MIONGONI mwa mapambo yanayotumika zaidi na
wanawake huku umaarufu wake ukiongezeka siku hadi siku ni urembo aina ya
vikuku, ambavyo huvaliwa miguuni.
Awali urembo huu ulionekana zaidi
katika baadhi ya makabila ya kiafrika ukivaliwa na watu wa rika zote; kuanzia
watoto wachanga, wasichana, wanawake wa makamo, hata wazee.
Kwa baadhi ya makabila
hayo, vikuku vimekuwa vikivaliwa kama mila kwamba kila mwanamke anapozaliwa
lazima avae urembo huo kwa kufuata desturi na tamaduni zao, tofauti na ilivyo
sasa ambapo wengi huvaa kama urembo wa kawaida.
Vikuku hivyo
vyaweza kuwa vya shanga, ngozi au hata madini kama dhahabu, fedha na shaba.
Kikuu kinaweza kuvaliwa mguu mmoja au miguu yote.
Wanajaamii wengi
wamekuwa na mtazamo tofauti kuhusu uvaaji wa vikuku wakihusisha na mambo
yasiyofaa na kuonyesha kuwa wengi wanaovaa urembo huo wamepotoka, au kwenda
kinyume na maadili ya kitanzania.
Hata hivyo, wapo
baadhi ya watu ambao ni wadau wa urembo wanafafanua kuwa pambo hilo halina
maana yoyote livaliwapo kwenye miguu ya mwanamke zaidi ya urembo kama ilivyo
kwa hereni na mikufu.
''Watu wanashindwa kuelewa kuwa kikuku ni urembo wa mwanamke kama
ulivyo urembo mwingine, mfano bangili, hereni, cheni ya shingoni, pete ,vidani
na mapambo mengine ambayo hupenda kujiweka mwilini, unajua mwanamke kujipamba'' anasema Nice
Siema
Anafafanua kuwa
uvaaji wa urembo huo hauwezi kutafsiri tabia ya mtu kwa kuwa ni pambo kama
yalivyo mapambo mengine yanayotumiwa na wanawake.
''Unajua siku zote wanawake wanapenda kupendeza ndiyo maana huwa na
furaha kama sehemu kubwa ya miili yao wataiweka urembo tunaona hata vidole vya
miguu vinavalishwa pete hiyo yote ni urembo tu hakuna maana yoyote mbaya'' anasema Siema
Kwa mujibu wa wadau wa urembo kikuku kinapaswa
kilegee kidogo katika mguu na kwamba hakipendezi kikiwa kimebana, kwani licha
ya kusababisha matatizo katika kuruhusu damu kutembea, hakiwezi kuwa na
mwonekano mzuri kikiwa katika hali hiyo.
Bila shaka katika mitindo inayoonekana kupokelewa
vizuri na wanawake hasa wasichana ni pamoja na uvaaji wa vikuku ambao sasa
umetikisa katika kila nyanja.
Na Malunde Blog
No comments:
Post a Comment