MGOMBEA ubunge anayewakilisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) jimbo la Bunda mjini, mkoani Mara, Esther Bulaya anajivuna kuwa amefanikiwa kumdhibiti mpinzani wake mkubwa katika uchaguzi mkuu, Stephen Wassira.
Akizungumza na MwanahalisiOnline, Bulaya ambaye alikuwa mbunge wa Viti Maalum akitokea Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), amesema kwamba amedhoofisha ngome ya Wassira, ambaye amekuwa kiongozi serikalini tangu awamu ya kwanza ya Mwalimu Julius Nyerere.
“Kulikuwa na matukio ya mikutano yetu kuvamiwa, wafuasi wetu kuvamiwa na kubambikiziwa kesi, hata hivyo tulijipanga na kudhibiti huku tukishirikiana na Jeshi la Polisi,” anasema akizungumzia mikakati iliyopangwa kumkwamisha kukubalika kwa wananchi.
“Ninavyoongea na wewe gari yangu ipo Polisi kwa madai kuwa imehusika na uhalifu wa kutumia silaha, dereva wangu pia anashikiliwa lakini wananchi kwa hasira wamenipatia gari sita za kampeni,” anasema Bulaya aliyejiunga Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) baada ya kuhama CCM mara tu bunge lilipovunjwa.
Bulaya ambaye pia kitaaluma ni mwandishi wa habari, amesema mpaka jana ameshafanya kampeni katika Kata 14 za jimbo hilo huku akipita kila kijiji na kila kitongoji na sasa anatarajia kuanza awamu ya pili ya kampeni akiwa ameimarika zaidi.
Kuhusu upinzani anaokumbana nao kutoka kwa Wassira, Bulaya anasema “pamoja na mbinu chafu dhidi yangu nipo imara sana, ninamkabili kisawasawa na anakosa watu kwenye mikutano mingi.”
Jimbo la Bunda mjini ni moja ya majimbo yenye upinzani mkali likishikiliwa na Wassira ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano), aliyewahi kuwa NCCR-Mageuzi na kushinda ubunge kabla ya kuvuliwa na Mahakama Kuu kwa kosa la kununua kura. Alikuwa ameshindana na Joseph Warioba wa CCM.
#MwanahalisiOnline
No comments:
Post a Comment