Monday, November 23, 2015

SIMULIZI YA WACHIMBAJI WALIVYOOKOLEWA KUTOKA MGODINI BAADA YA KUKAA SIKU 41 CHINI YA KIFUSI


Mmoja wa watu waliokuwa kuwa wakifanya kazi ya kuwaokoa wachimbaji wa madini walionusurika kufa  baada ya kuporomoka kifusi kwenye machimbo ya Nyangalata Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga na kuishi kwa siku 41, Mohamed Churi amesema ilikuwa kazi ngumu kuwatoa kutokana na mazingira yalivyokuwa hatarishi kwa maisha yao.

“Ilikuwa ni kazi ngumu kuingia kwenye shimo lenye njia nyembamba ambalo likiguswa, udongo unaporomoka na kuwafukia wote,” alisema.

Churi aliyekuwa akiwatoa wachimbaji hao moja baada ya mwingine, alisema kazi hiyo ilihitaji tahadhari kubwa na uangalizi wa hali ya juu.

  Alisema siku ya kwanza aliingia kwenye shimo lililopo  jirani kwa ajili ya uchimbaji na kusikia sauti ya watu wakiomba msaada wa kuokolewa.

Alisema sauti hizo zilimshtua akidhani huenda ilikuwa ni mizimu ya kwenye machimbo kwa kuwa hakuwa na wazo kama wachimbaji hao wangekuwa hai hadi siku hiyo.

 Churi alisema alivutasubira huku akiendelea kuwadadisi na walipoanza kujieleza mmoja baada ya mwingine na kujitambulisha majina yao, alitoka nje kwenda kutoa taarifa kwa uongozi wa mgodi huo. Alisema uongozi huo ulishindwa kuamini kama kulikuwa na wachimbaji waliofukiwa na kifusi kama walikuwa bado wako hai.

 Baada ya kuthibitika taarifa hizo, Churi alisema aliongoza msafara kuingia kwenye shimo ambalo chini yake kuna shimo ambamo wachimbaji hao walikuwa hai.

Alisema kabla ya kuingia ilimlazimu apate kilevi ili aondoke katika hali ya kawaida na woga.

 Churi alisema baada ya kufika kwenye chumba cha kwanza, kazi ilikuwa ni kuangalia namna ya kutoboa ili kuwafikia walipokuwa wachimbaji hao kwa kuwa walikuwa chini ya shimo na wao juu. “Tulifanikiwa kutoboa tundu dogo tukawaona, walikuwa umbali wa mita kama 20 kutoka chumba tulichokuwa, wenzangu wakabaki hapo kwenye kituo.

“Baada ya hapo, wakanifunga kamba, nikashuka nayo na kutokana na ufinyu wa njia kwenye shimo, nilichubuka mikono na taratibu niliwafikia,” alisema Churi. Alisema hali aliyowakuta hawezi kusimulia yote, (alinyamaza kisha kuanza kulia).

Baada ya kunyamaza, aliendelea kusimulia kuwa walikuwa sehemu nyembamba kwenye giza nene na harufu mbaya ya mwenzao, Mussa  Supana aliyekuwa amekufa pembeni na mwili wake kuanza kuharibika huku kiwiliwili kuanzia kiunoni hadi miguuni kikikiwa kimefunikwa na kifusi huku kikiwa kimebaki kichwa na kifua.

“Nilianza kuwabeba mmoja mmoja na kupanda nao kwenye kamba hadi kituo walichokuwa wenzangu ambao nao walinisaidia kuwatoa nje,”  alisema Churi.

Alisema wachimbaji hao walikuwa wamekonda mithili ya  watoto wadogo hali iliyomrahishia kazi ya  kuwabeba kutoka kwenye shimo walimokuwa kutokana na kupungua uzito. Alidai kila mmoja alipungua na kubaki uzito wa kilo zisizofikia 20.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mji wa Kahama, Dk Joseph Ngowi alisema wachimbaji hao,  Chacha Wambura, Joseph Bulule, Amosi Mhangwa na Msafiri Gerald,  hali zao zinaendelea vizuri isipokuwa Onyiwa Moris amegundulika kuwa na tatizo la kifua.

  Wachimbaji hao walifunikwa na kifusi Oktoba 5, mwaka huu katika machimbo hayo na kuokolewa Novemba 15  baada ya kuishi humo kwa siku 41,wakinywa maji magome ya miti, wadudu wakiwamo mende na chura.

No comments:

Post a Comment