Na Mwandishi Wetu, Dar
MSHAMBULIAJI na mpachika mabao wa Yanga na Nahodha wa timu ya Taifa ya
Burundi, Didier Kavumbangu, leo mchana amesaini Mkataba wa miaka miwili na
mabingwa wapya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Azam FC.
Kavumbangu aliyemaliza Mkataba wake wa miaka miwili Yanga SC, ameamua
kusaini Azam FC baada ya kuona Klabu yake haina mawasiliano naye licha ya
kumaliza Mkataba wake.
“Mimi ni mchezaji, kazi yangu ni mpira. Nimemaliza mkataba Yanga, lakini
viongozi hawaniambii kitu, nimepata ofa nzuri Azam nikaamua kusaini,” amesema
Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi, Kavumbangu, baada ya kusaini
Mkataba huo ambao unamfanya alipwe vizuri kuliko alivyokuwa analipwa Jangwani.
Pamoja na hayo, Kavumbangu ameishukuru Yanga SC na mashabiki kwa miaka
miwili aliyoichezea timu hiyo na anasema itabakia kwenye kumbukumbu zake kwa
kushinda nayo mataji kadhaa.
Mshambuliaji huyo mrefu mwenye nguvu amesema sasa akili yake anaipeleka
kwa mwajiri wake mpya, Azam FC ambako pia amepania kwenda kushinda mataji na
kuiwezesha timu hiyo ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake
kufanya vizuri kwenye michuano ya Afrika.
“Mimi sasa ni mchezaji wa Azam, nafurahi kujiunga na klabu hii kubwa.
Kawaida yangu huwa nashabikia klabu nayochezea, sasa mimi ni mshabiki namba
moja wa Azam,”amesema.
Kavumbangu alitua Yanga mwaka 2012 akitokea Atletico ya Burundi na
katika mechi misimu miwili ya kuichezea klabu hiyo, amefunga mabao 31 katika
mechi 63 za mashindano yote, moja tu la penalti.
No comments:
Post a Comment