MOTO mkubwa umeteketeza maduka 18 katika mtaa wa Kwakivesa wilaya ya Handeni mkoani Tanga baada ya lori lililokuwa limebeba mafuta kugonga nguzo ya umeme kupinduka na kisha kuanza kuwaka moto uliosambaa hadi kwenye maduka hayo.
Taharuki hiyo imetokea leo majira ya saa 5:00 asubuhi baada ya lori hilo lililokuwa kwenye mwendo kasi kutaka kumkwepa mwendesha bodaboda na kujikuta likiacha njia na kugonga nguzo ya umeme na kusababisha hasara kubwa kwa wananchi huo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Frasser Kashai amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kudai kuwa moto huo ulitokea saa 5.asubuhi katika mtaa huo kufuatia roli la mafuta aina ya Fuso kugonga nguzo ya umeme na kusababisha betri kutoa cheche zilizosababisha moto kuanza kuwaka.
Kamanda Kashai amesema roli hilo lilikuwa likiendeshwa na dereva Ali Makelele ambaye bado hajapatikana huku utingo wake aliyemtaja kwa jina moja la Mfundo akiwa amekimbizwa hospitali ya Wilaya ya Handeni kwa matibabu Zaidi baada ya kuungua vibaya.
“Moto ulianza kuliteketeza roli hilo la mafuta na baadaye ukasambaa kwenye maduka jirani ,hali ilikuwa mbaya sana, hadi sasa hatujajua hasara iliyopatikana, tutakapokuwa na taarifa kamili tutawataarifu“, amesema kamanda Kashai.
Aidha mashuhuda wa tukio hilo wanaeleza kuwa moto huo ulishika kasi kwa haraka kutokana na hali ya hewa kuwa ya upepo mkali licha ya juhudi za wananchi kuuzima lakini uliwashinda nguvu.
Aidha jeshi la polisi limelaani mtindo unaoota mizizi hivi sasa wa wananchi kujichukulia sheria mkononi kwani baada ya tukio la moto kutokea kikosi cha zimamoto kutokea Korogwe kilifika katika eneo la tukio lakini badala ya kuachwa kufanya kazi yake kikashambuliwa.
Shambulio hilo la wananchi kwa zimamoto limesababisha hasara ikiwa ni pamoja na kuvunjwa vioo vya gari, kupotea kwa vitendea kazi pamoja na baadhi ya askari wa zimamoto kujeruhiwa.
No comments:
Post a Comment