Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
BAADA ya kauli ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kusema atamwajibisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda iwapo hatasimamia ipasavyo kukomesha matumizi ya dawa za kulevya, aina ya shisha, Makonda afunguka.
Akiongea Ijumaa hii katika kipindi cha Power BreakFast kinachorushwa na Clouds FM, Mkuu huyo amesema anajua kuwa kazi za serikali ni zakupita huku akidai yeye anamtegemea Mungu katika kazi zake.
“Mimi bahati mbaya ninajua kuwa hizi kazi ni zakupita watu wengine unakuta wanasema huyu jamaa atanyooshwa tu, atatumbuliwa, tutaona mimi sikomolewi kwasababu mimi najua nipo kwa kusudi la Mungu. Wakati wa Mungu ukipita mambo mengine yatajitokeza, lakini ninachokijua ni kitu kimoja asilimia 80 ya watu hawafanyi kazi ipasavyo katika ofisi zao,”
Aidha Makonda alisema ripoti nyingi anazoletewa zinaonyesha mtaani hali ni shwari lakini akienda kuzungumza na wananchi unakuta mambo tofauti na yale yalioandikwa kwenye ripoti.
Pia mkuu huyo amezindua kampeni iitwayo ‘Dar es salaam Mpya’ ambayo itamfanya kuzunguka katika sehemu mbalimbali za jiji hilo kusikiliza kero za wananchi pamoja na kuzipatia majibu.
No comments:
Post a Comment