Wednesday, October 1, 2014

WANAFUNZI ELFU NANE WAACHA SHULE BAADA YA KUPATA MIMBA

 
LICHA ya jitihada zinazofanyika kutoa elimu ya uzazi salama kwa wanafunzi bado idadi ya wanafunzi wanaopata ujauzito wakiwa shuleni imeendelea kuongezeka takwimu za mwaka 2010 zikionyesha kuwa watoto wa kike elfu nane wanafunzi wa shule za msingi na sekondari nchini walikatiza masomo baada ya kupata ujauzito usiotarajiwa.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya uzazi salama duniani ambayo shirika la Marie Stopes nchini iliadhimisha kwa kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ya vijana, mkuu wa kitengo cha mawasiliano wa shirika hilo Bwana Johnbosco Basso anasema kuongezeka kwa idadi hiyo pia kunachangia kuongezeka kwa vifo kutokana na walio wengi kujaribu kuharibu mimba.
 
Hata hivyo baadhi ya kinamama wakazi wa Arusha wakizungumzia changamoto hiyo wanasema pamoja na kuendelea kutoa elimu mashuleni ipo haja pia wazazi kuchukua jukumu la malezi na ikiwezekana kurejesha utamaduni ulikua ukitumika awali wa kuwa na kipindi maalum cha watoto wa kike kupatiwa mafunzo ya namna ya kujilinda.
 
Matukio mengi ya wanafunzi kupata ujauzito yamekuwa yakihusishwa  na mazingira yasiyo rafiki ya shule wanazosoma ukiwemo umbali wa shule na wengine kulazimika kuishi kwenye nyumba za kupanga kilio ambacho kila mara kimeelekezwa kwa serikali kuharakisha mpango wa ujenzi wa hosteli hususani katika shule za kata .

No comments:

Post a Comment