TFF yataka wachezaji Congo wapimwe upya
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
limewasilisha barua ya malalamiko yake dhidi ya matumizi ya wachezaji wenye
umri
mkubwa na unyanyasaji uliofanyuwa kwa maofisa wa
timu ya taifa ya vijana walio na umri chini ya miaka 17 wa Serengeti Boys
wakati
wa mechi ya marudiano ya michuano ya Mataifa ya
Afrika kwa Vijana dhidi ya Congo.
Serengteti Boys iliondolewa kwenye mashindano hayo
kwa jumla ya mabao 2-1 baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mechi ya
kwanza iliyofanyika Novemba 18, 2012 kwenye Uwanja
wa Taifa jijini Dar Es salaam na baadaye kukubali kipigo cha mabao 2-0 kwenye
mechi ya marudiano jijini Brazaville Jumapili
iliyopita.
Hata hivyo, mechi hizo mbili zilizingirwa na
matukio tata, hasa kuhusu umri wa wachezaji wa Congo ambao kimaumbile
walionekana
kuwa ni umri mkubwa zaidi na kusababisha TFF
kuwasiliana na Shirikisho la Mpira wa Miguu la Afrika (CAF) kuhusu njia
zinazowezekana
kupata uthibitisho wa umri wa wachezaji hao, lakini
ilishindikana na ndipo TFF ilipocheza mechi hiyo ikiwa na imeweka pingamnizi.
Katika barua iliyotumwa CAF jana, TFF imerejea
barua ya pingamizi aliyokabidhiwa kamisaa wa mechi ya kwanza jijini Dar Es
salaam,
Bw. Chayu Kabalamula na malalamiko yaliyowasilishwa
kwa kamisaa wa mechi ya marudiano kuhusu vurugu walizofanyiwa maofisa wa
timu.
Katika barua hiyo, TFF imeomba CAF iagize kuwa
wachezaji wote wa Congo waliocheza mechi hizo mbili wapimwe tena kwa kutumia
kipimo cha M.R.I na gharama za zoezi hilo zilipiwe
na TFF; na pili Shirikisho limeomba kuwa CAF ikubali kuipa Tanzania wiki tatu
za
kukusanya ushahidi na kuuwasilisha Cairo kwa ajili
ya maamuzi.
Kwa mujibu wa kanuni za mashindano hayo, nchi
shiriki zinatakiwa kuwapima wachezaji wake kwa kutumia kipimo cha M.R.I ambacho
kinaweza kutambua umri wa vijana walio chini ya
miaka 17 na kwamba matokeo yake yanatumwa CAF, ambayo itahifadhi matokeo hayo
hadi hapo kutakapotokea pingamizi na ndipo itafanyia
kazi kwsa kutoa matokeo ya vipimo hivyo.
“Ni matumaini yetu kuwa suala letu litafanyiwa kazi
na kutolwewa ufumbuzi ili kulinda soka la vijana barani Afrika dhidi ya vitendo
vilivyokomaa vya udanganyifu wa umri,” alisema
katibu mkuu wa TFF, Angetile Osiah.
Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari
jana, kocha Jacob Michelsen alisema alishangaa kuona wachezaji wenye umri
mkubwa zaidi wakichezeshwa kwenye mechi ya
marudiano, lakini akaisifu TFF kuwa inafuata njia sahihi ya maendeleo na haina
budi
kuendelea na programu yake ya soka la vijana.
"Najivunia vijana wangu kwa kuwa walijituma
kwa muda wote pamoja na kwamba wenyeji waliongeza wachezaji wenye umri mkubwa
zaidi kuliko waliokuja huku," alisema kocha
huyo kutoka Denmark.
"Kitu cha msingi ni kufuata njia sahihi ya
kuendeleza soka na natumaini TFF iko kwenye njia sahihi na itaendelea na
programu yake ya
vijana. Hakuna njia ya mkato kama mnataka
maendeleo. Ni lazima tufuate njia sahihi na matunda yake tutayaona baadaye.
"Kila mara nasema mambo (ya vijana) huchukua
muda mrefu (Things Take Time) na hivyo hatuna budi kuwa wavumilivu.
"Wenzetu walitumia njia za ajabu na hata hiyo
penati ya bao la kwanza haikuwa faulo. Ilitokea nje kabisa ya eneo la penati.
Refa
alimuangalia kibendera akaona ametulia,
akamuangalia beki mchezaji akamuona amesimama, mara akaangalia juu na kupuliza
filimbi
kuonyesha kuwa ni penati."
Naye kocha msaidizi, Jamhuri Kihwelo alishindwa
kujizuia na kujikuta akibubujika machozi wakati alipoelezea jinsi
alivyoshambuliwa na
askari kabla ya mchezo huo.
Kozi ya Leseni C kufanyika Arusha
Kituo cha Kukuza Vipaji cha Rolling Stone kwa
kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kimeandaa kozi ya
leseni C ya
walimu wa mpira wa miguu itakayofanyika kuanzia
Desemba 10, 2012 hadi Desemba 23, 2012 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid
mjini Arusha.
Kozi hiyo itahusisha makocha walio na Cheti cha
Kumaliza Elimu ya Sekondari au wale waliohitimu kozi ya ualimu wa mpira wa
miguu ya
ngazi ya kati (intermediate).
Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Sunday Kayuni alisema
kuwa washiriki wa kozi hiyo wanatakiwa kuwa wamewasili Arusha ifikapo
Desemba 9, 2012 na wanatakiwa kwenda na vyeti vyao
halisi vya elimu. Alisema tayari Rolling Stone wameshasajili walimu 25 ambao
watashiriki kozi hiyo na hivyo kuwataka watu
wengine wanye sifa kutoka mkoa wa Arusha na mikoa mingine kujitokeza kushiriki
mafunzo hayo muhimu.
Kayuni alisema kuwa kadri taifa litakavyozalisha
walimu wengi, ndivyo taifa litakavyokuwa na uwezo wa kuandaa watoto na vijana
wengi katika misingi sahihi ya mpira wa miguu na
hivyo kuwa na matumaini makubwa ya kufanya vizuri.
Kozi hiyo itaendeshwa na Mkurugenzi wa Ufundi wa
TFF, Kayuni kwa kushirikiana na mkufunzi kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu la
Afrika (CAF), Bw. Dominic Niyonzima kutoka Rwanda.
Kwa mujibu wa Rolling Stone, kila mshiriki
atajigharimia nauli ya kwenda Arusha na atatakiwa kwenda na ada ya fedha
zinazolingana na
Dola 100 za Kimarekani (dola moja ni sawa na
Sh1,580 za Tanzania).
Sita wapitishwa kuwania uongozi TAFCA
Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Waliku wa Mpira wa
Miguu (TAFCA) imetangaza matokeo ya usaili wa wagombea uongozi chama hicho,
ikiwa imepitisha wagombea sita sita na kuwaengua
wagombea watano kwenye nafasi tofauti.
Baada ya usaili wa wagombea hao, Kamati ya Uchaguzi
ya TAFCA iliwaengua wagombea hao watano kwa kutokidhimasharti ya Ibara ya
26 (2) ya Katiba ya TAFCA na Kanuni ya 9 ya Kanuni
za Uchaguzi za Wanachama wa TFF na pia kutokidhi utashi wa masharti ya 11 (1)
ya
kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.
Katika nafasi ya mwenyekiti Oscar Don Korosso
alipitishwa kuwa mgombea pekee baada ya Kenedy Mwaisabula na Jamhuri Kihwelo
kuenguliwa kwa kutokidhi masharti ya ibara ya 26
(2) ya Katiba ya TAFCA na kanuni ya tisa ya Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa
TFF.
Katika nafasi ya makamu mwenhyekiti, Kamati
imempitisha Lister J. Manyara kuwa mgombea pekee wa nafasi hiyo huku Marco Bundara
akipitishwa kuwa mgombea pekee wa nafasi ya katibu
mkuu wa TAFCA.
Hali kadhalika wagombea wawili wa nafasi ya mjumbe
wa mkutano mkuu wa TFF, Wilfred Kidau na Magoma Rugora wamekidhi masharti
ya Katiba ya TAFCA na Kanuni za Uchaguzi za
Wanachama wa TFF na hivyo watachuana kuwania kura za wajumbe wa mkutano mkuu,
huku Ally A Mtumwa akienguliwa kwa kutokidhi
masharti ya kanuni ya 11 (1) ya Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.
Katika nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji,
wagombea wote wawili, Abubakar Balingula na Aboubakar Salum wameenguliwa kwa
kutokidhi masharti ya Ibara ya 26 (2) ya Katiba ya
TAFCA na Kanuni ya 9 ya Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF)
No comments:
Post a Comment