Saturday, November 7, 2015

WASANII WATAKIWA KUCHAGAMKIA MAAZIMISHO YA SIKU YAO

WASANII nchini wametakiwa kuwa mstari wa mbele kuhamasika na kushiriki kikamilifu kwenye maazimisho ya Siku ya Msanii maarufu kama Msanii Day ambayo yanatazamiwa kufanyika mwezi Desemba mwaka huu wa 2015 jijini Dar es Salaam na maeneo mbalimbali nchini.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye programu maalum ya kujadili ushiriki wa wasanii kwenye siku hii muhimu kwao marais wa mashirikisho ya wasanii nchini walisema kwamba wakati umefika kwa wasanii wote nchini kuamka na kuwa mstari wa mbele kutambua maazimisho haya ya siku yao kwani kwa muda mrefu wamekuwa wakitumiwa katika kuazimisha vilele vya tasnia zingine.
“Tumekuwa tukitumika sana sisi Wasanii kung’alisha na kuzifanya kazi za wengine kuwa na mafanikio, tumekuwa tukihamasisha kazi za wengine. Hii siku ya Msanii ni yetu, tuamke, tuibebe zaidi ya tunavyofanya kwenye kazi za wengine. Tuungane tuifanye siku hii yenye tija” alisisitiza Symon Mwakifamba ambaye ni Rais wa shirikisho la Sanaa za Filamu nchini.
Aliongeza kusema kwamba, Wasanii wana nguvu na mchango mkubwa katika jamii na kwamba kwa idadi yao wanatosha kabisa kuwa na uwakilishi katika maeneo mbalimbali ya maamuzi ili kuhakikisha hawaachwi nyuma.
“Naomba wasanii wote tuitumie siku ya Msanii kuonesha nguvu yetu, tuwaoneshe na tutume ujumbe kwa viongozi kwamba kundi hili ni kubwa na muhimu katika kujenga Taifa lenye ustawi” Aliongeza Mwakifamba.
Kwa upande wake Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi Adrian Nyangamale alisema kwamba siku ya msanii ni mahsusi kwa ajili ya wasanii wote nchini na kwamba kama ilivyo kwa maadhimisho ya siku zingine kama za walemavu, wanawake, wanasheria na nyinginezo wasanii nao hawana budi kuhakikisha wanaifanya siku hii kuwa yenye kufana na mafanikio makubwa.
“Hauwezi kuizungumzia siku ya Msanii bila kuwataja na kuwahusisha wasanii moja kwa moja. Wasanii lazima tujiunge pamoja na tushirikiane kwa dhati ili kuifanikisha siku hii” Alisisitiza Nyangamale.
Awali viongozi wa mashirikisho ya Wasanii nchini Msule Jumanne (Sanaa za Ufundi), Samwel Mbwana (Sanaa za Muziki), Dennis Mango (Sanaa za Maonesho) na Biko wa Sanaa za Filamu walieleza namna wasanii walivyojipanga kushiriki siku hiyo na kusisitiza kwamba kila msanii nchini ajisikie furaha na heshima kushiriki siku hii muhimu kwao.
Siku ya msanii Tanzania inatarajiwa kuanza kuazimishwa kwa shamrashamra mbalimbali yakiwemo maonesho ya kazi za wasanii, semina na makongamano ya kujadili mustakabali wa sekta hiyo nchini kuanzia tarehe 7-11 Desemba mwaka 2015  na baadaye kilele chake tarehe 12 Desemba mwaka 2015 kwenye Ukumbi wa Blue Pearl uliko jengo la Ubungo Plaza Ubungo jijini Dar es Salaam.


IMETOLEWA NA KITENDO CHA HABARI NA MAWASILIANO, BASATA

No comments:

Post a Comment