Mjumbe
wa Bunge Maalum la Katiba ambaye pia ni mwanachama wa CHADEMA, Leticia
Nyerere (kushoto) akitoka kujaza fomu ya mahudhurio ya vikao vya Bunge
hilo huku akisindikizwa na mjumbe mwenzake, Steven Ngonyani
**************
**************
KUMEKUCHA katika Bunge Maalumu la Katiba, ambapo sasa baadhi ya wajumbe wa
Bunge hilo wa kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wamekiuka viapo na
vitisho vya viongozi wao, kwa kuamua kutinga bungeni.
Katika
mijadala mbalimbali, msemaji wa Ukawa ambaye pia ni Mwanasheria wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, amekuwa akisisitiza kwamba
wajumbe wa Ukawa na hasa kutoka Chadema, hawatahudhuria Bunge Maalumu la
Katiba.
Aidha, wiki
iliyopita Chama cha Wananchi (CUF) kilisambaza waraka kwa vyombo vya habari,
kuwataka wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanaotoka katika chama hicho,
kutohudhuria vikao vya Bunge hilo, vilivyoanza juzi.
Hata hivyo,
katika kile kilichoonesha kutoungwa mkono kwa viongozi wa Ukawa ndani ya vyama
vyao, baadhi ya wabunge waliozuiwa kushiriki vikao hivyo, wameonekana bungeni
wakijisajili, kuashiria ushiriki wao bila kujali viapo na makatazo ya viongozi
wao.
Leticia,
Shibuda
Jana saa
5:55 asubuhi mjumbe wa bunge hilo, Leticia Nyerere ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu
kutoka Chadema, aliwasili kwenye viwanja vya bunge na kwenda moja kwa moja
kwenye eneo la kujisajili na kukamilisha taratibu zinazotakiwa.
Hata hivyo,
Leticia hakuwa tayari kuzungumza na waandishi wa habari, wakati akienda
kujiandikisha.
Hata wakati
anatoka kukamilisha taratibu zinazotakiwa za kujisajili, pia alikataa kupigwa
picha. “Unajua kwamba kunipiga picha bila idhini yangu ni ‘illegal (kinyume na
sheria)? Sitaki,” alisema huku akielekea mlango wa kutokea, ambako alikutana na
mjumbe mwingine wa bunge hilo, ambaye pia ni Mbunge wa Korogwe Vijijini, Steven
Ngonyani (CCM), aliyekuwa akitoka pia kujisajili.
Ngonyani
alisalimiana na Leticia na wakawa wanaongozana kutoka eneo la Bunge. Ngonyani
alionekana mwenye furaha baada ya mjumbe mwenzake, kukamilisha taratibu za
usajili.
Mapema juzi,
wajumbe wengine wa Bunge hilo, Mbunge wa Maswa Mashariki, John Shibuda
(Chadema) na Clara Mwatuka ambaye ni Mjumbe wa Viti Maalum kutoka CUF, nao
walijisajili kushiriki vikao hivyo.
Wanaojishauri
Jana asubuhi
pia zilikuwepo taarifa bungeni kwamba Mbunge wa Mpanda Kati, Said Arfi
(Chadema), naye alijisajili. Lakini, akizungumza na mwandishi kwa simu, alisema
alifika Dodoma, lakini hajaamua kama ajisajili ili ashiriki vikao au la.
“Sijajisajili
bado, sio kweli, sijaamua nichukue huo uamuzi wa kushiriki au la, kama nikitaka
kujisajili nitasema, ila kweli nipo Dodoma,” alisema Arfi ambaye alijiuzulu
nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema hivi karibuni.
Zitto
Mbunge wa
Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema), hivi karibuni aliibuka na kupingana na
harakati za Ukawa.
Zitto
alikaririwa akisema, hana uhakika wala hauamini Ukawa kama utakuwa umoja
endelevu hadi kufikia Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, kwa sababu si mara ya kwanza
vyama vya upinzani, kuungana na kugawanyika.
Zitto alitoa
kauli hiyo wakati akihojiwa kwenye kipindi cha Power Breakfast, kinachorushwa
na Kituo cha Redio cha Clouds cha jijini Dar es Salaam, ambapo alisema
Watanzania wanakabiliwa na changamoto nyingi na si Katiba pekee.
Alisema siku
zote Watanzania, wamekuwa wakipenda kuwa na upinzani imara, ambao watu wanaweka
tofauti zao pembeni na kuungana dhidi ya chama ambacho kinaongoza, lakini haoni
kama Ukawa utaendelea hadi kufikia kipindi cha Uchaguzi Mkuu.
Alisema
hatua ya kusimama kwenye ajenda moja ya Katiba, haitausaidia umoja huo, kwani
kipindi cha Uchaguzi Mkuu, kinakuwa na ajenda nyingi.
Alisema
wananchi watapenda kusikia masuala ya kushughulikia rushwa, matumizi ya
rasilimali, maji, umeme, afya na barabara.
“Mambo haya
ndiyo yatakayowafanya wananchi waamue namna gani watakabidhi dhamana ya
uongozi, si suala la Katiba pekee,” alisema Zitto.
Samuel
Sitta Juzi wakati akizungumza bungeni, Mwenyekiti wa
Bunge, Samuel Sitta alisema zaidi ya robo tatu ya wajumbe wa bunge hilo,
walikuwa wamejiandikisha, ingawa hakutaja namba kamili. Pia, majina ya
waliojiandikisha, hayatolewi kwa vyombo vya habari.
Kwa mujibu
wa Sitta, wajumbe wakishajisajli, fedha zao zinawekwa kwenye akaunti zao moja
kwa moja kwa wale wenye akaunti ya Benki ya NMB. Wale ambao hawana akaunti NMB,
wanachukua mkononi.
Aidha,
katika mitandao mbalimbali, kulikuwa na taarifa kuwa karibu wajumbe 50
kutoka Ukawa, walikuwa wameshafika Dodoma, ingawa hawakuonekana katika viwanja
vya Bunge.
Taarifa
zingine zilieleza kuwa katika vyama hivyo, baadhi ya wabunge wanalalamikia
viongozi wao, kususia Bunge Maalumu kutokana na ajenda zao binafsi, huku wao
wakitakiwa na wapiga kura wao kuhudhuria bunge hilo.
Wajumbe
waliojiundia kundi la Ukawa ambao wanatoka vyama vya NCCR Mageuzi, Chadema na
CUF walisusia vikao vya bunge hilo Aprili mwaka huu, kwa kile walichodai
halijadili Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya
Jaji Joseph Warioba.
Bulembo Wakati huohuo, Mjumbe wa Bunge hilo, Alhaji Abdallah Bulembo, alisema
anaamini Katiba itapatikana na Ukawa watazidi kupasuka kadri muda unavyoenda.
“Tayari
wameanza kujiandikisha, nasema watagawanyika siku si nyingi na Katiba
itapatikana, hotuba ya Mwenyekiti (Sitta) juzi ilikuwa nzuri sana na imetoa
mwelekeo wa mzuri,” alisema Bulembo, ambaye anatoka Kundi la Wajumbe 201,
walioteuliwa na Rais Jakaya Kikwete.
“Leo (jana)
tumeanza kujadili rasimu kwenye kamati, tunajadili bila jazba, tunaenda vizuri
na naamini mambo yatakamilika kama tunvyopanga." Mwandishi alimtafuta
Msemaji wa CUF, lakini mara zote simu yake haikupatikana.
Baadaye,
mwandishi alimpigia simu Jusa Ismail na kumuuliza juu ya tukio la Mbunge wa
CUF, Clara Mwatuka kujisajili katika Bunge Maalum la Katiba, linaloendelea na
vikao vyake huko Dodoma.
Jusa
alijibu, “Siwezi kukisemea Chama. Mimi ni Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa chama,
naomba umtafute Naibu Katibu Mkuu wa chama, Magdalena Sakaya, atakupa
ufafanuzi”.
Ndipo,
mwandishi alimpigia simu Sakaya, ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum wa CUF.
Lakini, mara zote simu yake ilikuwa haipatikani.
Kwa upande
wa Chadema, mwandishi alimpigia simu Mkurugenzi wa Uenezi wa Chadema, John
Mnyika ili atoe ufafanuzi wa juu wa wabunge wao wawili, Leticia Nyerere na John
Shibuda, kujisajili kwenye Bunge Maalum la Katiba mjini Dodoma.
Hata hivyo,
simu zote mbili za Mnyika, hazikupatikana.
Chanzo: Eddy blog
No comments:
Post a Comment