Baadhi ya Washiriki wa Mkutano wa Wadau wa Zanzibar Press Club ZPC wakiwa katika Picha ya pamoja na Mgeni rasmi wa Mkutano huo Dkt. Aboubakar Rajab wakatikati waliokaa huko Hoteli ya Zanzibar Ocean mjini Zanzibar.
Picha na Makame Mshenga - Maelezo Zanzibar
Na Maelezo Zanzibar
[ZANZIBAR] Wanahabari wametakiwa kuendelea kutii Sheria zilizopo zinazoongoza mwenendo wa utoaji wa habari nchini, huku Taasisi za kihabari zikiendelea kufuatilia upatikanaji wa sheria Bora za habari zinazoendana na wakati uliopo.
Hayo yameelezwa na Katibu wa Tume ya Utangazaji Zanzibar Chande Omar alipokuwa akiwasilisha Mada katika Mkutano Mkuu wa Wadau wa Jumuiya ya Waandishi wa Habari Zanzibar ZPC uliofanyika ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar Ocean mjini Zanzibar.
Amesema licha ya kuwepo kwa baadhi ya Sheria za habari zilizopitwa na wakati, ni vyema Wanahabari kuziheshimu na kuzitii huku juhudi mbalimbali zikifanywa na Wadau kuondoa Sheria hizo.
Chande amefahamisha kuwa Taasisi kama Vile Baraza la Habari Tanzania, Tume ya Utangazaji na Jumuiya ya Waandishi wa Habari Zanzibar ZPC ni miongoni mwa Taasisi ambazo zinafanya kazi za kuwepo kwa Sheria zinaendana na wakati kwa maslahi mapana ya Taifa.
Aidha katika Mkutano huo uliojumuisha Washiriki kutoka Taasisi mbalimbali za Serikali na Binafsi maazimio mbalimbali yalipitishwa ikiwemo Wamiliki wa Vyombo vya Habari na Waaandishi kwa ujumla kuzingatia Weledi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Azimio jingine ni kuhakikisha kuwa Taasisi kama Vile Baraza la Habari Tanzania, Tume ya Utangazaji na Jumuiya ya Waandishi wa Habari Zanzibar ZPC zinashiriki kikamilifu katika kuhamasisha upatikanaji wa Maslahi bora kwa Wanahabari ili kuwaepusha kupokea Zawadi kutoka Vyanzo vya habari ambazo hupelekea kukiuka maadili yao.
Aidha wameazimia kujiepusha na Ushabiki wa Kisiasa ili kuepuka upendeleo wa habari wanazojitoa kwa jamii.
Mmoja wa Wachangiaji kutoka Jumuiya ya Wakulima Mpwapwa amewaomba Waandishi wa habari kuandika pia habari za watu wa shamba badala ya kuandika habari zinazohusu watu wa mijini pekee.
Ametoa mfano kwamba katika uchaguzi Mkuu uliopita habari zilizoandikwa zilihusu Watu wa Mijini ambapo kwa upande wa Vijijini Waandishi walishindwa kuonekana kwenda kuchukua habari.
Hata hivyo Washiriki wa Mkutano huo pia Waliafiki wazo hilo na kuazimia kufanya kazi kizalendo na kushirikisha makundi yote ya kijamii ikiwemo kuandika habari za Vijijini ili kuibua Fursa na changamoto zinazowakabili.
Akitoa hutuba ya Ufunguzi Mkuu wa Chuo cha Habari Zanzibar Dkt. Aboubakar Rajab kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari Utamaduni Utalii na Michezo Zanzibar Ally Mwinyikai alisisitiza wanahabari kuzingatia maadili ya kazi zao ili waheshimike katika jamii.
Amesema kukosekana kwa Maadili ya Habari hupelekea Migogoro mingi ikiwemo kuzalisha chuki na fitna miongoni mwa jamii husika.
Jumuiya ya Waandishi wa Habari Zanzibar hufanya Mkutano Mkuu wa Wadau wake kila mwaka na kujadili mada kulingana na wakati husika ambapo katika Mkutano huo Walijadili umuhimu wa Waandishi kuzingatia Maadili katika kupatikana uchaguzi huru na Wahaki.
Mkuu wa Chuo cha Habari Zanzibar Dkt. Aboubakar Rajab akitoa hutuba ya ufunguzi kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari Utamaduni Utalii na Michezo Zanzibar Ally Mwinyikai katika Mkutano Mkuu wa Wadau wa Jumuiya ya Waandishi wa Habari Zanzibar (ZPC) uliofanyika ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar Ocean mjini Zanzibar ambapo alisitiza wanahabari kuzingatia maadili ya kazi zao. Kulia ni Katibu wa Tume ya Utangazaji Zanzibar Chande Omar na kushoto ni Mwenyekiti wa ZPC Abdallah Mfaume.
Katibu wa Tume ya Utangazaji Zanzibar Chande akitoa Mada ya umuhimu wa kuzingatia Maadili kwa Wanahabari katika fani yao.
Mkulima kutoka kikundi cha Ushirika cha Bambi Mwaka Saburi akichangia katika Mkutano wa Wadau wa ZPC uliofanyika ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar Ocean mjini Zanzibar ambapo alishauri Wanahabari kuandika zaidi habari za Vijijini bada ya mijini pekee.
Makamu wa Rais wa Chama cha Siasa ADA-TADEA akichangia katika Mkutano wa Wadau wa Mkutano wa Wadau wa ZPC uliofanyika ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar Ocean mjini Zanzibar.
No comments:
Post a Comment