WANANCHI wa Kijiji cha Lowa katika kata ya Nyandekwa Wilayani Kahama Mkoani Shinynga jana wamejitokeza na kuchoma moto Bendera za Chama cha Mapinduzi pamoja na kadi kutokana na Chama cha Mapinduzi Wilaya kukata jina la Mshindi wa kura za maoni ngazi ya udiwani na kumrudisha mshindi wa pili.
Tukio hilo limetokea majira ya saa saba mchana wakati Wananchi hao waliopo andamana hadi katika ofisi za kijiji wakidai kuwa jina la Mgombea Udiwani katika kata hiyo Menad James alikuwa ni mshindi halali katika kinyanganyiro hicho baada ya kumshinda Kurwa Kadebe kwa kura tano katika mchuano huo.
Wakiongea na Waandishi wa Habari Wananchi walisema kuwa katika mchuano huo Menad James alipata jumla ya kura 724 huku Mpinzani wakewa karibu ambaye ni Diwani anayetetea kiti chake Kurwa Kadebe akipata jumla ya kura 719.
“Tunashangaa kusikia kuwa jina la Mshindi wa kwanza katika mchuano huo ambaye ni Menad James aliyepata kura 724 likikatwa na kurudi jina la Kurwa Kadebe aliyepata jumla ya kura 719 ndio maana tumeamua kuchoma Bendera za CCM pamoja na Kadi zake na sasa tumehamia CHADEMA”, Alisema Anna Ngasa Mkazi wa Lowa.
Pia wakazi hao walimtuhumu Diwani huyo wa kipindi kilichopita kuwa hakuweza kuleta maendeleo katika kata hiyo kwani alikuwa hasomi mapato na matumizi ya fedha za maendeleo ya kata na kuongeza kuwa michango yote iliyokuwa ikichangwa na Wananchi kutoka katika Vitongoji 27 katika kata hiyo hazikutumika ipasavyo.
“Tumechangishwa sama michango katika kata hii hususani ile ya ujenzi wa Maabara kila kila kitongoji tulichanga kiasi cha shilingi 300,000 na kupatikana jumla ya shilingi milioni nane 8.1 lakini hatujui fedha hizo ziko wapi ingawa tuliambiwa kuwa fedha za ujenzi wa maabara zilitolewa na Mgodi wa Buzwagi kwa ajili ya ukamilishaji”,Aliongeza John Maganga.
Aidha wananchi hao walisema kuwa kama matokeo hayatabadilishwa basi Mshindi huyo wa Pili katika kura za maoni asije katika kata hiyo kufanya kampeni kwani watamkamata na kumchulia hatua kali kutokana na kufuja fedha zao za maendeleo walizokuwa wakichanga kwa ajili ya maendeleo ya kata yao.
Pia wananchi hao walitaka kujua kuwa ni utaratibu gani ulitumikam katika kumpata mshindi wa kura hizo za maoni na kuongeza kuwa kwa utaratibu huo ni bora Chama kikawa kinachagua Mgombea huko huko na kuwaletea kuliko kupoteza muda wa kumchangua kiongozi ambaye hakubaliki ndani ya chama huku kwa Wananchi akikubalika.
Katibu wa CCM Wilaya ya Kahama Alexandrina Katabi alipotakiwa kutoa ufafanuzi juu ya tuhuma hizo alisema kuwa ukatwaji wa majina ya Wagombea ni tendo la utaratibu wa Chama cha Mapinduzi sehemu zote hapa nchini.
Nae Katibu Mwnezi wa Mkoa CCM Mkoa wa Shinyanga Emmanuely Mlimandago alisema kuwa suala hilo ni makosa yaliyofanywa na uongozi wa Chama hicho ndani ya Wilaya na kumtaka katibu wa CCM Wilaya ya Kahama kulitolea ufumbuzi suala hilo.
No comments:
Post a Comment