Friday, May 8, 2015

MKUU WA MAJESHI BURUNDI AKEMEA WANASIASA

 Mkuu wa majeshi ya Burundi Meja Jenerali Prime Niyongabo

Mkuu wa majeshi nchini Burundi Meja Jenerali Prime Niyongabo ametoa wito kwa wanasiasa kutotumia jeshi la taifa kwa manufaa yao ya kisiasa.
Jenerali Niyongabo amekariri tangazo lililotolewa na waziri wa ulinzi Jumamosi kuwa jeshi la nchi hiyo litahakikisha kuwa mkataba wa Arusha umetekelezwa kikamilifu na kuwa jeshi hilo halitumiwi na mtu au chama chochote cha kisiasa.

Kuhusiana na maandamano yanayoendelea, mkuu huyo wa jeshi amesema kuwa maandamano hayo sio halali na wanaichi wanapaswa kutumia mbinu za sheria zilizopo kutatua mizozo yao.
Polisi wa kuzuia ghasia wakikabiliana na waandamanaji katika mitaa ya Bujumbura nchini Burundi

Wakati huo huo Meja Jenerali Niyongabo amesema jeshi hilo litasalia kuwa lenye nidhamu ya hali ya juu na tiifu kwa taifa la Burundi na wala sio kwa mwanasiasa yeyote.

Ameongeza kusema kufikia sasa jeshi limefanya kazi nzuri kuhakikisha kuwepo kwa usalama nchini Burundi na katika mataifa mengine wanakohudumu katika vikosi vya Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika.

Mkuu huyo wa majeshi amesema wanajeshi wataendelea kushirikiana na polisi kushika doria ili kuhakikisha amani na utulivu vinakuwepo nchini Burundi.

Huku hayo yakijitokeza muungano wa upinzani umesema kuwa maandamano yataendelea siku ya Jumatatu baada ya mapunziko ya siku mbili.

Upinzani umepinga hatua ya rais Pierre Nkurunziza ya kuwania muhula wa tatu kama rais.
Wanafunzi wa vyuo vikuu nchini Burundi wakisubiri kuondoka baada ya vyuo vikuu kufungwa kufuatia maandamano ya kupinga Rais Pierre Nkurunziza kuteuliwa na chama chake cha CNDD-FDD kugombea muhula wa tatu
Viongozi wa upinzani wanasema kuwa Rais Nkurunziza ni sharti atekeleze mkataba wa Arusha ambao ulimaliza mapigano ya wenyewe kwa wenyewe nchini Burundi.
Lakini chama tawala cha CNDD FDD kimepinga madai hayo na kusema kuwa Rais Nkurunziza anatumikia muhula wake wa kwanza kwa sababu, miaka mitano ya kwanza ilikuwa kipindi cha mpito na hakuchaguliwa na raia kama inavyohitajika kisheria.
Wakaazi wa mji mkuu wa Bujumbura wameshuhudia uhaba mkubwa wa bidhaa muhimu kama vile petroli, na kadi za simu za muda wa mazungumzo huku kukiwa na misururu mirefu katika vituo vya kununua mafuta.
Idadi kubwa ya raia wa Burundi wamekimbilia nchi jirani kwa hofu ya kuzuka mapigano zaidi.

No comments:

Post a Comment