Sunday, August 30, 2015

RIPOTI MAALUM: MABADILIKO YA TABIANCHI YALIVYOATHIRI ZAO LA MPUNGA MKOANI MOROGORO KWA VIRUSI VYA UGONJWA WA KIMYANGU

Mwandishi wa makala hii Andrew Chale akishuhudia mpunga huoMwandishi wa Makala haya, Andrew Chale, ambaye pia ni Mhariri wa mtandao (blog) ya modewjiblog.com, akiwa katika moja ya shamba la Mpunga  la Mkulima Bwana Nguji, Kijiji cha Mtimbira, Wilayani Ulaanga  Mkoa wa Morogoro -Tanzania hivi karibuni.
Na Andrew Chale, Modewjiblog
[Morogoro, Tanzania] Zikiwa zimebaki siku zaidi ya 90, kuelekea mkutano mkuu wa 21 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Mabadiriko ya Nchi (COP21) unaotarajiwa kufanyika Paris , Ufaransa, Desemba mwaka huu. Dulu za kitafiti  zinaeleza kuwa, Wakulima wa  Mkoa wa Morogoro  wanakabiriwa na janga kubwa la ugonjwa wa wa ‘Kimyangu’  ambapo virusi  kitaalamu vikijulikana kama (Rice Yellow Mottle Virus (RYMV)  ushambulia mpunga shambani.
Kwa mujibu wa Afisa Kilimo Bwana. Joseph Nyange katika  Wilaya ya Ulanga,  ambaye alifanya mahojiano na mwandishi wa mtandao huu katika Tarafa ya Mtimbira iliyopo Mkoani Morogoro, anakili tatizo hilo  kwa mwaka huu limekuwa kubwa hasa kutokana na mabadiliko ya tabianchi yanayoendelea kuikumba Tanzania kila wakati.
Bwana Nyange anaeleza kuwa,  tatizo hilo la virusi vya RYMV  ama Kimyangu, kushambulia mazao ya wakulima katika ukanda huo, ni baada ya mwaka jana na mwaka huu kutokea mabadiliko ya unyeshaji wa mvua zaidi ya mazoea ya nyuma.
“Tatizo hili la ugonjwa wa Kimyangu kwenye mipunga, limeweza kuathiri wakulima wengi na hali hii imetokea mwaka huu kwa kiwango kikubwa sana. Baada ya kukosekana mvua ya uhakika iliyosababishwa na tabianchi” anasema Bwana Nyange.
Anaongeza kuwa, ugonjwa huo unakuwa mkubwa sana na hasa kipindi ambacho kunakuwa na jua kali hivyo mashamba mengi yanakumbwa na athari hiyo ya Kimyangu.  Athari hizo zinakuwa kilio kikubwa kwa wakulima kwani hadi sasa  ugonjwa huo haujapatiwa dawa licha ya wataalam kuendelea kufanya utafiti  huku wakulima nao wakiendelea kujaribu kutibu mashamba yao kwa kutumia madawa ya kienyeji.
Hata hivyo,  Bwana Shamba huyo, ana kili kuwa, kuwa  licha ya Ugonjwa huo kuwa si mgeni sana kwa ukanda huo, Kwa Tanzania upo karibu sehemu mbalimbali huku tofauti yake ni namna ya uibukaji wake.
“Ugonjwa huu upo maeneo mbalimbali ya Tanzania hasa sehemu zinazolimwa mpunga kwa wingi ndani ya Tanzania na hata nje ya Tanzania hasa kwa nchi hizi za jangwa la Sahara. Kwa kwetu huku mwaka huu tumeathiriwa na mabadiliko ya tabianchi, kwani kukatika  ghafla kwa mvua na kupelekea jua kuwa kali na athari pia imekuwa kali” anaeleza Bwana Shamba huyo.
Mvua zilivyo athiri:
Bwana Shamba Joseph Nyange anaeleza kuwa, kwa mwaka jana na mwaka huu mvua zilichelewa na hata zilipokuja zilinyesha  kwa kiwango kidogo tofauti na viwango vya mvua vilivyozoeleka hapo awali. Lakini mvua hiyo hiyo iliyochelewa kunyesha na hata kuwa kwa kiwango kidogo, ilikatika ghafla na kusababisha ugonjwa huo kuwa mkubwa huku akibainisha kuwa, kwa mwaka huu pekee mvua ilikatika ghafla mnamo mwezi wa tano na baada ya hapo haikunyesha tena hadi sasa.
Hata hivyo, ametaja vyanzo vinavyopelekea kwa mabadiliko ya tabianchi  katika maeneo hayo ni pamoja na ukataji wa miti hovyo hasa katika vyanzo vya maji, Kuingia kwa wafugaji wengi katika maeneo ya ardhi yenye rutuba ya kilimo na upanuzi wa mashamba ambapo watu wengi kwa sasa wameweza kulima hadi milimani mazao ambayo yanafyonza maji mengi  ambapo shughuli hizo za kibanadamu ndizo zinazopelekea kutotabirika kwa misimu ya mvua ya uhakika na hata kusababisha ugonjwa huo kuendelea kuwa sugu katika mazao ya mpunga.
Utafiti uliofanywa na mwandishi wa mtandao huu, umebaini kuwa, Mkulima mmoja ana uwezo wa kupata gunia 10 hadi 15, kwa shamba la hekari moja, ambaye analima kilimo cha kienyeji, Lakini kutokana na ugonjwa huo wa Kimyangu, wakulima wengi wamevuna katika shamba kama hilo la hekari moja, wapo waliovuna gunia moja na wapo waliovuna magunia matano na wapo waliokosa kabisa kwa shamba zima kuathiriwa na ugonjwa.
(Inaelezwa kuwa endapo Mkulima wa kawaida, atalima mpunga kwa kutumia kilimo cha kisasa  katika shamba la hekari moja, ana uwezo wa kupata magunia 18 hadi 25).
Inaelezwa kuwa, ugonjwa huo wa Kimyangu, mpunga shambani unakuwa katika hali ya kubabuka sana, huku ukiuona shambani kwa mbali ukionekana kama upo salama, lakini ukiuvuna ndipo utagundua kuwa umeathirika na virusi hivyo vya RYMV.
kk;aMmoja wa wakulima katika Kijiji cha Mtimbira, Bwana Daraja Daraaja  akiwa pembeni mwa shamba lake huku kwa kiasi kikubwa mpunga ulioungua kutokana na mabadiliko ya tabianchi na kupelekea ugonjwa wa virusi vya RYMV ama ugonjwa wa Kimyangu. (Picha na Andrew Chale, modewjiblog).

Mashuhuda:

Baadhi ya wakulima walizungumza na mwandishi wa mtandao huu katika maeneo kadhaa ya Wilaya za Mahenge, Ulanga na Kilombero wameweka wazi kuwa,  mabadiliko ya tabianchi wamewaathiri kwa kiwango kikubwa huku na kushindwa la kufanya licha ya kutegemea kilimo kama mtaji wa kujipatia pesa na chakula.
Hivyo kwa kutokea ugonjwa huo kwa kiwango kikubwa umewashangaza sana na kushindwa kutojua la kufanya kwa msimu wa kilimo hapo baadae kwani  kilimo kikuu kwao ni zao la mpunga.
(Kimyanga ni kwa Kiswahili cha kawaida au Kimyangu  kwa lugha ya Kipogolo, ambao ni kabila kubwa katika maeneo hayo ya Wilaya za Ulanga, Mahenge, Kilombero na maeneo mengine ndani ya Mkoa huo wa Morogoro).
 “Endapo hakuna ugonjwa huu wa Kimyangu,  huko nyuma tumevuna magunia mengi tu  lakini sasa kila mmoja analia hali imekuwa ngumu, wengine tulikopa  vitu  na tulitegemea baada ya kuvuna mpunga turejeshe lakini hali imekua kinyume” anasema Samson Mwenda, Mkazi wa Mahenge.
Kwa upande wake, William Sijombele mkazi wa Mtimbila anaeleza kuwa,  elimu ndogo ya kutojua baadhi ya mambo ndio inayopelekea tatizo hilo kuwa kubwa kila mwaka kwani wakulima wengi wamekuwa wakiendeleza shughuli nyingi mbadala wa kilimo hali inayochangia athari za mabadiliko hayo.
“Utakuta Mkulima ana jishughulisha na kilimo hapo hapo ana mifugo. Mkulima huyo huyo anajishughulisha na biashara ikiwemo ya mbao ama uchoaji wa mikaa hali ambayo anasababisha athari kubwa ya mabadiliko ya tabianchi. Haya yote hakuna mtu wa kuingilia kati si Serikali si wanakijiji wengi wanajiona wapo juu ya sheria” anasema Mzee Sijombele.
Kwa upande wake mkazi wa Wilaya ya Ulanga, kijiji cha Mtimbira, Bwana. Daniel Nguji anabainisha kuwa,  yeye kwenye shamba lake la hekari tano, alitegea angepata magunia zaidi ya 50, lakini  baada ya kutokea ugonjwa huo wa Kimyangu, ameweza kuambulia magunia machache kiasi cha kupata athara kubwa.
“Kuliandaa shamba, upandaji na kuulinda mpunga shambani hadi kufikia hatua ya kuvuna,  inagharimu pesa nyingi sana.  Huu ugonjwa wa mpunga umenitia athara kubwa tunaomba wataalamu watupatie dawa ilikukabiliana na ugonjwa huu” anaeleza Nguji.
(Kwa mauzo: Mtimbira Gunia moja la Mpunga wanauza kuanzia kiasi cha Sh.60,000, hii ikiwa ni gunia la debe Saba, yaani debe moja la Mpunga likiwa linauzwa kwa Sh. 8000.)
mpunga huo unavyoonekanaMpunga huo unavyoonekana wakati wa kufikia muda wa kuvuna, ukiwa umekauka kutokana na kushambuliwa na ugonjwa wa virusi vya RYMV ama ugonjwa wa Kimyangu. kama unavyoonekana katika moja ya mashamba katika kijiji cha Mtimbira, Ullanga, Morogoro, Tanzania. (Picha na Andrew Chale, modewjiblog).
images
Mpunga huo ukiwa katika hatua ya kukomaa shambani huku tayari virusi vya ugonjwa wa RYMV ama Kimyangu ukiwa umeshambulia. (Picha kwa hisani ya mtandao wa:www.agriskmanagementforum.org)
Rice yellow mottle virus, computer artwork.
Rice yellow mottle virus, computer artwork.
Aina hiyo ya virusi  ya RYMV, vinavyosababisha ugonjwa wa Kimyangu
MRMpunga ukiwa umefikia steji ya mwisho ya kuungua shambani baada ya kuathiriwa na virusi vya  RYMV ama ugonjwa wa Kimyangu.
Kilimo Tanzania:
Kwa mujibu wa  Tovuti Kuu ya Serikali (Website):http://www.tanzania.go.tz/home/pages/92
Kilimo ni msingi wa uchumi wa Tanzania. Kinachangia kiasi cha nusu ya pato la taifa. Robo tatu ya bidhaa zinazouzwa nchi za nje, kinachangia asilimia 95 ya mahitaji ya chakula nchini, kinachangia 25.7% ya GDP na 30.9% ya fedha za kigeni, hutoa ajira kwa 75% ya watanzania, bajeti ya serikali inayotengwa kwa kilimo imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka, hivi sasa imefikia zaidi ya asilimia 7.
Kilimo-cha-mpunga
Kilimo cha Mpunga kinavyoonekana nchini Tanzania pichani…
Ripoti hii imeandaliwa na Andrew Chale, Mwandishi wa Habari na Mhariri wa mtandao (blog) ya modewjiblog.com  Tanzania. ( Anuani : +255719076376 au barua pepe: andrewchale@gmail.com).
cfi logo
Makala haya yamefadhiliwa na kwa ufadhili wa Shirila la ( CFI)  la nchini Ufaransa, chini ya mradi wa Medias 21 Africa & Asia.
CFI, iliandaa mafunzo haya maalum ikiwa ni juhudi za kutoa elimu ya mabadiliko ya tabianchi kuelekea  mkutano wa kimataifa wa mazingira COP21, utakaonyika nchini Ufaransa mwishoni mwa  mwaka huu.
projet_image_8 (2)Logo ya mradi..
#(Picha na modewjiblog).

No comments:

Post a Comment