Saturday, January 9, 2016

FAHAMU NAMNA MTI WA MPERA UNAVYOTIBU MAGONJWA MENGI

Mti wa mpera ni miongoni mwa miti ya matunda ambayo inafahamika vizuri katika jamii ya watu wengi hapa nchini. Mti huu hutoa matunda yanayofahamika kama mapera  na asili ya mti huu ni Amerika ya Kati na Kusini licha ya kuwa kwa siku hizi mti huu unapatikana sehemu mbalimbali hapa duniani.

Mmea huu kama ilivyo kwa mimea mingine ya matunda, unastawi zaidi katika hali ya hewa ya kitropiki. Hapa nchini Tanzania mmea huu unasadikika uliletwa na wakoloni waliotoka mashariki ya mbali waliokuja Afrika kwa madhumuni mbalimbali ikiwemo suala la kueneza dini ya Kiislamu na Kikrosto.


Wataalam wa tiba asili wanauzungumzia mti huu kama tiba nzuri inayoweza kutibu magonjwa mbalimbali yakiwemo yale ambayo ni tishio  kwa kizazi cha sasa kama figo.

Tabibu wa tiba asili hapa nchini Dk Abdallah Mandai kutoka Mandai Herbalist Clinic anasema majani ya mti huo yanasaidia sana kuondoa kichefuchefu, lakini pia yanapopondwa na yakitumiwa vizuri yanazuia ugonjwa wa kiharusi.

“Majani ya mpera yanaponya vidonda vya tumbo na pia yanavirutubisho vingi ambavyo husaidia kuimarisha fizi na kuongeza vitamin B na A mwilini” anaeleza Dk  Mandai.

Aidha, anaendelea kusema kwamba majani ya mpera yenye uzito wa kilo moja yanapopondwa na kisha mgonjwa akanywa lita moja yana saidia sana kukinga seli za mwili dhidi ya magonjwa.

Dawa hiyo pia hutibu ugonjwa wa malaria , aidha anasema mgonjwa atumie tiba hiyo kati ya siku 14 hadi mwezi mmoja kulingana  na ukubwa wa tatizo la mgonjwa husika.
Hali kadhalika anasema kwamba juisi ya mapera husaidia sana kutibu mgolo au bawasila, figo na hata kuondoa mafuta katika moyo.

Anabainisha kuwa,  mizizi ya mpera ikichemshwa inasaidia sana kwa akinamama wenye matatizo ya hedhi au wanaotoa maji yenye harufu mbaya kutoka sehemu zao za siri.
Matunda yanayotokana na mti wa mpera yaani mapera ambayo pia watu wengi wanapenda kula
Sambamba na hayo, Dk Mandai anaeleza kuwa, majani mateke yanapofungwa shingoni kwa mwenye tezi yanauwezo wa kuponyesha tatizo hilo pia na mwenye jipu akifunga sehemu husika hulifanya jipu kuiva haraka mno.

Watoto wadogo wenye matatizo ya kutopata choo zaidi ya siku mbili, Dk Mandai anasema wakinyweshwa maji ya majani hayo baada ya kuchemshwa wanapona kabisa tatizo hilo, lakini pia maua ya mpera yanasaidia katika kutibu tatizo la manjano na hata homa kali.

Mizizi na matunda hali kadhlika husaidia  kuongeza vitamin B na C, ambapo mtumiaji atapaswa kuchemsha majani yenye ujazo wa gramu moja kisha anywe kikombe kimoja mara tatu kwa siku.

Hata hivyo, Dk Mandai anaonya kuwa endapo unasumbuliwa na maradhi hayo ambayo yameelezwa kutibika kwa mti huo wa mpera ni vizuri ukafanya utaratibu wa kuonana naye kwanza kabla ya kuanza tiba hiyo kwa ajili ya maelekezo na ushauri wa kitabibu zaidi. Dk Mandai anpatikana Ukonga, Mongolandege kwenye kituo chake kiitwacho Mandai Herbalist Clinic.

No comments:

Post a Comment