sana muda huo kupiga hodi endapo utakwenda na hujapiga hodi ukimkuta utaumwa ama kufa hapo hapo kwani haruhusiwi kuonwa na binadamu.
“Hurusiwi kuingia katika mto huo bila ya kupiga hodi mara tatu hasa unapoingia eneo hilo kuanzia saa sita za mchana, utakapopiga hodi hakuna atakaeitikia lakini ndio unaruhusiwa kuingia… na ukiingia bila kupiga hodi unaweza kumkuta mwali (malkia) anaoga au kapumzika akikwambia kwanini umeingia bila ya kupiga hodi basi huwezi kupona utaugua sana au kufa kabisa”
MASHARITI YA KUINGIA MTONI
Unapoingia ndani ya mto Mgulwi muda wa saa 6:00 mchana ni lazima upige hodi kama ilivyoelezwa awali kuwa ndani ya eneo hilo kuna wenyewe (mizimu) ambao ndio wanaotunza eneo hilo hivyo usipopiga hodi unaweza kupoteza maisha au kuugua sana.
Mwisho wa kuingia mtoni hapo ni saa 12:00 jioni baada ya hapo hakuna mwanakijiji anaeruhusiwa kuingia tena hadi kesho yake na ukikaidi yatakayokukuta ni kupoteza maisha msituni humo, ama kusikia au kuona vitu vya ajabu.
MASHARTI YALIYOWEKWA
Kabla ya uvamizi wanakijiji walijiwekea masharti mbalimbali ambayo kutoruhusiwa kuchota maji na sufuria chafu yenye masizi.
Pia kwa bahati mbaya ukimchota samaki unatakiwa kumrudisha mtoni haraka iwezekanavyo la sivyo atatoa harufu mbaya ambayo sio ya kawaida na maji uliochota yote yatageuka kuwa damu.
Hakukuwa na ruhusa ya kukata mti eneo hilo na ikitokea ukikata mti unapotea njia ya kurudi nyumbani hadi utupe mti ulioukata ndio fahamu itakurudia na kuifahamu njia ya kurudi nyumbani.
Mzee Luhezi anasema kwasasa hali ya msitu huo imekuwa mbaya na baadhi ya maajabu yamepungua.
SERIKALI YA KIJIJI YAZUNGUMZA
Akielezea kuhusu tatizo la uharibifu wa mazingira katika eneo hilo Ofisa Tarafa wa Kwamsisi, Baraka Hassan anasema kuwa ni kweli kuna uharibifu wa mazingira katika eneo hilo.
Baraka anasema kuwa kutokana na hiyo tayari ameshawaagiza watendaji wa kata kutenga maeneo maalumu kwaajili ya wakulima na wafugaji.
JE BADO KUNA MAAJABU?
Afisa tarafa huyo anadai kuwa bado kuna maajabu kwani kuna samaki ambao hawaliwi kwa imani kuwa ukimla unakufa.
Pia yupo nyoka mwenye masikio licha ya kuwa huonekana kwa nadra.
Na Rajabu Athumani, Mwananchi
0 comments:
Post a Comment