Wednesday, July 13, 2016

RAIS DKT. MAGUFULI AZINDUA MPANGO WA UGAWAJI WA MADAWAJI KWA MAJIMBO MBALIMBALI NCHINI *PICHAZ*


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimkabidhi Mbunge wa Jimbo la Ilala Mh. Idd Azzan Madawati yaliyotolewa na Ofisi ya bunge kwa ajili kwa niaba ya wabunge waliopata mgao huo katika awamu ya kwanza.Wanaoshuhudia kutoka kushoto ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Kassim Majaliwa wakati wa hafla ya utoaji madawati kwa waheshimiwa wabunge kwa ajili ya shule zilizo kwenye majimbo yao, katika viwanja vya Karemjee Jijini Dar es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akikagua madawati katika mfano wa Darasa wakati wa hafla ya utoaji madawati kwa waheshimiwa wabunge kwa ajili ya shule zilizo kwenye majimbo yao, katika viwanja vya Karemjee Jijini Dar es Salaam. Anayemfuata ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Kassim Majaliwa na kulia ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akifurahia jambo na baadhi ya watoto wa shule ya msingi bunge wakati wa hafla ya utoaji madawati kwa waheshimiwa wabunge kwa ajili ya shule zilizo kwenye majimbo yao, Leokatika viwanja vya Karemjee Jijini Dar es Salaam.
 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya waheshimiwa wabunge waliohudhuria hafla ya utoaji madawati kwa waheshimiwa wabunge kwa ajili ya shule zilizo kwenye majimbo yao katika viwanja vya Karemjee Jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi kutoka shule ya msingi bunge iliyopo Jijini Dar es Salaam, wakati wa hafla ya utoaji madawati kwa waheshimiwa wabunge kwa ajili ya shule zilizo kwenye majimbo yao katika viwanja vya Karemjee Jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Kassim Majaliwa, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Temeke Abdallah Diwani, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni Boniface Jacob, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala Charles Kuyeko, Meya wa Jiji la Dar es Salaam Mstahiki Meya Isaya Mwita na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson, wakati wa hafla ya utoaji madawati kwa waheshimiwa wabunge kwa ajili ya shule zilizo kwenye majimbo yao katika viwanja vya Karemjee Jijini Dar es Salaam.PICHA NA HASSAN SILAYO-MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amezindua mpango wa ugawaji wa madawati yanayotengenezwa kutokana na fedha zilizotolewa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kubana matumizi katika bajeti yake.

Uzinduzi huo umefanyika leo tarehe 13 Julai, 2016 katika viwanja vya Karimjee Jijini Dar es salaam ambapo Rais Magufuli amekabidhi madawati 537 kwa mbunge wa jimbo la Ilala Mheshimiwa Mussa Azan Zungu kwa niaba ya wabunge wa majimbo yote ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar ambayo yatagawiwa idadi hiyohiyo ya madawati kwa kila jimbo.

Madawati hayo 537 ni sehemu ya madawati 61,385 ambayo yametengenezwa katika awamu ya kwanza na yatafuatiwa na madawati mengine 60,000 yatakayogawiwa katika awamu ya pili na yote kwa ujumla yatagharimu shilingi bilioni 4 ambazo zilitolewa na Bunge tarehe 11 Aprili, 2016 baada ya kubana matumizi katika bajeti yake, ikiwa ni kuitikia wito wa Mhe. Rais John Pombe Magufuli.

Mikoa itakayonufaika katika awamu ya kwanza ya ugawaji wa madawati hayo ni Dar es salaam, Pwani, Morogoro, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe, Rukwa, Katavi, Unguja, Pemba na Tanga.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Magufuli amewashukuru na kuwapongeza wabunge kwa kutoa mchango huo na pia amewapongeza wadau wengine ambao wameitikia wito wake wa kuchangia madawati kwa lengo la kuondoa tatizo la wanafunzi kukaa chini.

Rais Magufuli amesema baada ya kuanza kutekeleza ahadi ya kuondoa ada kwa shule za msingi na sekondari, idadi ya wanafunzi waliojiandikisha kuanza darasa la kwanza imeongezeka kutoka wanafunzi 1,282,100 hadi kufikia wanafunzi 1,896,584 sawa na ongezeko la asilimia 84.5 hali iliyosababisha upungufu wa madawati 1,400,000 lakini tatizo hilo limetatuliwa kwa kiasi kikubwa ambapo mpaka sasa zaidi ya madawati 1,000,000 yametengenezwa.

Aidha, Dkt. Magufuli amelitaka Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Jeshi la Magereza kuongeza kasi katika utengenezaji wa madawati ili yakamilike haraka na kuanza kutumika.

Hafla hiyo imehudhuriwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson, Wabunge wa kamati ndogo ya tume ya huduma za bunge, Viongozi wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Magereza pamoja na wanafunzi wa shule ya msingi Bunge.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
13 Julai, 2016

No comments:

Post a Comment