Friday, October 30, 2015

POLISI YAVAMIA KITUO CHA UKUSANYAJI TAARIFA CHA TACCEO NA KUKAMATA MAAFISA 36 PAMOJA NA VIFAA

Mtandao wa Asasi za Kiraia za Kuangalia chaguzi nchini jana ulipata pigo katika mwendelezo wake wa kukusanya taarifa juu ya mchakato wa uchaguzi mkuu wa 2015 kama unavyoendelea nchi nzima baada ya Jeshi la Polisi kuvamia kituo cha kukusanya taarifa kilichopo katika ofisi za Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ofisi ya Mbezi Beach. Tukio hilo lisilo la kawaida lilitokea Majira ya saa nane mchana baada ya polisi kufika kituoni hapo na kuwaweka wahusika wa kituo hicho wapatao 36 chini ya ulinzi na kuwashinikiza kusimamisha kazi na Kufungua mitambo bila kutoa sababu ya kufanya hivyo.

Akizungumza na waandishi wa habari Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC ambao ndio waratibu wa TACCEO Wakili Imelda – Lulu Urio amelaani vikali kitendo cha jeshi la polisi kuvamia na kusimamisha shughuli ambazo zinafanyika kwa mujibu wa sheria na pia zinafanyika kwa kibali kutoka Tume ya Uchaguzi ya Tanzania.”Kitendo hiki ni cha kidhalilishaji ukizingatia sisi( TACCEO)  tunafanya kazi kwa mujibu wa sheria na pia tuna vibali vya kufuatilia uchaguzi kwa mujibu wa sheria” Kituo chetu kinaaminika kwa kufanya kazi kwa maslahi ya umma wa Tanzania na hii sio mara ya kwanza kwa sisi kufuatilia uchaguzi za nchi hii hivyo tumeshangazwa na kusikitishwa na kitendo hiki cha polisi kuvamia bila taarifa” – Aliongeza.

Mkurugenzi wa Utetezi na Maboresho wa LHRC Wakili Harold Sungusia akizungumza kwa masikitiko katika eneo la tukio alisema “mpaka sasa hatujui kosa kwani tumekuwa tukifuatilia chaguzi mbali mbali toka kuanza kwa mfumo wa vyama vingi nchini na tumekuwa tukifuata sheria na taratibu zote zinazopaswa kama waangalizi na hata Tume ya Taifa ya Uchaguzi imetupa vitambulisho vya uangalizi kwa kutambua mchango na nafasi yetu”.

Hata hivyo sakata hilo bado linaendelea kwani wafanyakazi pamoja na vifaa vyao vya kazi ikiwemo kompyuta 27 pamoja na simu zao za mkononi ambavyo vimeshikiliwa na Jeshi la polisi likiongozwa na afisa mpelelezi wa Kituo cha Polisi cha Kawe aliyefahamika kwa jina la Mgonja. Wafanyakaizi wamefikishwa Makao Makuu ya Polisi jijini Dar es Salaam kwa uchunguzi zaidi.

No comments:

Post a Comment